September 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ugonjwa Polio watokomezwa kwa kiwango kikubwa Katavi

Na George Mwigulu,TimesMajira Online,Katavi

UGONJWA wa Polio umetokomezwa kwa kiwango kikubwa katika Mkoani Katavi kufutia Serikali kuongeza idadi ya vituo vya kutolea huduma ya chanjo mbalimbali za kujikinga na maambukizi ya magonjwa ya milipuko

Hayo yamesemwa na Dkt.Taphinez Machibya mratibu wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko katika hosptali teuli ya rufaa ya Mkoa wa Katavi,wakati alipokuwa akizungumza na wandishi wa Habari juu ya jitihada zilizofanyika na serikali ya kupambana na magonjwa ya mlipuko.

Ameeleza kuwa hali ya ongezeko la vituo vya kutolea huduma vilivyojengwa kwenye Mkoa wa Katavi vimesaidia upatikanaji wa huduma za afya ambapo wazazi na walenzi wamekuwa wakipatia ushauri wa kitabibu hasa kwa wamama wajawazito kuzingatia kanuni za afya hata pale watoto wanapozaliwa.

‘’…chanjo hizi zinazotolewa kwa watoto zimesaidia kupunguza vifo kwa kiasi kikubwa hasa vya watoto wadogo vilivyokuwa vikisababishwa na magojwa ya mlipuko wa polio na kupelekea ulemavu’’ amesisitiza Dkt. Machibya.

Amebainisha kuwa hapo awali idadi ya vituo vya kutolea huduma za chanjo kwenye Halmashauri mbalimbali za mkoa huo vilikuwa ni vichache tofauti hali ya sasa ambapo idadi ya kutolea huduma imeongezeka.

Amefafanua kwa mfano hapo awali katika halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe kulikuwa na vituo vya afya viwili vya Usevya na Mamba na idadi za zahanati chache wakati kwa sasa wana Hospitali moja ,vituo vya afya viwili na kingine cha maji moto kimeanza kujengwa hali ambayo imefanya vituo vya kutolea huduma kufikia kumi na tatu kwa sasa.

Dkt. Mchibya amesema kuwa kuongezeka kwa vituo hivyo kumesaidia kuwafanya wananchi kusogezewa huduma karibu zaidi tofauti na hapo awali ambapo watu walikuwa wakisafiri umali mrefu zaidi kutafuta huduma ya chanjo.

Magonjwa ambayo hapo awali yalikuwa yakisumbua aliyataja baadhi ya magonjwa hayo yalikuwa yakisumbua kuwa ni ugonjwa wa polio,surua,kuharisha na kutapika.

Naye Mkazi wa Mtaa wa Misukumilo Manispaa ya Mpanda Cosmas Tungu amesema kuwa wanawake wajawazito walikuwa wanapata shida wa kwenda kwenye vituo vya kutolea afya kwa kutembea umbali mrefu jambo ambalo lilizorotesha juhudi za kupatia elimu na ushauri wa kitabibu.

Kushindwa kwa kupatiwa elimu huko kulisababisha wazazi kukosa utaalamu wa kumlea watoto vizuri katika kumhudumia kama vile lishe bora na wakati mwingine kupuuza chanjo kwa imani potofu.

Paulina Shindika amesema kuwa wanawake wengine baada ya upatikanaji wa huduma ya afya kwenye maeneo yao wameweza kujitokeza kwa wingi kwenye huduma za wamama wajawazito na kuzinagatia kanuni za afya.

Hata hivyo amewaomba kinababa kuweza kuambatana nao pindi wanapokuwa wajawazito na hata wanapojifungua kwani kutasaidia kujenga uelewa wa pamoja kama familia namna ya kumlea mtoto na kumkinga na magonjwa ya mlipuko kama vile polio na surua.