Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), imeendelea kushangaza mataifa mbalimbali kwa umahiri wake wa matibabu ya kibingwa ya moyo ambao safari hii imeadhimisha siku ya moyo duniani kwa kufanya upasuaji wa moyo kwa wagonjwa 30 Zambia.
Wiki moja kabla ya siku ya moyo duniani JKCI ilipeleka madaktari bingwa wanne wa moyo kwenda kufanya upasuaji kwa nchi jirani ya Zambia kama ishara ya kujenga uhusiano mzuri kati ya Zambia na Tanzania na kutoa fursa ya kujifunza na madaktari wa JKCI kufundisha wenzao wa Zambia.
Akizungumza mara baada ya kuwasili nchini, kiongozi wa ujumbe wa madaktari wa JKCI waliokuwa Zambia, Dk. Viviane Mlawi alisema madaktari hao waliokuwa Zambia kwa wiki moja walitumia muda huo pia kuwajengea uwezo wa upande wa tiba ya moyo na kufungua milango Tanzania kama kituo cha umahiri wa mafunzo kwa madaktari wanaotaka kuja kujifunza Tanzania matibabu ya kibingwa ya moyo.
Alisema gharama za matibabu ya kupeleka wagonjwa wa moyo katika mataifa yaliyoendelea ni kubwa lakini JKCI inauwezo wa kutoa huduma kama hizo na kwa ubora ule ule kwa gharama ambayo watu wengi wanaweza kuzimudu.
Alisema Tanzania inaweza kushirikiana na Zambia kwa wagonjwa wao kuja kupata matibabu ya kibingwa ya moyo hapa nchini au wataalamu bobezi wa moyo kwenda nchini humo kufanya matibabu kama ilivyofanya kuanzia tarehe 23 mpaka 29 mwezi wa tisa.
“Ubalozi wa Tanzania kule Zambia hauko tu kwaajili ya kuimarisha diplomasia bali kutoa fursa kwa watu wanaoumwa kuja kutibiwa nchini Tanzania kila nchi ambayo itakuwa tayari kusaidiana na Tanzania watumie balozi wetu na tunafanya hivyo kwasababu Tanzania imeshaboresha huduma za afya kwa teknollojia za kisasa na madaktari bobezi,” alisema
Alisema Rais Samia Suluhu Hassan amewekeza kwa kiwango kikubwa kwenye sekta ya afya kwa kuweka vifaa tiba vinavyokwenda na wakati hali ambayo imesaidia nchi kupunguza utegemezi wa kupeleka wagonjwa wa moyo nje ya nchi kwa asilimia 95.
Alisema katika kuonyesha umahiri wake ndiyo sababu JKCI ikaamua kuadhimisha siku ya moyo duniani kwa kuweka kambi ya moyo nchini Zambia ambayo iliwakilisha tu nchi zingine majirani kama Malawi, Kenya Uganda, Msumbiji na nchi za kusini mwa jangwa la sahara.
“Kwa nchi zinazotaka kufanya tafiti na mafunzo watumie JKCI katika kuwajengea uwezo kwa kuwafundisha madaktari wao wanaotaka kubobea kwenye tiba ya moyo, waje Tanzania kujifunza badala ya kutumia fedha nyingi kuwapeleka nchi zilizoendelea kutafuta matibabu na mafunzo ya ubobezi,” alisema.
Alisema katika mwendelezo wa kuadhimisha siku ya moyo duniani, JKCI kuanzia tarehe 2 Oktoba imepeleka wataalamu wake Geita ambapo wataendesha kambi ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo bure kwa wananchi wa maeneo hayo wakati wa maonyesho ya madini.
Alisema hayo yote yanafanyika katika jitihada za kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ametumia gharama kubwa kuboresha afya ya mama na mtoto na huduma bora ya afya ya moyo Tanzania.
“JKCI kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Geita imepanga kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo bure na kauli mbiu ya mwaka huu inahamasisha matumizi ya teknolojia upande wa moyo kwa hiyo JKCI imeona ni wakati wa kwenda kwenye maeneo hayo ya kanda ya ziwa kwasababu hakuna hospitali bobezi ya moyo na ikiwezekana kuanzishwe kituo bobezi cha matibabu ya moyo,” alisema
Alisema mbali na uchunguzi wa afya ya moyo, JKCI itatoa elimu ya afya ya moyo kwa wachimbaji na kuweka mkakati bora endelevu wa kutoa elimu ya afya ya moyo kwa wachimbaji wa madini na kuhakikisha hospitali zote za kanda ya ziwa ikiwemo ya rufaa ya Geita na Chato zinashirikiana na JKCI kuanizsha kituo kikubwa cha matibabu ya moyo.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best