Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam
BARAZA la Mitihani la Tanzania (NECTA) limetangaza matokeo ya mtihani wa darasa la nne na kidato cha pili huku kukiwa na ongezeko la ufaulu kwa asilimia 2.90 kwa wanafunzi waliopata fursa ya kuendelea na darasa la tano. Hata hivyo, jumla ya wanafunzi 151 wamefutiwa matokeo kwa kushiriki udanganyifu na kuandika matusi kwenye karatasi zao za majibu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania, Dkt. Said Mohamed, alithibitisha kwamba matokeo ya wanafunzi 105 wa darasa la nne na 46 wa kidato cha pili yamefutwa kutokana na udanganyifu. Alisema hatua hiyo imechukuliwa kwa mujibu wa kifungu cha 5(2)(j) cha Sheria ya Baraza la Mitihani, sura ya 107, pamoja na kifungu cha 30(2)(b) cha Kanuni za Mitihani za Mwaka 2016.
Dkt. Mohamed alisema kuwa katika wanafunzi hao waliobainika kufanya udanganyifu, 100 ni kutoka darasa la nne ambapo 98 walifanya udanganyifu na 5 waliandika matusi kwenye karatasi zao. Aidha, kwa upande wa kidato cha pili, 41 walibainika kufanya udanganyifu na 5 walifanya hivyo kwa kuandika matusi.
“Kati ya wanafunzi 100 wa darasa la nne waliopoteza matokeo, 98 ni watoto wa muda mrefu na walimu wakuu walikuwa wanawaandaa wanafunzi wenzao kutoka darasa la tatu, tano na sita kufanya mitihani kwa maslahi yao binafsi,” alifafanua Dkt. Mohamed.
Katika hatua nyingine, Baraza la Mitihani limelifunga Kituo cha Upimaji na Mitihani ya Taifa cha GoodWill kilichopo mkoani Arusha, baada ya kuthibitika kwamba Mkuu wa Shule na baadhi ya walimu walihusika katika udanganyifu kwa lengo la kuwasaidia wanafunzi.
Dkt. Mohamed alisema kwamba kituo hicho kilijaribu kuwarubuni wasimamizi na askari wa mitihani mnamo Oktoba 28 na 29, 2024, lakini walikosa mafanikio. Baada ya kushindwa, walibuni mbinu mbadala kwa kupanga wanafunzi kupata majibu kupitia chooni.
“Kwa kuwa kituo hicho kilikiuka maadili na sheria za mitihani, tumeamua kuliwekea kifungo na pia tutawasilisha mapendekezo kwa Kamishna wa Elimu ili kufutiwa usajili wake kabisa, kwani hakistahili kuendelea kuwa Shule,” alisisitiza Dkt. Mohamed.
Kuhusu matokeo ya darasa la nne, Dkt. Mohamed alisema kuwa jumla ya wanafunzi 1,320,227 kati ya 1,530,805 (asilimia 86.24) wamefaulu na watakuwa na fursa ya kujiunga na darasa la tano mwaka 2025. Hii ni ongezeko la asilimia 2.90 ikilinganishwa na mwaka 2023 ambapo wanafunzi 1,287,934 (asilimia 83.34) walifaulu.
Kwa upande wa matokeo ya kidato cha pili, Dkt. Mohamed alisema kuwa jumla ya wanafunzi 680,574 kati ya 796,825 (asilimia 85.41) wamefaulu na wataendelea na kidato cha tatu. Ufaulu huu pia umeonyesha ongezeko dogo la asilimia 0.10 ikilinganishwa na mwaka 2023, ambapo wanafunzi 592,741 (asilimia 85.31) walifaulu.
Katika kundi la wanafunzi waliofaulu kidato cha pili, wasichana ni 367,457 (asilimia 83.99) na wavulana ni 313,117 (asilimia 87.13), hivyo wavulana wameonyesha ufaulu bora zaidi kuliko wasichana.
“Kwa ujumla, matokeo haya yanaonyesha ongezeko la ufaulu na ufanisi wa mifumo ya upimaji wa kitaifa, ingawa bado kuna changamoto za udanganyifu ambazo tunendelea kukabiliana nazo kwa nguvu zote,” alisisitiza Dkt. Mohamed. Baraza la Mitihani la Tanzania linatoa wito kwa wadau wote wa elimu kuendelea kushirikiana na kuliunga mkono katika kuhakikisha mitihani inakuwa na hadhi na uadilifu, na kwamba hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka sheria na taratibu za mitihani.
More Stories
Maofisa Watendaji watakiwa kufanya kazi kwa weledi
Muhoji Sekondari kumaliza changamoto ya umbali kwa wanafunzi Musoma vijijini
Tanzania mwenyeji mkutano wa nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika