January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ubaguzi ulivyochangia wanawake kushindwa
kuingia kwenye vyombo vya maamuzi

Na Penina Malundo,TimesMajira.Online

BADO kumekuwa na changamoto kubwa katika usawa wa jinsia katika vyombo vya maamuzi ikiwemo kwenye Bunge, hali inayofanya wanawake kujiona kuwa bado wapo nyuma kwenye vyombo vya maamuzi.

Hali hiyo imekuwa ikilalamikiwa na wanawake wengi kwa kile walichokuwa wanasema hawapewi fursa sawa katika vyombo vya maamuzi kama Bunge na kujiona kuwa bado wanakazi kubwa ya kufanya na kuonyesha juhudi zao katika uchapaji kazi.

Hatua hiyo inafanya ushiriki wa wanawake katika siasa katika ngazi ya maamuzi ikiwemo Bunge kusuasua kutokana na kuwa na idadi ndogo nahilo sio jambo geni kwakuwa limetokea mara kadhaa huko nyuma hata kwa katika mabunge ya hivi karibuni.

Mathalani katika Bunge la 12 liloanza Novemba 2020 baada ya uchaguzi mkuu linalotakiwa kuwa na jumla ya wabunge 393 ambapo hadi sasa Bunge hilo linawabunge 383 kati yao wanawake waliochaguliwa majimboni ni takribani 25 tu kati ya wabunge 264 wanao takiwa kuchaguliwa kutoka majimboni.

Huku wabunge wengine wanawake wakipitia katika mfumo wa vitu maalum ambapo Chama cha Mapinduzi wakiwa 94 na Chadema 19.

Idadi hiyo ya wabunge 25 wabunge la 12 inalingana kabisa na idadi ya wabunge la 11 liloanza mwaka 2015 na kuisha mwaka 2020 kiwango hicho ambacho hakikaribii hata chembe ya wabunge wanaume waliochanguliwa majimboni na ikiwa ni chini takribani mara 10 ya wabunge wa wanaume waliopo majimboni.

Huku viti maalum katika bunge la 11 kutoka Chama cha Mapinduzi wakiwa Wabunge 64, Chadema wakiwa 36, Chama cha CUF wakiwa 10 kwa mujibu wa taarifa ya Bunge.

Hata hivyo idadi ya wanawake wanaojitokeza kugombea ubunge kupitia majimbo bado ni mdogo kulinganisha na ya wanaume ambapo wanawake wamekuwa wakilalamika juu ya kukosekana kwa usawa hivyo kufanya kuwa mstari wa nyuma pale linapokuja suala la ushiriki wao kusababisha fursa nyingi kuchangamkiwa na wanaume jambo linalofanya kuendelea kuleta pengo kubwa baina yao.

Katika bunge la 12 liloanza Novemba lina wabunge wanawake wawili tu wa upinzani waliofanikiwa kuchaguliwa na wananchi ukilinganisha na Bunge la 11 ambalo liliokuwa na wabunge saba wanawake waliochaguliwa kutoka majimboni.

Aidha miongoni mwa wabunge wanawake wa Bunge la 11 ambao wamerudi katika Bunge la 12 ni pamoja na Mbunge wa Babati Pauline Gekul, Ukonga (Bonnah Kamoli), Ilemela (Dr. Angeline Mabula), Dkt.Ashatu Kijaji, Urambo (Magreth Sitta), Peramiho (Jenista Mhagama) na Nyasa( Eng.Stella Manyanya).

SABABU YA UWAKILISHI MDOGO BUNGENI

Miongoni mwa mbunge alikuwa katika Bunge la 11, Anna Tibaijuka ambaye alikuwa Mbunge wa Muleba Kusini wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), anasema kipindi cha miaka ya nyuma walipoingia katika ulingo wa siasa hali ilikuwa ngumu zaidi kuliko sasa ya wanwake kujitokeza katika michakato ya uchaguzi.

Anasema katika kipindi hicho wanawake wengi walikuwa hawajitokezi katika michakato ya uchaguzi kwa sababu mbalimbali .

