December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UDSM wajidhatiti mradi wa utunzaji nafaka

Na Hadija Bagasha, Timesmajira Online,Tanga

Chuo Kikuu cha Dar -es-Salaam (UDSM) kimesema kimejidhatiti kwenye miradi mbalimbali ikiwemo ya utunzaji wa nafaka uliofanywa kwa utafiti wa wanafunzi na walimu kwa lengo la kuwawezesha wananchi kutunza nafaka zisishambuliwe na wadudu.

Lakini pia chuo hicho kimekuja na mfumo wa kuangalia visababishi vya sumu kuvu inayozalishwa na fangasi na yenye madhara ya kiafya na kiuchumi ikiwemo kusababisha maradhi ya saratani ya ini na udumavu kwa watoto huku kwa upande wa uchumi ikisababisha kushuka kwa mazao ya nafaka.

Mkuu wa Mawasiliano na Masoko wa UDSM Dkt. Dotto Kuhenga ameyasema hayo wakati akiongea na waandishi wa habari jijini Tanga ambapo amesema mbali na mradi huo chuo hicho pia kinafanya mradi mwingine wa namna ya kuhifadhi maji ambao unamtaarifu muhusika kupitia simu ya kiganjani hivyo kuepusha miundombinu ya umeme kuharibika wakati maji yanapokosekana.

Pia amesema wanajivunia mradi wa chakula na mazingira ambapo chakula kwa ajili ya wanyama kwa mfano vitu vinavyoharibika vinaweza kutengenezwa na kutumika kwa ajili ya chakula cha wanyama huku wakiwa na mradi mwingine wa kutumia chupa za plastiki kuweza kutengeneza nguo kuanzia hatua za uzi mpaka kutengeneza nguo ambao mtu anaweza akatumia.

Dkt. huyo amesema hayo ni baadhi ya mambo machache yanayofanyika kwenye chuo hicho hivyo kushiriki kwao katika maonesho hayo huku akiwakaribisha wakazi wa Mkoa Tanga kutembelea bando lao ili waweze kujionea namna ambavyo wanaweza kujiunga na chuo hicho.

“Tumebobea katika maeneo mbalimbali na sisi ni wakongwe tunao wataalamu wengi wa kutosha karibu kila eneo na kwamba ni msaada mkubwa kwa Taifa hivyo wakazi wa Tanga tumieni fursa hii adhimu, “

Kwa upande wake Julio Nyakunga ambaye ni muhitimu kutoka chuo hicho amesema wamekuja na mfumo wa kuangalia visababishi vya sumu kuvu inazalishwa na fangasi na yenye madhara ya kiafya na kiuchumi.

Ikiwemo kusababisha maradhi ya saratani ya ini na udumavu kwa watoto huku kwa upande wa uchumi ikosababisha kushuka kwa mazao ya nafaka.

Amesema kupitia mfumo huo wanaweza wakakuza thamani ya mazao yao na kuboresha afya ya walaji kwa ujumla.

“Tumeona jamii haijui sana kuhusu sumu kuvu watu tumekuwa tukitumia nafaka hizi bila kujua ni salama au si salama kwaio tunashauri wanaTanga kwa ujumla waje kupata elimu kuhusu sumu kuvu na kujionea mfumo wetu unavyofanya kazi na namna gani tunaweza kuwasaidia wao wakiwa kama wakulima na watumiaji pia wa nafaka hizi,”a mesisitiza Julio.