Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Ileje.
SERIKALI imetangaza rasmi kuanza kwa ujenzi wa barabara ya lami ya Isongole II – Ibungu – Isoko yenye urefu wa kilomita 52.419, huku mkandarasi wa mradi huo, kampuni ya China Road and Bridge Corporation (CRBC), akitambulishwa kwa wananchi.
Akizungumza Machi 7, 2025 na wananchi wa kata ya Isongole, Wilayani Ileje, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, alisema kuwa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeidhinisha na kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi huo, licha ya madai ya upotoshaji kutoka kwa baadhi ya watu waliodai kuwa mradi huo hautatekelezwa.
“Wale waliokuwa hawaamini na kuwapotosha wananchi vijiweni kuwa barabara hii haitajengwa sasa wamekosa ajenda na hata kama wataibuka na upotoshaji mwingine hawatawez ,” alisema Kasekenya.

Aliongeza kuwa, tayari serikali imetoa shilingi bilioni 7.2 kama malipo ya awali kwa mkandarasi, huku gharama ya jumla ya mradi huo ikifikia zaidi ya shilingi bilioni 75.
Naibu Waziri Kasekenya, ambaye pia ni Mbunge wa Ileje, alisisitiza kuwa uboreshaji wa miundombinu, hususan barabara, ni kichocheo kikubwa cha maendeleo, hasa kwa vijana.
“Leo sio uzinduzi rasmi wa mradi huu, kwani Waziri wangu atakuja kufanya kazi hiyo, lakini mimi kama Naibu Waziri mwenye dhamana na mbunge wa hapa, nimekuja kuhakikisha kuwa mkandarasi yuko tayari kuanza kazi na kumtambulisha kwenu,” alisema.

Aidha, aliwataka wananchi wa Ileje kuacha kusikiliza propaganda za kisiasa na badala yake waunge mkono juhudi za maendeleo zinazoendelea kufanyika.
Alieleza kuwa vijana wa eneo hilo watapewa kipaumbele katika ajira zitakazotokana na mradi huo, akitoa maelekezo kwa wasimamizi wa mradi kuhakikisha kuwa kazi zote zisizo za kitaalamu zinapewa kwa vijana wa Ileje.
“Ninawaagiza wasimamizi wa mradi huu kuhakikisha kuwa kazi zote zisizo za kitaalamu zinatolewa kwa vijana wa Ileje ili waweze kunufaika na fursa hii,” alisisitiza.
Pia alibainisha kuwa mkandarasi amepewa maelekezo madhubuti ya kufuata viwango vilivyoainishwa kwenye mkataba wa ujenzi, pamoja na kuheshimu taratibu, mila na desturi za wakazi wa Ileje.
Akizungumza kwa niaba ya Mkandarasi wa kampuni ya China Road and Bridge Cooperation ya China (CRBC) ambaye ni
Meneja mradi, Wang Zhing, alisema mradi huo
unatekelezwa kwa miezi 28 na kwamba utaanza rasmi mwezi Mei 2025 na kwamba kinachifanyika sasa ni kazi za ukusanyaji wa vifaa eneo la mradi, kufuatiwa na uwekaji wa alama barabarani, pamoja na matayarisho ya kambi.

Kwa upande wake, Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ileje, Maoni Mbuba, alisema kuwa mradi huo utafungua fursa nyingi kwa wananchi wa Ileje, ikiwa ni hatua kubwa ya maendeleo kwa wilaya hiyo.
“Kukamilika kwa barabara hii kutarahisisha usafiri na biashara na kuunganisha Wilaya ya Ileje na wilayani Kyela, Mkoa wa Mbeya na kuimarisha biashara za mpakani kati ya Tanzania na Malawi, katika mipaka ya Isongole na Kasumulu” alisema Mbuba.
Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Irene Limo, ambaye ni Ofisa Tarafa ya Bulambya, alisisitiza kuwa serikali imekuwa mstari wa mbele katika kupeleka fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo wilayani humo.
Awali, Mwenyekiti wa Kijiji cha Isongole, Kalela Masimbi, alitoa ombi kwa serikali na mbunge Kasekenya kuhakikisha kuwa wananchi wa eneo hilo wanapewa kipaumbele katika ajira zinazotokana na ujenzi wa barabara hiyo, ili waweze kunufaika kiuchumi badala ya kubaki watazamaji.
Nao wananchi wa Isongole wamepokea kwa furaha tangazo la kuanza kwa ujenzi wa barabara hiyo, wakisema kuwa itawaondolea changamoto za usafiri na kusaidia kukuza biashara zao.


More Stories
Rais Dkt.Samia mgeni rasmi Tuzo za Waandishi wa habari za Maendeleo
Wawekezaji watakiwa kuwekeza kwa tija
Mkazi Lushoto adai kutishiwa kuuawa,atoa kilio chake kwa timu ya Mama Samia