Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
KUBORESHWA kwa huduma ya maji safi katika halmashauri ya manispaa Tabora kumeleta neema kubwa kwa wananchi baada ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Tabora (TUWASA) kutoa ofa ya kurejeshewa huduma wale wote waliokatiwa.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo Mhandisi Mayunga Kashilimu alipokuwa akiongea na vyombo vya habari ofisini kwake ambapo alisema ofa hiyo itasaidia kupanua wigo wa utoaji huduma kwa wateja.
Alisema Mamlaka hiyo ina jumla ya wateja 32,184 waliounganishiwa huduma hiyo Mjini Tabora na kati yao wateja 26,000 hadi 27,000 ni watumiaji wazuri na 5,000 hawajalipia ankara zao kwa muda sasa hali iliyopelekea kukosa huduma
Alibainisha kuwa ofa hii ni promosheni maalumu ya wiki ya maji na imeanza Machi 16 mwaka huu na itaendelea hadi Aprili 15 mwaka huu ambapo wale wote waliositishiwa huduma watarejeshewa bure ila watatakiwa kulipa nusu ya deni lao na nyingine watalipa kidogo kidogo hadi Juni.
Mhandisi Mayunga aliongeza kuwa waliokatiwa huduma kutokana na kuharibika miundombinu ndani ya mita 15 watatakiwa kulipia sh 150,000 na kuwekewa miundombinu mipya ila kuendelea kupata huduma hiyo
Alitaja wengine watakaonufaika na ofa hiyo kuwa ni wateja wapya ambao watatakiwa kulipia sh 150,000 kwa mkupuo mmoja na kuunganishiwa ndani ya siku 7 za kazi na waliokatiwa huduma isiyozidi umbali wa mita 50 nao watalipia 150,000 tu na kuwekewa miundombinu mipya.
‘Hii ni fursa muhimu sana kwa wananchi wote kuwa na huduma ya maji safi nyumbani kwao na sio kwenda kwenye vibanda vya mitaani, changamkieni fursa hii adimu’, alisisitiza.
Aidha kwa wale waliositishiwa huduma baada ya kubainika kutumia maji kinyume na taratibu ikiwemo wizi, uharibifu wa miundombinu na walio na madeni makubwa zikiwemo taasisi za umma, alisema hawatahusika na ofa hiyo.
Naye Meneja Biashara wa Mamlaka hiyo Bernard Biswalo aliwataka wateja kuwa makini na vitendo vya wizi wa mita ambavyo vimekuwa vikijitokeza katika maeneo mbalimbali na kuwataka kutoa taarifa za uharibifu huo ikiwemo kufichua wanaohusika na vitendo hivyo.
More Stories
CP.Wakulyamba ashuka Katavi na Nguzo nne za Uongozi
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Maandalizi ya mkutano mkuu CCM yapamba moto