Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania(TASAC), limeeleza kuwa bado linaendelea na uchunguzi wa kubaini nini chanzo cha kupinduka na kuzama kwa meli ya MV.Clarias katika Bandari ya Mwanza Kaskazini huku likisisitiza kuchukua hatua kwa yeyote atakayekuwa amehusika.
Meli ya MV. Clarias ilijengwa mwaka 1961 ,ina uwezo wa kubeba abiria 216 na tani kumi za mizigo, alfajiri ya kuamkia Mei 19, mwaka huu, majira ya saa 10 ilibainika kulalia upande mmoja ikiwa imetia nanga bandarini kabla ya kupinduka na kuzama majini.
Tukio hilo lilitokea ikiwa ni siku moja baada ya meli hiyo kurejea kutoka Kisiwa cha Goziba,wilayani Muleba,Mkoa Kagera ambapo ilishusha abiria na mizigo katika mwalo wa Kirumba, Manispaa ya Ilemela na kuja kutia nanga Bandari ya Mwanza kaskazini.
Akizungumza Mei 29,mwaka huu katika kikao cha TASAC na wadau wa usafirishaji wa majini mkoani Mwanza, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC),Mohamed Salum, ameeleza kuwa kama walivyokuja kwa mara ya kwanza wiki iliopita,watachukua hatua baada ya kupata taarifa rasmi.
“Tumeisha fanya taarifa ya awali tutawasilisha kwa wenzetu pia tutapeleka Wizarani lakini taarifa kamili mpaka chombo kitakapo okolewa kutoka majini kwani bado hatujajua sababu ya msingi na iwapo kama watahusika mabaharia tutaona hatua za kuchukua ili kuongeza umakini kwao na uweledi katika usimamizi wa chombo,” Salum na kuongeza kuwa;
“Tukio la kupinduka na kuzama kwa meli ya MV. Clarias imetufundisha kuwa tuna haja ya kuwekeza katika masuala.ya uokozi wa vyombo,”.
Sanjari na hayo Salum ameeleza kuwa kuna mradi wa kikanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa kuhakikisha Ziwa Victoria linakuwa salama na yapotokea matukio watu wanafikiwa na kuokolewa kwa wakati kwa msingi huo ikaonekana ipo haja ya kujenga kituo kikubwa cha kikanda cha utafutaji na uokoaji.
“Makao yake ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yatakuwa hapa Mwanza kwaio nchi yetu imepata bahati ya kuwa makao makuu ya kituo cha kikanda cha utafutaji na uokoaji kwaio vifaa vingi vitakavyo nunuliwa vitakuwa vina’base’ Mwanza,pia vinajengwa vituo vidogo vidogo katika nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki kwa maana ya Uganda wanajenga vituo vyao,Kenya hivyo hivyo na sisi tunajenga pembezoni mwa Ziwa Victoria,”ameeleza Salum.
Aidha ameeleza kuwa mradi huu pia utakuwa na masuala ya mawasiliano ndani ya ziwa kwaio kuna minara ya mawasiliano.
“Tumeisha ainisha’identify’ visiwa ambapo itajengwa minara kwa kushirikiana na wenzetu Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA) na TCCL itajengwa minara pia mradi huo una vifaa vya hali ya hewa vitakavyofungwa ndani ya Ziwa kwaio taarifa za hali ya hewa zitakuwa zinapimwa maeneo yote ya ziwa, tunajua ziwa linatabia tofauti tofauti,”.
Hivyo wanaamini mradi huu utakapo kamilika mwishoni mwa mwaka huu utakuwa suluhisho la kwanza katika kuokoa maisha ya watu na mali zao ziwani.
Hata hivyo amesisitiza wadau wa usafiri ndani ya maji kuzingatia sheria, miongozo ikiwa pamoja na kutengeneza mifumo ya Udhibiti usalama ndani ya meli.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli Nchini (MSCL)Eric Hamissi, amependekeza kuundwa kwa Kamati ya kuimarisha usalama ndani ya maziwa makuu ambayo itakuwa kila baada ya miezi mitatu inakutana kwa ajili ya kuangalia tathimini na mikakati ya kuimarisha usalama kwenye maziwa makuu pamoja na kubainisha mahali pa kupata vifaa kwa ajili ya uokoaji.
“Kila siku yanaibuka mengine,tunapopata ajali ndio tunashtuka lakini ni vyema tuwe na Kamati itakavyokuwa inashughukika na masuala ya usalama tu kwa mfano inaweza kuainisha maeneo ambayo tunaweza kupata vifaa pindi likitokea la kutokea,ndege ilivyo anguka Presicion Air imetufundisha kitu,Mv.Bukoba miaka 28 iliopita imetufundisha jambo hata hii imetufundisha jambo,”.
Nao baadhi ya wadau wa usafirishaji majini wameomba katika suala la kuzingatia usalama ndani ya Ziwa pia TASAC waangalie na ongezeko la kina cha maji ziwani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mkombozi Fishing & Marine Transport Ibrahim Kitano,amependekeza kuwa kama kuna uzembe umefanyika katika tukio la kupinduka na kuzama kwa meli ya MV.Clarias basi hatua zichukukiwe kwa aliyehusika huku akiiomba TASAC kuweka taa ndani ya ziwa za kuongoza meli ili mtu aone hapa kuna hali ambayo siyo nzuri.
Meneja Mafunzo na Utoaji Vyeti kwa Mabaharia kutoka TASAC Mhandisi Lameck Sondo, ameeleza kuwa meli zote bila mabaharia haziwezi kutembea, mabaharia ni fani kama zilivyo nyingine hivyo ichukuliwe kwa umuhimu wake kwani nchi yoyote hasa ambayo ina meli au imezungukiwa na ukanda wa maji mabaharia wanachangia sana katika kukua kwa uchumi kwenye sekta hiyo.
Amesisitiza kuwa kila wamiliki wa vyombo vya usafiri majini kuhakikisha kila baharia anayeingiza ndani ya meli awe na mkataba wake sahihi ambao utakuwa na mambo ambayo umeainisha ikiwemo stahiki anayopaswa kupata huyo baharia ndani ya meli ikiwemo masaa gani ya kazi anayotakiwa kufanya.
Naye Meneja Usajili na Ukaguzi wa Meli kutoka TASAC Mhandisi Said Kahemeko, ameeleza kuwa mtu akiwa na nia ya kutaka kuanza kjenga meli anatakiwa kutoa taarifa TASAc ambapo jukumu lake ni kumpa muongozo ni namna gani na taratibu gani anatakiwa azifuate pamoja na sheria na miongozo mingine iliowekwa ili aweze kutengeneza chombo kilicho salama.
“Katika vyeti vya ubora na usalama tunatoa vinavyodumu kwa muda wa mwaka mmoja hivyo usije kuingizwa chombo chako ndani ya maji bila kuhakikisha vyeti vyako havijaisha muda wake na endapo vinakaribia kuisha kwa mujibu wa sheria miezi mitatu kabla havijaisha muda wake unatakiwa utoe taarifa TASAC lakini tumeweza kuona mazoe mengi unakuta mtu meli yake vyeti vinaisha kesho anaadika barua leo,”.
Pia ameeleza kuwa TASAC tunaisimamia vyombo vingi kwa upande wa vyombo vidogo tunavyo takribani 52,189 na upande wa vivuko tunavyo 33 na tunavingine vipya ambavyo serikali inaendelea kuwekeza kuhakikisha kwamba wanapata huduma salama tunamkadaradi wetu mzawa Songoro Marine anajenga vivuko 5, na sisi tunaendelea kuvisimamia.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi