July 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tutunze mazingira kwa kutumia Nishati Mbadala

Na Frank Abel, TimesMajira Online


Mkaa ni moja ya vyanzo vya nishati ya kupikia vinavyotegemewa na watu wengi nchini Tanzania.

Inakadiriwa asilimia 88 ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam wanatumia mkaa kama chanzo kikuu cha nishati ya kupikia (NBS, 2017a).

Ukataji wa misitu kwa ajili ya shughulI mbalimbali za kiuchumi ikiwemo uchomaji mkaa umepelekea Tanzania kuwa nchi ya tano duniani katika orodha ya nchi zinazopoteza misitu yake kwa kasi kubwa huku ikiongoza katika ukanda wa nchi za Afrika ya Mashariki (FAO, 2015).

Kutokana na mwenendo wa ongezeko la idadi ya watu, inakadiriwa ifikapo mwaka 2030, matumizi ya mkaa kwa ajili ya kupikia nchini Tanzania yataongezeka maradufu kutoka makadirio ya tani milioni 2.3 kwa mwaka 2012 (Sera ya Taifa ya Nishati, 2015).

Mwenendo huu unaashiria hitaji la haraka la mikakati madhubuti ya kupunguza au kuondoa kabisa ukataji miti kwa ajili ya uchomaji wa mkaa.
Ukataji misitu kwa ajili ya kuchoma mkaa una athari nyingi sana katika nyanja mbalimali.

Kiuchumi, ukataji misitu unaathiri mchango wa sekta ya misitu kwenye pato la Taifa ambapo kwa mwaka 2010 ulikuwa ni asilimia 4 (FAO, 2014; NBS, 2017b). Kiafya, matumizi ya mkaa unaotengenezwa na miti iliyokatwa katika misitu unasababisha madhara na magonjwa mbalimbali yanayopelekea vifo vya watu na viumbe mbalimbali.

Kwa mfano kwa mwaka 2020 pekee, shirika la afya duniani (WHO) liliripoti kwamba takribani vifo milioni 3.2 vya watu duniani vilisababishwa na magonjwa yanayosababishwa na hewa ukaa inayotokana na shughuli za majumbani. Kimazingira, ukataji misitu na uchomaji mkaa unaathiri uoto wa asili na hivyo kuhatarisha maisha ya viumbe mbalimbali.

Pia ukataji miti unasababisha ukame unaoathiri sekta mbalimbali kama kilimo, mifugo, nishati ya umeme na vyanzo vya maji ambavyo vikiharibiwa vinasababisha ukosefu wa maji katika jamii unaoweza kusababisha magonjwa mbalimbali ikiwemo kipindu pindu.

Kumekuwa na jitihada mbalimabi za serikari na wadau mbalimbali katika kupunguza na hatimaye kukomesha kabisa matumizi ya mkaa unaotokana na ukataji wa miti.

Serikali imekuwa mstari wa mbele kwa kuhakikisha inasambaza umeme katika vijiji vyote vya Tanzania kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA). Hata hivyo, uzoefu unaonyesha watanzania wengi hawatumii umeme kwa kupikia kwa hofu ya gharama za matumizi kuwa kubwa.

Elimu ya uelewa (Public Awareness) inatakiwa iendane na jitihihada za usambazaji wa umeme. Hii itasaidia upatikanaji wa umeme vijijini uendane na matumizi ya umeme katika kupika hili kupunguza na kuondoa kabisa matumizi ya mkaa.

Serikali pia kwa kushirikiana na sekita binafsi imeendelea kuhakikisha kuna upatikanaji wa kutosha wa gesi ya kupikia. Mikakati kama nishati safi ya kupikia (Clean Cooking Energy) inayoendeshwa na Wizara ya Nishati ni ya kupongezwa. Hata hiyo, ni ukweli usiopingika kwamba hata kama familia zote za kitanzania zitapewa mitungi ya gesi, sio zote zitaweza kugharimia gharama ya kujaza gesi kila itapoisha hasa kwa wale wa kipato cha chini.

Kwa ufanisi, ni vizuri jitihada hizi zikaenda sambamba na jitihada za kupata mbadala wa nishati hii muhimu kwa kaya za kipato cha chini kwa kutumia njia na teknolojia rafiki, rahisi na ambayo watakaoshindwa kununua gesi wataitumia bila kuwa na athari kubwa kwenye mazingira, afya zao na na uchumi wao.

Katika ufuatiliaji mdogo nilioufanya, nimegundua ziko bunifu (innovations) mbalimbali za watu binafsi, mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali pamoja na vikundi mbalimbali ambazo kama zikiratibiwa vyema, zinaweza kukomesha kabisa ukataji wa miti kwa ajili ya kuchoma mkaa na kuongeza ajira kwa vijana na wakinamama.

Bunifu hizi ziko kwenye makundi makubwa mawili, kundi la kwanza ni la wabunifu wanaotengeneza majiko yanayoweza kutumia umeme mdogo sana wa TANESCO au solar kutoa nishati ya kupikia kwa kutumia aidha mawe, kokoto, matofari au udongo vinavyosaidiwa na chenga chenga chache sana za mkaa (Majiko banifu).

