March 26, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uchambuzi wa bajeti kuchochea ufanisi taasisi za umma

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Timu ya wataalamu 53 kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) itajifungia kwa wiki mbili, kuanzia Jumatatu (Leo), kufanya uchambuzi wa mipango na bajeti za taasisi na mashirika ya umma, kazi ambayo ni muhimu katika kuhakikisha usimamizi mzuri wa rasilimali za serikali.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari  jana na Mkurugenzi Msaidizi wa Usimamizi wa Mashirika yasiyo ya kibiashara, Ofisi ya Msajili wa Hazina, Joseph Mwaisemba, alisema kuwa Uchambuzi wa bajeti za mwaka wa fedha 2025/26 unahusisha taasisi za umma 252.

“Zoezi la uchambuzi linalofanyika katika Shule ya Uongozi Mwalimu Nyerere, ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha kwamba fedha za umma zinatumika kwa njia bora na yenye ufanisi,ili kufanikisha lengo lililokusudiwa na kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 10(2) (c) cha Sheria ya Msajili wa Hazina SURA 370 na kifungu cha 17(a) cha Sheria ya Bajeti SURA 439, OMH inatakiwa kufanya uchambuzi wa mipango na bajeti ya Taasisi na Mashirika ya umma yaliyochini yake,”amesema.

Amesema lengo  ni kuidhinisha mikakati, mipango ya mwaka ya Taasisi na Mashirika ya umma na kuijumuisha katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo kwa ajili ya usimamizi wa utekelezaji na kugharamiwa.

“Utekelezaji wa maelekezo ya Mwongozo huu kwa ukamilifu utachangia: udhibiti wa matumizi ya fedha za umma na kuleta tija iliyokusudiwa,” alisema Mwaisemba, ambaye pia ni msimamimizi wa zoezi la uchambuzi wa bajeti.

Aidha, amesema utekelezaji utapelekea kuongezeka kwa ushiriki wa sekta binafsi kwenye shughuli za uwekezaji na biashara na kutoa fursa sawa za ajira kwa wote.

Amesema utekelezaji wa maelekezo ya muongozo utapelekea  kuendelea kuimarika kwa utoshelevu wa chakula nchini na kuongeza upatikanaji wa huduma za jamii kwa wote.

Mwaisemba, amesema matokeo tarajiwa ya serikali  OMH na mashirika husika ni pamoja na kuongeza rejesho la uwekezaji wa mashirika ya umma kwa Serikali kupitia makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi, ulipaji wa kodi, utoaji wa huduma, na ajira.

“Uwekezaji wa serikali katika taasisi, mashirika ya umma na wakala za serikali 252 ni Sh83.4 trilioni, ambao ni uthibitisho wa dhamira ya serikali katika kuimarisha sekta mbalimbali za uchumi na kuhakikisha kwamba huduma muhimu zinapatikana kwa wananchi.

“Rejesho la uwekezaji wa serikali, inatarajiwa kushuhudiwa kuimarika kwa utawala bora, kuongezeka kwa ufanisi kwa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, pamoja na kuelekeza rasilimali katika maeneo yenye tija ambayo yatachangia katika ukuaji wa uchumi,”amesema.

Mwaisemba, amesema kuwa serikali inatoa Mwongozo wa Mpango na Bajeti ambao unaandaliwa kwa mujibu wa Kifungu Na. 21 cha Sheria ya Bajeti, Sura 439. 

Amesema mwongozo huo unalenga katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 (TDV 2025) pamoja na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26, na utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa ajili ya Uchaguzi ya Mwaka 2020.

“Maeneo yanayopewa kipaumbele ni pamoja na maelekezo kuhusu ulazima wa kuzingatia vipaumbele vya mpango, maelekezo ya ujumla kuhusu uandaaji wa mpango na bajeti  na maelekezo mahususi kwa mashirika na taasisi za umma.

“Vigezo vinavyotumika katika uchambuzi wa mipango na bajeti ni pamoja na Utekelezaji wa maelekezo mahususi ya Serikali yaliyotolewa katika mwongozo wa mpango na bajeti wa Serikali katika mwaka husika,Vigezo vya kupima utendaji wa taasisi na mashirika ya umma ambayo vinahusu masuala ya kifedha, rasilimali watu, utawala bora, huduma kwa wateja, na utekelezaji wa majukumu ya msingi ya taasisi.

“Matokeo tarajiwa (faida kwa Serikali, OMH na mashirika husika) ni pamoja na  kuongeza rejesho la uwekezaji wa mashirika ya umma kwa Serikali kupitia makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi, ulipaji wa kodi, utoaji wa huduma, na ajira,”amesema.

Mwaisemba ametoa wito wa kuwepo kwa ushirikiano wa karibu kutoka kwa wenyeviti wa Bodi za Wakurugenzi, Menejimenti, na watumishi wa taasisi na mashirika ya umma. 

“Tunahitaji tushirikiane kwa pamoja kuhakikisha malengo ya serikali ya uanzishwaji wa mashirika hayo yanafikiwa ili yaweze kuchangia katika maendeleo ya nchi yetu,” amesema. 

Amesema hiyo ni muhimu hasa katika kipindi hiki ambapo dhamira ya serikali ni kuondokana au kupunguza utegemezi wa wadau wa maendeleo katika kutekeleza majukumu yake.