May 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UAE yamtunuku Rais Samia Medali ya juu kabisa

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan ametunukiwa Medali ya Mother of the Nation Order kutoka kwa Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu Mtukufu Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan.

Medali hiyo iliwasilishwa kwake na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Sheikh Abdullah Bin Zayed Al Nahyan Ikulu Jijini Dar es Salaam, jana Mei 5, 2025.

Aidha, Medali hiyo ni moja kati ya Medali za juu kabisa kutoka kwa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Medali hiyo hutolewa kutambua mchango Kiongozi katika kuleta maendeleo endelevu kwa jamii yake.

Serikali ya UAE imetambua mchango mkubwa wa Rais Dkt. Samia katika kuwaletea Watanzania maendeleo endelevu ambayo yanaendana na Sera za UAE za maendeleo endelevu katika kijamii, uwezeshaji wanawake na ushirikiano wa kimataifa.

Sheikh Abdullah aliwasilisha salamu kutoka kwa Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu Mtukufu Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan na kuwatakia kheri wananchi wa Tanzania katika maendeleo pamoja na ustawi zaidi.

Pia alisisitiza kuimarishwa zaidi uhusiano wa kudumu baina ya nchi hizo mbili na kusisitiza umuhimu wa kupanua ushirikiano katika sekta muhimu.