November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ufugaji wa nzi kwenye madampo umeonekana kuwa tija nchini

Na Agnes Alcardo,Timesmajira online, Dar es Salaam

UFUGAJI wa wadudu aina ya nzi wanaopatikana kwenye madampo ya taka, umekuwa na tija nchini, hususani katika uzalishaji wa mbolea aina ya samadi pamoja na chakula cha mifugo.

Kauli hiyo imetolewa leo na Msimamizi wa Kiwanda cha Chanzi, kinachoshughulika na chakula kinachotokana na nzi Nicko Nyamanga, wakati akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari juu ya mafanikio yanayopatikana kwenye ufugaji wa inzi.

Nyamanga amesema, kuwepo kwa mradi huo kunasaidia kuimarisha, kuboresha afya za mifugo wakiwemo kuku kutokana na protini inayopatina kupitia chakula cha kuku.

Aidha, Mkurugenzi wa Tafiti na Mazingira kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira(NEMC), Dkt Menan Jangu amesema kuwepo kwa kiwanda kama hicho inaleta faida ya kupunguza taka ngumu zinazozalishwa katika madampo na kupelekea kuwepo kwa upatikanaji wa mbolea ya asili.

“Naomba serikali kuunga mkono jitihada hizi zilizofanywa na wadau hawa wa sekta binafsi katika kuhakikisha inasaidia kupunguza kuzagaa kwa taka ngumu, ambazo madampo mengi yameonekana kuzidiwa kupokea taka hizo,”a mesema Jangu.

Kiwanda cha kufuga Inzi kilianzishwa mwaka 2019 Jijini Arusha na kwa upande wa Dar es salaam kilianzishwa mwaka jana na kimetoa ajira kwa vijana wapatao 16 ambapo mpaka hivi sasa vijana hao wanaendelea kufanya kazi katika kiwanda hicho.