Kundi la pili ni la watu na mashirika binafsi wanaotengeneza mkaa mbadala kwa kutumia mabaki ya mazao na misitu pamoja na takataka zinazozalishwa katika jamii.

Majiko banifu ni majiko ambayo yanapunguza matumizi ya mkaa kwa asilimia 70-90 huku yakitumia umeme mdogo sana unaolingana na umeme wa kuchaji simu.

Tekinolojia hii ikifanyiwa kazi ikaingizwa kwenye mkakati wa kupunguza matumizi ya mkaa inaweza kuokoa asilimia 70-90 ya miti inayokatwa kila mwaka kwa ajili ya kutengeneza mkaa.

Ni tekinolojia rafiki, rahisi kutumia kwa mtu yoyote mwenye umeme wa TANESCO na asiye na umeme anaweza kutumia solar ndogo yenye gharama nafuu kabisa. Malighafi zingine kama mawe, matofari, udongo na kokoto zinapitikana kwa wingi katika maeneo mbalimbali nchini.

Wabunifu wa majiko banifu wanasema changamoto zinazowakabili ni pamoja na uelewa mdogo wa manufaa ya majiko haya kwa wananchi, uwezo mdogo wa uzalishaji kutokana na kutokuwa na mitaji mikubwa na gharama ya vifaa ya utengenezaji wa haya majiko.

Ikiwa hawa wabunifu wataratibiwa kwa maana ya kutafutwa, kusilkilizwa na kuwasaidia kutatua changamoto zinazowakabili, wataweza kuzalisha majiko ya kutosha .

Kama kila kaya ya kitanzania ikiwa angalau na jiko banifu moja, tunaweza kuokoa asilimia 70-90 ya misitu inayokatwa kila mwaka kwa ajili ya kuchoma mkaa maana matumizi ya mkaa yatapungua sana.
Kundi la pili ni la wadau wanaojihusisha na utengenezaji wa mkaa mbadala.

Hawa wanatumia aidha mabaki ya mimea,mabaki ya misitu au takataka zinazozalishwa katika jamii. Kundi hili limekuwa na mchango mkubwa sana kwenye jamii na uchumi wa nchi katika maeneo makubwa matatu.

Kwanza, linapunguza matumizi ya mkaa unaotokana na kukatwa kwa misitu. Pili, kundi hili linasaidia kupunguza taka zilizoko kwenye jamii hivyo kuepusha magonjwa ya milipuko na yasiyo ya milipuko. Tatu, kundi hili linasaidia kutatua tatizo la ajira kwa vijana na wakinamama.

Wako wadau mbalimbali katika kundi hili ambao kama wakiratibiwa vizuri kwa kutafutwa, kuwekwa pamoja, kusililizwa na kutatua changamoto wanazokabiliana nazo katika uzalishaji wa mkaa mbadala, tunaweza kupata faida tatu kwa wakati mmoja ambazo ni kupunguza ukataji miti, kuondoa taka mitaani na kutengeneza ajira kwa watu wetu.

Mkaa huu unatengenezwa kitaalamu na uzalishaji na matumizi yake hayana madhara makubwa kama mkaa wa kawaida unaotokana na uchomaji miti.

Wabunifu hawa wanaotengeneza mkaa mbadala pia wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo ni kama uelewa mdogo wa watu kuhusu faida za mkaa mbadala, mahitaji kuwa makubwa kuliko uwezo wa uzalishajii na uhaba wa mitaji ya kuzalisha zaidi hili kukidhi mahitaji ya soko.

Kwa watumiaji wa mkaa mbadala wanatoa ushuhuda kwamba ni mkaa wenye uwezo mkubwa wa kupika kwa haraka na unadumu kwa muda mrefu na pia wanaokoa fedha ukilinganisha na matumizi ya mkaa wa kawaida. Malighafi za uzalishaji wa mkaa mbadala ziko za kutosha na zinapatikana kila mahali palipo na shughuli za kibinadamu.

Mfano, vijijini kuna mabaki ya mazao ya kutosha ambayo yasipotumika yanaharibika na hatimaye kutumika kama mbolea.Kwa mijini taka zinazozalishwa ni nyingi kiasi cha kutosha kuzalisha mkaa mbadala mwingi sana.

Shirika lisilo la kiserikali la Amref Heath Africa Tanzania (Amref) ni mmoja wa wadau ambao kupitia msaada kutoka kwa wafadhili walifanikiwa kuendesha mradi wa ukusanyaji wa taka na kuzitumia kuzalishaji mkaa mbadala kupitia mradi unaoitwa TAKA NI MALI uliotekelezwa katika Manisipaa ya Ilala jijini Dar es salam.

