November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ucheleweshaji mabadiliko Sheria ya Ndoa waibua mashaka kwa wanaharakati nchini

*Mwanaharakati aliyepinga sheria hiyo akashinda afunguka

Na Reuben Kagaruki,TimesMajira,Online,Dar

KILIO cha muda mrefu cha wanaharakati nchini ni madai ya mabadiliko kwenye vifungu vya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 ambavyo ni kikwazo kwa mtoto wa kike.

Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanaendeleza kupaza sauti yakitaka vifungu hivyo vinavyoruhusu mtoto mwenye umri chini ya miaka 18 kuolewa vibadilishwe.

Vifungu vya sheria hiyo vinavyopigiwa kelele ni vile vinavyoruhusu msichana kuolewa akiwa na umri chini ya miaka 18 kwa idhini ya mzazi, lakini umri huo usiwe chini ya miaka 15.

Kwa mujibu wa sheria hiyo mtoto wa kike mwenye umri usiopungua miaka 14 anaweza kuolewa kwa idhini ya Mahakama. Udhaifu katika sheria hiyo, ndiyo unachangia vifungu hivyo vya Sheria hiyo ya Ndoa ya Mwaka 1971 kupingwa nje na ndani ya Mahakama.

Mfano, mwanaharakati wa kutetea haki za mtoto wa kike nchini na Mkurugenzi wa Shirika la Mwanamke ni Uwezo, Rebeca Gyumi, aliamua kufungua kesi Mahakama Kuu kupinga vifungu vya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 vinavyoruhusu mtoto wa kike chini ya miaka 18 kuolewa.

Katika shauri hilo, Mahakama Kuu ilimpa ushindi mwanaharakati huyo, lakini Serikali ilikata rufaa katika Mahakama ya Rufani, ikipinga hukumu ya Mahakama Kuu Dar es Salaam.

Hukumu iliyotolewa Oktoba 23,2019 mahakama ilitengua kipengele cha sheria ya ndoa kinachoruhusu mtoto mwenye umri wa miaka 14 (aliye chini ya umri wa miaka 18 kuolewa.

Ushindi huo uliipa nguvu Serikali kwenda Bungeni kurekebisha sheria hiyo, lakini hadi sasa haijafanya hivyo. Swali kubwa ambalo wadau wengi wanajiuliza ni kwa nini Serikali haijatekeleza uamuzi huo wa mahakama wakati hukumu ilikuwa wazi?

Akizungumza hivi karibuni kwenye kikao kilichokutanisha wabunge na wenyeviti wa halmashauri kwa lengo la kutoa maoni na mapendekezo yatakayosaidia mabadiliko ya Sheria ya Ndoa yasiyoathiri mtoto wa kike, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju, alisema Januari mwaka huu walikutana na Kamati ya Kudumu ya Sheria na Katiba ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwasilisha maoni ya marekebisho ya sheria hiyo kwenye Bunge.

Alisema baada ya maoni hayo kuwasilishwa, Bunge lilielekeza kuwa kutokana na unyeti wa sheria hiyo ni vema sasa wakapate maoni zaidi kutoka kwa wananchi.

Anasema kwa sasa maoni zaidi yanachukuliwa kutoka kwa wananchi kuhusu mabadiliko ya sheria hiyo.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Geofrey Pinda, anarejea uamuzi wa Mahakama ya Rufani kuhusu vifungu namba 13 na 17 vya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, akiwasihi wadau kutoa maoni yanayolenge maboresho.

Naibu Waziri Pinda, alisema; “Ninyi wenyewe ni mashahidi, wakati mwingine tunawaozesha watoto wakiwa hawana uwezo wa kumiliki nyumba zao, Nyumba nyingi ‘zinaharibika’ katika umri mdogo wa ndoa kwa sababu wanandoa wanakuwa hawajakomoa.

