January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ujazaji wa fomu za afya sasa ni kwa mtandao

Na Yusph Digosi, TimesMajira Online, Dar es Salaam,

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imebadili utaratibu wa ujazaji fomu ya ufuatiliaji wa afya ya msafiri yenye lengo la kuboresha afya ya umma.

Kwa mujibu wa tangazo lilitolewa kwa vyonbo vya habari, utaratibu huo ni kwa mujibu wa Sheria ya Afya ya Umma ya mwaka 2009, ambapo utekelezwaji wake umeanza rasmi Aprili 25, mwaka huu.

Utaratibu wa awali ulikuwa msafiri anajaza fomu baada ya kuwasili sasa atajaza fomu hiyo kwa mfumo wa mtandao saa 24 kabla ya kusafiri.

Aidha tangazo hilo limesema kuwa msafiri atajaza fomu katika tovuti ya Wizara ya Afya ambapo ataweka taarifa zote muhimu kama vile sehemu anayotoka na anayokwenda, siku ya kusafiri, aina ya usafiri, namba ya kiti, muda atakaowasili pamoja na taarifa zote muhimu kuhusu mwenendo wa afya yake.

Pamoja na taarifa hizo pia msafiri ametakiwa kuambatanisha vielelezo ambavyo ni pamoja na hati ya kusafiria (passport) pamoja na tiketi.

Baada ya kukamilisha taratibu hizo, mhusika ataiwasilisha fomu hiyo katika dawati la afya ili kupatiwa huduma na kukamilisha taratibu nyingine.

Taarifa hiyo imewashauri wote watakaotumia mfumo huo kujaza taarifa za kweli kwani kuweka taarifa za uongo ni kinyume cha sheria ya Afya ya umma ya 2009, hivyo watachukuliwa hatua kisheria

Wadau mbalimbali wamekuwa wakitoa maoni katika ukurasa wa Wizara ambapo wameonesha kuguswa na jinsi Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyojipanga kwa kuweka mfumo huo wenye nia ya kuhakikisha usalama na kulinda afya za raia wake.

Kizito Kipangala ni miongoni mwa waliopongeza Wizara ya Afya huku akiandika, “haya ni mafanikio katika Wizara ya Afya hasa kupunguza msongamano na usumbufu usio wa lazima”