March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UDOM yabuni mafuta ya nywele na ngozi kutokana na mabaki ya zabibu

Mafuta ya nywele na ngozi yaliyobumiwa na wanafunzi wa UDOM kutokana na mabaki ya zabibu

UDOM yabuni mafuta ya nywele na ngozi kutokana na mabaki ya zabibu

Na Joyce Kasiki, TimesMajiraoline

CHUO  Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimeonesha mfano bora wa ubunifu na matumizi ya sayansi kwa vitendo baada ya wanafunzi wake kubuni mafuta ya nywele na ngozi yanayotokana na mabaki ya zabibu, hatua inayolenga kutatua changamoto za kimazingira huku ikichochea ujasiriamali kwa vijana.

Ubunifu huo umeonyeshwa  katika Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba, ambapo mwakilishi wa chuo hicho, Uswege Mwangoge, amesema wazo hilo lilizaliwa kutokana na uchunguzi wa mazingira unaoonesha kuwa mabaki ya zabibu mara nyingi hutupwa hovyo, na hivyo kuchangia uchafuzi wa mazingira.

“Wanafunzi wetu waliamua kugeuza changamoto hiyo kuwa fursa. Walifanya utafiti na kugundua kuwa mabaki ya zabibu yana virutubisho vingi vinavyoweza kutumika kutengeneza mafuta yenye faida kubwa kwa ngozi na nywele,” amesema Mwangoge.

Kwa mujibu wa maelezo yake, mafuta hayo ya asili hayana kemikali hatarishi na yanapenya haraka kwenye ngozi, huku yakiwa na vitamin mbalimbali zenye uwezo wa kulainisha, kuimarisha, na kurudisha ngozi katika hali yake ya kawaida.

 “Mafuta haya hayatoboi ngozi kama ilivyo kwa baadhi ya bidhaa za viwandani, bali huimarisha vinyweleo na kulinda ngozi dhidi ya athari za mazingira,” amesema.

Kwa upande wa matumizi kwenye nywele, Mwangoge amesema mafuta hayo huchochea ukuaji wa nywele, huongeza unyevu, kuzuia kukatika kwa nywele, na kuimarisha mizizi. 

Amesema pia mafuta hayo huondoa mba, hutuliza ngozi ya kichwa na kuhakikisha afya ya nywele bila kutumia kemikali yoyote ya viwandani.

Ubunifu huu umepongezwa na wadau mbalimbali wa sekta ya elimu na afya ya uzuri, wakieleza kuwa ni mfano wa namna elimu ya juu inavyoweza kutumika kuleta suluhisho la matatizo ya jamii na mazingira, huku ikiibua ajira na fursa za kiuchumi.

Chuo Kikuu cha Dodoma kimeahidi kuendelea kusaidia wanafunzi wake katika tafiti na ubunifu wa aina hii kwa lengo la kukuza ujuzi wa vitendo na kuchochea maendeleo ya viwanda vidogo kupitia maarifa ya ndani.