December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC apongeza mradi wa kuwezesha vijiji 14 kuingia kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi


Na Mary Margwe, Timesmajira Online,Simanjiro

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara Dkt. Suleiman Serera amelipongeza shirika lisilo la Kiserikali la Ujamaa Community Resource Team ( UCRT) kuja na mradi mpya wa kuwezesha vijiji 14 vya Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro na Kiteto kuingia kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi, hali itakayosaidia kuondokana na migogoro mingi ya ardhi wilayani humo.

Hayo amezungumza kwenye mapokezi ya mradi mpya wa Uhifadhi Jumuishi wa Mazingira na kuboresha maisha ya Jamii katika Halmashauri mbili za Mkoa wa Manyara ambayo ni Simanjiro na Kiteto, na kuzinduliwa katika Mji Mdogo wa Orkesument.

Dkt. Serera amesema UCRT ni shirika linalofanya vizuri ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro katika kuhakikisha inafikia jamii moja kwa moja na kugusa matatizo yao,hatimaye kuweza kupanga matumizi bora ya ardhi na kuondokana na migogoro mingi.

Pamoja na kuwezesha jamii za asili kumiliki, kusimamia ardhi na kunufaika nayo ili kuboresha maisha yao.

“Tunaona matokeo mazuri ambayo yamechangia hata kuondoa baadhi ya migogoro mikubwa ya ardhi tuliyokuwa nayo katika Wilaya hizi,” ameeleza Dkt.Serera.

Naye Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Christopher Ole Sendeka ameeleza kuwa awali zaidi ya vijiji 30 vimeingia katika matumizi bora ya ardhi na sasa vijiji 9 jambo ambalo ni jema kwa maendeleo endelevu ya wanaSimanjiro.

” Mradi huu unatoa elimu kwa wananchi juu ya sera, sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia masuala ya ardhi na wakati mwingine biblia inasema ukishaijua kweli na hiyo kweli itakuweka huru, nina maana wakati mwingine wananchi wetu wakishajua sera ya nchi inasema nini katika masuala ya ardhi,”.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Baraka Kanunga amesema palipo na migogoro kamwe maendeleo huwa ni vigumu kupatikana hivyo kuwepo kwa UCRT wilayani Simanjiro ni jambo linalotakiwa kuungwa mkono wazi wazi.

Mratibu wa Shirika la UCRT Edward Loure amesema mchakato wa uibuaji wa mradi huo mpya umekuja baada ya shirika hilo kupokea maombi kutoka Halmashauri za Wilaya kadhaa zikiwemo hizi za Simanjiro and Kiteto kuomba kufanyiwa michakato ya mipango ya matumizi ya ardhi.

” Jamii hizi ni za wawindaji, wakusanyaji, waokota matunda, (Wahadzabe na Waakie),wafugaji (Wamaasai na Wadatoga) pamoja na wafugaji-wakulima (Wabatemi na Wairaqw), UCRT inafanya kazi katika wilaya 10 Kaskazini mwa Tanzania iliyoko ndani ya mikoa ya Arusha na Manyara, ambapo mradi huo upo katika vijiji ni zaidi ya 140, “amesema Loure na kuongeza kuwa:

“Tuliomba mradi wenye thamani ya dola laki nane na elfu arobaini (USD 840,000), baadaye kiwango kiliongezeka hadi kufikia dola zaidi ya milioni moja na laki nne, ambapo kati ya fedha hizo Wilaya mbili za Simanjiro na Kiteto tumepata zaidi ya milioni 400 fedha za Kitanzania, ambapo mradi huu utatekelezwa kwa kipindi cha miaka 4 kuanzia mwaka huu (2024-2027),”.

Ameeleza lengo kuu la mradi huo ni kuweka ulinzi wa miliki za ardhi kwa jamii, kujengea uwezo taasisi za vijiji ili kuweza kusimamia, kutumia na kunufaika na rasilimali katika msingi endelevu.

” Vijiji vilivyolengwa na mradi mpya kwa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro ni pamoja na Ruvuremit, Lerumo, Ngage, Lobosoit B, Gunge, Lemkuna, Lengasiti,Losoito na Naisinyai huku Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto mradi umelenga vijiji vya Makame, Ngabolo, Irkiushioibor, katikati na Ndebo,”.