Tibaijuka anasema miongoni mwa sababu hizo ni pamoja na ubaguzi dhidi ya wanawake pia kutoaminika kwa wanawake kulikosababisha kushindwa kuingia kwenye vyombo vya maamuzi.

“Ila kwa sasa hali imebadilika kabisa na sisi ndio tumefanya haya yote wanawake wamekuwa wakijitokeza kwa wingi katika michakato ya siasa na wengi kuingia Bungeni.

“Ile hali ya ubaguzi na kutoaminika imepotea kabisa kipindi hiki ukilinganisha na miaka ya nyuma,”anasema Tibaijuka

Anasema anaona sasa hivi wanawake wanavyosimama majukwaani wanavyotoa hoja zao,ambazo zimepangilika hiyo yote ni kwasababu sisi wabunge wanawake wa zamani ndiyo tumewafikisha hapa.

“Wanahoja nzuri sana wanawake wanasiasa wa sasa kama wasipochaguliwa ni utashi wa wapiga kura lakini sio ishu nyingine,”anasema

Kwa Upande wake Mbunge pekee wa kuchaguliwa kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Nkasi,Aida Khenani ,anasema changamoto kubwa alizokumbana nazo kama mbunge wa kwanza wa upinzani ambaye ni mwanamke aliyechaguliwa katika mkoa huo, ni pamojana kudhalilishwa.

Mbunge huyo aliyemshinda mbunge mwanaume wa CCM ambaye alikuwa machachari sana ameleza kuwa inapotokea ushindani kati ya mwanamke na mwanaume mara nyingi mwanamke anadhalilishwa zaidi hali inayowafanya wanawake wengine kuogopa kugombea nafasi mbalimbali.

Aida anasema kitu cha kwanza alijua yeye ni mtu wa namna gani na alimjua mtu anaeenda kushindana naye,hali hiyo ilimfanya amsome mgombea mwenzie tangu alipokuwa Bungeni yeye akiwa Viti Maalum.

Anasema wanawake wengi wanaogopa kushiriki nafasi mbalimbali za maamuzi kwa kuhofia lugha za udhalilishaji na kukatishwa tamaa.

Akitaoa wito kwa wanawake anasema mwanamke anapoingia katika siasa asione kama anashindwa bali aone anaingia kama anavyoingia mwanaume kwani inawezekana mtu akidhubutu.

“Mimi kama Aida ni mbunge mwanamke wa Kuchaguliwa katika jimbo la Nkasi Kaskazini na ni kwa mara ya kwanza mkoa wa Rukwa kupata Mbunge Mwanamke wa kuteuliwa,”anasema.

Naye mmoja wa wachambuzi wa masuala ya siasa nchini, Benson Bana anasema ushiriki wa wanawake katika siasa una haki sawa kama walivyo wanaume kwani wao ni binadamu.

Anasema wanapaswa kutumia haki zao za kibinadamu bila vikwazo kwani haki zao za kisiasa na kiraia ziko palepale.

“Ushiriki wao haupaswi kuhojiwa wala kuingiliwa au kuzuiwa na mtu yeyote au chombo chochote kwani Wanawake wanayo haki ya kushiriki katika nafasi za uongozi kwa kuchaguliwa au kuteuliwa.,”anasema Dkt.Bana

Anasema tafiti za kisayansi na uzoefu vinaonesha kuwa wanawake wanao uwezo, maarifa na stadi za uongozi na pale ambapo wanapungukiwa kama walivyo wanaume, mipango endelevu ya kuwajengea uwezo iandaliwe na kutekelezwa.

Anasema kipindi cha uchaguzi mkuu wa mwaka jana ushiriki wao umeonekama kuongezeka sana na kujituma tangu katika kura za maoni hadi katika uchaguzi mkuu.

Aidha anasema kuna nafasi mbalimbali ambazo wanawake wamepata ikiwemo unaibu Spika ambapo imefanya wazidi kung’ara ,kuna ongezeko la wanawake katika tasnia ya sheria- Majaji na Mahakimu.

Anasema katika uchaguzi Mkuu uliopita wanawake walijitokeza kugombea mpaka hadi nafasi ya Urais inaonyesha ni namna gani wanawake walivyoshawishika.