January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tuzo za michezo zaleta
chachu Sekta ya Michezo

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira

Serikali imesema, itaendelea kuwathamini na kuwatambua Wanamichezo katika maeneo mbalimbali nchini, kutokana na kazi kubwa wanayoifanya katika Sekta hiyo ndani na nje ya nchi.

Akizungumza wakati wa Halfa ya Utoaji Tuzo za Michezo zilizoandaliwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Machi 17 mwaka huu, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Dkt. Pindi Chana amesema Tuzo hizo ni chachu kwa wachezaji kufanya vizuri zaidi katika siku za usoni na kuiletea Heshima Tanzania.

“Natumia nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kukutana mahali hapa kwa ajili ya kusherehekea mafanikio ya wanamichezo wetu waliong’aa na kuiwakilisha nchi vyema katika mashindano mbalimbali ya Kimataifa,” amesema Balozi Dkt. Chana

Ametumia nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kuleta maendeleo katika sekta ya michezo, ikiwemo kuwezesha gharama za Kocha wa Timu ya Taifa ( Taifa Stars)

Dkt. Pindi Chana ametaja baadhi ya mafanikio katika Sekta hiyo, kufanikiwa kwa timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu kwa Wasichana chini ya umri wa miaka 17 (Serengeti Girls) pamoja na Timu ya Watu wenye Ulemavu ( Tembo Worrios) ambazo zilifuzu kushiriki Kombe la Dunia na kufanikiwa kufika hatua ya Robo Fainali

Mafanikio mengine ni Timu za Riadha na Ngumi zilizoshiriki mashindano ya Jumuiya ya Madola mwaka 2022 ambazo ziliibuka na medali tatu na Timu ya Taifa ya Mchezo wa Gofu kwa Wanawake kuibuka mshindi wa tatu kwenye mashindano ya All Africa Challenge Trophy.