Ndiyo maana hata majaji walipoamua kuihukumu kesi hii wakatupa mwongozo kuwa tukaeni na kutafuta namna nzuri ya kuwalea watoto wa kike hadi wafiki miaka 18, ndipo tuingie kwenye makubaliano ya ndoa.”

Akizungumza Bungeni jijini Dodoma Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Paramagamba Kabudi, alisema baada ya Serikali kutafakari kwa makini suala la mabadiliko ya Sheria ya Ndoa, inaona suala hilo linahitaji umakini mkubwa sana.

Alisema Mwaka 1971 wakati Sheria ya Ndoa inapitishwa, elimu ya mwisho ya mtoto ilikuwa darasa la saba.

“Asipoendelea kuingia kidato cha kwanza ina maana amekaa nyumbani, na turudi kwenye jamii na kila mmoja nyumbani kwake anakujua, hivyo mtoto wa kike aliyevunja ungo kwake kipi chema, aolewe azae katika ndoa au azuiwe kuolewa mpaka afike miaka 15 wakati huko kwingine hakujafungwa na anaweza kupata ujauzito?

Na atakapoupata ujauzito huo akazaa huyo mtoto kama ni mkatoliki hatabatizwa mpaka aende afanye maungamo na maungamo hayo kikatoliki ni ya yeye mama siyo baba aliyemzalisha.”

Anatahadhari kwamba sheria ya ndoa wakiiendea haraka watabomoa na sio kujenga kwa sababu sheria ya ndoa ni jamii sio mtu.

Pamoja na kauli hiyo ya Serikali kwamba Bunge limeielekeza Wizara kukusanya maoni zaidi kuhusu mabadiliko ya sheria hiyo, Rebeca anasema wao wanachotaka kuona ni mabadiliko.

“Tunadhani Serikali inatumia mwanya wa kusema wanarudisha muswada huo kwenye jamii kutafuta maoni ili baadaye ufikishwe Bungeni kama kutafuta sababu,” anasema Rebeca.

Kwa mujibu wa Rebeca, hukumu ya mahakama ilikuwa wazi na sheria zetu zipo wazi kuhusu shughuli na wajibu wa kila muhimili wa Serikali.

“Kwa hiyo muhimili wa Mahakama unapotafsiri sheria na kuipa Serikali muda iwe imebadilisha kifungu fulani, Serikali inabidi kutekeleza inavyoelekezwa, inatakiwa ifanye hivyo haraka,” anasema Rebeca na kuongeza;

“Lakini kama Wizara wanasema wamepeleka muswada bungeni, halafu Bunge likasema linaurudisha wizarani kuchukua tena maoni ya wananchi, kwetu sisi, tunaoshughulikia masuala ya ustawi wa wasichana tunabaki na maswali mengi.

Tunajiuliza nia hasa inakuwa ni nini? Na je utayari wetu wa kusimamia sheria ukoje! Au tunasimamia sheria zetu wakati gani kwa sababu tunajua sheria ipo wazi kuhusiana na utekelezaji wa hukumu na jinsi mihimili hiyo ya Serikali inavyopaswa kusaidiana hasa linapokuja suala linalohusu Katiba.”

Hata hivyo, anasema Bunge kusema nendeni mkakusanye maoni ni sehemu ya utekelezaji wa hukumu. “Lakini sisi kwa upande wetu tunasema ni kwa nini hukumu ilitoa muda maalum na ikasema hili linatakiwa ifanyike kwa haraka?

“Ukweli ni kwamba Serikali inatoa kauli kwamba inakusanya maoni na inasubiri maoni yakirudi ndiyo ipeleke Bungeni. Mimi naona ni kutumia mwanya huo kuchelewesha mabadiliko,” anasema Rebeca na kusisitiza;

“Nia ya kupeleka mchakato katika ngazi ya jamii ni nini wakati maana ya hukumu ilikuwa ni kwamba sheria inaonekana ipo kinyume na sheria na Bunge lilitakiwa kutekeleza tu uamuzi wa mahakama na si vinginevyo.”

