Na Aveline Kitomary,TimesMajira Online, Dar
WIZARA ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto imebaini mapungufu katika utoaji wa huduma za dawa na vipimo katika hospitali 28 za Rufaa za mikoa ambapo jumla ya fedha zilizothaminishwa kwa mapungufu hayo zinakadiriwa kuwa ni sh.Bilioni 26.7.
Kutokana na kuonekana kwa mapungufu hayo Waziri wa Afya,Dkt.Dorothy Gwajima, amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Prof.Mabula Ntemba kufanya mabadiliko ya viongozi wa timu ya uendeshaji wa hospitali zote 28 za rufaa za mikoa kulingana na nafasi ya kila kiongozi walivyoshiriki kusababisha hasara.
Akitoa matokeo ya kamati mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Dkt.Gwajima amesema, kumekuwepo kwa malalamiko mengi toka kwa wananchi kuhusu kukosa huduma za dawa na vipimo katika vituo vya kutolea huduma licha ya kuongezeka kwa bajeti ya dawa kutoka sh.bilioni 31 hadi sh.bilioni 270.
“Ili ukweli ujulikane Februari 1, mwaka huu wizara iliunda kamati ya wataalamu kutoka wizara na taasisi za sekta binafsi ili kufanya ufuatiliaji katika hospitali hizo kuanzaia Julai 2019 hadi Disemba 2020 ili kubaini changamoto iliyopo, kwa jumla ya bidhaa za dawa na vipimo 25-30 tu kati ya nyingi zilizopo kwenye orodha ya bidhaa za afya kwa kituo husika kufanyiwa ufuatiliaji kuanzia manunuzi,mapokezi na matumizi.
“Taarifa ya kamati imethibitisha uwepo wa uzembe na kutojali katika usimamizi wa mfumo wa ugavi wa bidhaa za afya,viashiria vya hujuma,wizi na udokozi,mapungufu yamechangiwa na utendaji wa mazoea wa baadhi ya viongozi wasio waadilifu na wasiowajibika kuanzia ngazi ya Taifa,mkoa,halmashauri pamoja na watumishi mmoja mmoja,”amesema Dkt.Gwajima.
Akiainisha maeneo yaliyofanyiwa ufuatiliaji na thamani ya fedha, Dkt. Gwajima alisema bidhaa zilizopelekwa bohari za hospitali husika na hazikuingizwa kwenye vitabu vya mali vilisababisha upotevu wa sh.milioni 621.7.
“Ankara ambazo hazikuonekana kwenye hospitali za Rufaa za mikoa ni sh. bilioni 1.1,bidhaa zilizokosa ushahidi wa kutoka bohari ya hospitali kwenda kwenye idara husika ya kutolea huduma ni sh.bilioni 3.2,bidhaa ambazo zilitolewa hospitali za rufaa za mikoa kwenda vituo vingine kama msaada na hazikufika huko ni sh. milioni 354.7 na bidhaa zilizokosa ushahidi wa kufika kwa wateja au wagonjwa kwenye vitengo vya kutolea huduma ni sh. bilioni 2.4.
“Bidhaa zingine ni zilizonunuliwa kwa washitiri bila kuwa na ushahidi wa kukosekana bohari ya dawa ni sh.bilioni 5.6,bidhaa zilizonunuliwa nje ya bohari ya dawa na washitiri teule wa hospitali husika ni sh. bilioni 1.12,bidhaa zilizonunuliwa na washitiri kinyume na makataba sh.milioni 640.2,”ameanisha Dkt.Gwajima.
Ameongeza kuwa, bidhaa zingine ni zile zilizonunuliwa bila kuidhinishwa na kamati ya dawa ya tiba ambazo gharama yake ni sh.bilioni 1.9.
“Hasara ya fedha itokanayo na kukosekana kwa dawa kwa wateja wa bima na kuwaelekeza kupata dawa hizo nje ya hospitali jambo ambalo linaweza kuzuilika ni jumla ya sh.bilioni 6.1,hasara itokanayo na makato ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) yaliyosababishwa na makosa mbalimbalia ya kitaalamu ambayo yangeweza kuzuilika ni sh. bilioni 2.4.
“Bidhaa kumaliza muda wake wa matumizi huku vituo vingine vikiwa na uhitaji ni sh.milioni 714.9,bidhaa kununuliwa kwa kutumia masurufu bila kufuata utaratibu ni sh.milioni 124.5,hospitali kutokulipwa kwa kuhudumia wagonjwa wa mifuko mingine ni sh.milioni 321.
“Hospitali 26 kati ya 28 kutumia asilimia ndogo ya fedha kununua bidhaa za afya hususani dawa na vitendanishi kwa asilimia 35 chini ya asilimia 50 iliyoelekezwa na mwongozo wa wizara na hospitali nyingi kukosa takwimu za wanaotibiwa kwa msamaha huku saba zilizokutwa na takwimu kuonesha kuwa msamaha ni asilimia tisa hadi asilimi 12 tu tofauti na maelezo kuwa ni asilimia 60 hadi 70,”amefafanua Dkt.Gwajima.
Kutokana na hilo, Dkt. Gwajima alimuagiza katibu mkuu kuanzisha hatua za kinidhamu dhidi ya kila mtumishi aliyeenda kinyume na sheria na kanuni za ununuzi na ugavi.
“Na pia aunde kamati kwa kushirikiana na ofisi ya Rais TAMISEMI kufanya mapitio ya mikataba ya washitiri wa bidhaa za afya nchini,aratibu zoezi la maboresho ya miongozo ya ushirikiano na ofisi ya Rias TAMISEMI na makatibu tawala wa mikoa.
“Ndani ya siku 14 kuanzi leo Machi 1 (jana) anipatie taarifa ya utekelezaji inayojibu masuala yote yaliyoibuliwa kwa kuwa yametokea wakati huko kuna waganga wakuu wa halmashauri na mikoa husika wanaoiwakisha wizara na yafanyike mapitio ya ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya bodi zote za ushauri wa hospitali za mikoa kubaini kwanini zimeshindwa kutimiza wajibu wao,”ameagiza Dkt.Gwajima.
Pia amesema zoezi hilo litakuwa endelevu katika hospitali mbalimbali hapa nchini ikiwemo Taifa na zile za Rufaa za Kanda.
More Stories
Watakiwa kushirikiana kutikomeza matatizo ya lishe
CCBRT yazidi kuunga mkono juhudi za Rais Samia
Madaktari bingwa wa Samia watua Rukwa