Na Raphael Okello, Timesmajira Online,Bunda.
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Mji wa Bunda mkoani Mara, Emmanuel Mkongo ameishukuru Timu nzima ya TWENDE BUTIAMA kwa kuichangia shule ya msingi Nyerere madawati 70 yenye thamani ya zaidi ya milioni 5.
TWENDE BUTIAMA pia imetoa miche ya miti 1,000 itakayopandwa katika shule hiyo ikiwa ni kampeni yao yakumbukizi ya miaka 24 ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Msafara wa Twende Butiama ulianza safari ya kuendesha baiskeli kutoka Jiji la Dar es salaam kuelekea Butiama ambapo jana umefika Wilaya ya Bunda katika Halmashauri ya Mji wa Bunda na kuweka kambi katika shule ya Msingi Nyerere.
Mkongo ameishukuru Timu ya Twende Butiama kwa heshima waliyoipatia Wilaya ya Bunda kwa kuwa sehemu ya malengo yao.
Aidha, Mkongo amewasihi kuendelea kuenzi kwa vitendo fikra za Mwalimu Nyerere za kudumisha upendo,umoja,amani na kuendelea kupambana na maadui watatu ambao ni ujinga, maradhi na umasikini.
Mwenyekiti wa mbio hizo za Twende Butiama, Gabreil Landa amesema kwamba mbio hizo zimefikisha miaka mitano toka kuanzishwa kwake mwaka 2019 na malengo yake makuu matatu yakiwa ni kudumisha amani,umoja, mshikamano na upendo.
Lengo la pili ni elimu kwa kuhamasisha Watanzania kuchangia katika Elimu na mwisho suala la mazingira kwa kuhamasisha wananchi kutunza mazingira kwa kupanda miti ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Ameongeza kuwa tangu waanze msafara huo wa kwenda Butiama wameshatoa zaidi ya madawati 300 katika maeneo yote waliyopita ambapo kwa shule ya Msingi Nyerere wametoa madawati 70.
Twende Butiama imekua na wadhamini mbalimbali ambapo mdhamini mkuu kwa mwaka 2023 ni kampuni ya vodacom ambao wamesaidia kupatikana kwa madawati hayo pamoja na miti 1,000 ya kupandwa.
Awali akisoma risala yale Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Nyerere, Edwine Byangwamu ameishukuru kampeni ya Twende Butiama ambao wamekuwa na mchango mkubwa sana katika shule hiyo.
Msafara wa Twende Butiama ni mara ya tatu wamefika shule ya msingi Nyerere na kufanya matukio mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupanda miti.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dkt. Vicent Anney amempongeza Joseph Juma Keraryo kwa kuweza kuikumbuka shule yake ya Msingi na kuweza kurudisha fadhila kwa kutoa mashine ya kutolea kopi, Kompyuta, Rimu na kufanya sherehe ya pamoja na walimu kwa kutoa zawadi kwa kila mwalimu.
Mkuu wa Wilaya amesema Joseph ameunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kuboresha elimu.
Aidha, Dkt. Anney ameutaka uongozi wa shule hiyo kuvitumia vizuri vifaa hivyo ili viwe chachu ya kuinua taaluma katika shule hiyo kwa kutoa machapisho ya mitihani na mazoezi mbalimbali na kuwataka wanabunda kuiga mfano huo.
Joseph Keraryo ambaye alihitimu darasa la saba katika shule hiyo mwaka 2011 amesema yeye ameamua kufanya hayo ili kuongeza nguvu katika kuwaandaa wanafunzi wa shule yake ya zamani ili kuchangia kuboresha shule hiyo.
Joseph amesema ametumia zaidi ya milioni sita ambapo amewashauri vijana wenzake kuacha alama nzuri katika maeneo wanayoishi, wanayofanya kazi, wanakoabudu au katika shule walizosoma ili kuunga mkono juhudu zinazofanywa na Serikali kuleta Maendeleo nchini.
More Stories
Mwalimu adaiwa kumfanyia ukatili mwanafunziÂ
NAOT watakiwa kuendana na viwango vya ukaguzi
Rais Samia kuzindua mfuko wa kuendeleza kazi za wabunifu