Mwanasheria, Anna Paul, anasema Serikali ilielekezwa kufanyia mabadiliko vifungu namba 13 na 17 vya sheria hiyo, kwa hiyo utekelezaji ulitakiwa kufanyika haraka, kwani mtu wa miaka chini 18 bado ni mdogo na hatakiwi kuingizwa kwenye ndoa.

Anatoa mfano kwamba hata sheria ya mikata nchini hairuhu mtu mwenye umri wa miaka 18 kuigia makubaliano ya mikataba kwa sababu sheria inamtambua kwamba ni mtoto.

Hata hivyo, anasema sheria ya ndoa kuruhusu mtoto wa miaka chini 18 na kuruhusiwa kutia saini cheti cha ndoa ni kinyume na sheria ya mikataba.

“Cheti cha ndoa ni mkataba baina ya anayeoa na kuolewa, hivyo binti wa miaka chini ya miaka 18 akisaini cheti cha ndoa anakuwa anakinzana na Sheria ya mikataba inayozuia mtu wa chini ya miaka 18 kusaini mikataba,” anasema na kusisitiza;

“Serikali inabidi iyaone haya na kwa kutekeleza hukumu ya mahakama na diyo kuendelea kukusanya maoni kwa ajili ya kufanyia mabadiliko vifungu hivyo, huku wengine wakiendelea kuozesha,” anasema.

Anatolea mfano sheria ya uchaguzi akisema mtoto chini ya miaka 18 haruhusiwi kupiga kura kwa sababu anahesabika bado ni mtoto. “Wakati sheria hii inatambua mtu wa chini ya miaka 18 kuwa bado ni mtoto, haruhusiwi kupiga kura, sheria ya ndoa inamlazimisha kumuingiza kwenye ndoa,” anasema Anna na kutoa mwito sheria hiyo ifanyiwe mabadiliko haraka pasipo visingizio.

Mratibu wa Mradi wa Nguvu ya SAUTI ya Msichana, Arodia Aloyce, anakiri kuwa tatizo la ndoa za utotoni linachangia watoto wa kike kushindwa kufikia ndoto zao

“Kunapotokea ndoa za utotoni, mimba za utotoni na ukatili wa kijinsia haki za watoto au za akina mama zinakandamizwa na kupelekea kushindwa kutetea haki zao,” anasema Aloyce.

Anatolea mfano kwamba matukio ya ukatili wa kijinsia ikiwemo wazazi kufikia hatua ya kuwaozesha watoto wenye umri chini ya miaka 18.

Katika kukabiliana na ndoa za utotoni anasema wanafanya kazi na mamlaka mbalimbali kama vile uongozi wa kata au wilaya ambapo shirika hilo linatoa taarifa kama kuna mtu anahitajika kuondolewa kwenye mazingira hayo (ndoa za utotoni).

Kwa mujibu wa Aloyce wana kituo Bunju kwa ajili ya makazi salama ya watoto wanaoondolewa kwenye ndoa na wakiwa hapo, ndipo taratibu nyingine za kisheria huwa zinachukuliwa dhidi ya waliohusika kuoa au kuozesha watoto.

“Tunapopata taarifa ya tukio la ukatili wa kijinsia hushirikiana na viongozi wa Serikali kama kata au mtaa husika kwa ajili ya kufatilia kwa undani zaidi tukio hilo,”anasema Aloyce.

Anataja moja ya changamoto zinazowakabili ni pale wanapotaka kumuondoa mtoto kwenye tatizo hilo na mhusika akakataa kutoa ushirikiano.

Ili kuwajengea wasichana uwezo wa kutumia nguvu ya sauti zao, anasema wanawashari wasichana na wale wanaofanyiwa ukatili ikiwemo kuozeshwa katika umri mdogo upaza sauti zao ili kupata msaada iliyopo karibu.

“Lakini tunatoa mwito kwa wadau na Serikali kupambana na matukio hayo kwa ushirikiano ili kufanya jamii kupinga vitendo hivyo,” anasema.