Mradi huu ulitekelezwa kwa kushirikiana na uongozi wa Manisapaa husika na viongozi wa kata husika ambazo mradi ulikuwa ukitekelezwa.Kwa Dar es salaam mradi huu ulitekelezwa kata za Vingunguti, Kiwalani, Buguruni na Kipawa. Mradi huu ulitumia vikundi vilivyokuwepo vya ukusanyaji taka na kuvijengea uwezo wa namna ya kuzibadili taka kuwa mali.

Upo Ushahidi wa kutosha kwa wanavikundi hawa na uongozi wa Afya katika Manispaa zilizotekeleza mradi huu namna ambavyo mradi huu umeleta manufaa makubwa. Manufaa waliyoyapata ni kama kuondoa taka zilizokuwa zinabaki mitaani hivyo kupunguza magonjwa ya mlipuko, kuongeza ajira na kipato kwa wanavikundi pamoja na kupunguza matumizi ya mkaa unaotokana na kukatwa kwa miti.

Kama zitafanyika jitihada za makusudi za kuhakikisha kila kaya inakuwa na jiko banifu wakati huo huo tukigeuza taka zinazozalishwa na shughuli mbali mbali za kibinadamu kuwa mkaa mbadala, kwa hakika hakuna mti utakatwa kwa ajili ya kuchoma mkaa.

Hili litawezekana tu kama serikali na wadau mbalimbali wataamua kuunganisha nguvu na kuunda kamati au mradi utakaoratibu bunifu zilizopo na kuweka mkakati thabiti wa kisera na kibiashara wa kuzitumia kuondoa hili tatizo.

Tunaweza kuanza na jiji la Dar es salaam ambapo takwimu zinaonyesha ndiko aslimia kubwa ya mkaa unauzwa na kutumika.

Hata katika jiji la Dar es salaam pia tunaweza kuanza kwa awamu tukianza na maeneo ambayo taka zinapatikana kwa wingi kama masoko ya Kariakoo, Mabibo, Tandika na mengineyo kabla ya kusambaa katika maeneo mengine.

Tanzania ikiwa moja kati ya nchi zinazoendelea, inabidi iwe na mikakati madhubuti ya kuhakikisha inabidili changamoto zinazoikabiri jamii kuwa fursa. Ukataji wa miti kwa ajili ya kuchoma mkaa ni changamoto ambayo ikifanyiwa kazi kimkakati kama ilivyoelezwa hapo juu inaweza kuwa fursa ya ajira, fursa ya kuondoa taka mitaani ambazo zinaweza kuleta magonjwa lakini pia fursa ya kuibua,kulea na kukuza vipaji na hali ya watanzania kuwa wabunifu katika kutatua matatizo yanayoikabili jamii yao.

Ninatoa wito kwa Serikali kuchukua hatua hili kuratibu bunifu zote zilizoko kwenye hii sekta kwa kutengeneza mazingira rafiki ya kusaidia mikakati hii kuzaa matunda.

SerikalI inaweza kusaidia uratibu wa hizi bunifu kwa kutumia taasisi zake kama VETA, SIDO, NACTE, NEMC, serikali za mitaa (Halimasahuri za Miji na Manisapaa), vyuo mbalimbali vya ufundi na taasisi zake nyingine.

Pia inaweza kuwaomba wadau wa maendeleo wanaotoa ufadhili kwenye eneo la mazingira kutoa kipaumbele kwenye mkakati huu.

Natoa pia wito kwa taasisi za fedha kuona namna ya kuwasaidia wabunifu hawa kupata mitaji ya kuwawezesha kusambaza tekinolojia hii kwa watanzania wengi ili kunusuru mazingira yetu.

Natoa pia wito kwa Mashirika yasio ya kiserikali kuungana na serikali na sekta binafsi kwa kutoa utaalamu na uzoefui wao katika kufanikisha mikakati hii muhimu ya kukomesha uzalishaji mkaa wenye madhara kwa mazingira.

Tunaweza pia kufikiria namna ya kuanzisha mfuko wa mazingira (Trust Fund) utakaokuwa na lengo la kusaidia kuratibu na kuendeleza wabunifu watakaoleta suluhisho la matatizo ya tabia nchi tunayoendelea kuyashuhudia. Mfuko huu unaweza kuchangiwa na mapato mbalimbali yanayotokana na mazao ya misitu na faini za mazingira. Pia inaweza ikatengenezwa namna ya sekta binafsi na wadau mbalimbali wa maendeleo kuchangia.

katika mfuko huu. Kwa wabunifu wanaotengeneza bidhaa au kutoa huduma zinazosaidia kupunguza uharibifu wa mazingira wanaweza kupewa ruzuku au motisha kupitia mfuko huu.

Mfuko pia unaweza kuwasaidia wabunifu kukopa fedha katika mabenki kwa ajili ya kuwasaidia kuongeza uzalishaji wa bidhaa ambazo zitathibitishwa kuwa na msaada katika kuokoa mazingira.

Mwandishi wa Makala hii ni mdau wa maendeleo endelevu, anaitwa Frank Abel na anapatikana kwa kwa namba ya simu +255 753 732 355 na barua pepe ni Abelfrank54@yahoo.com.