January 18, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tutazame mbele kutimiza maono ya hayati Dkt.Magufuli

Na Stephano Mango,TimesMajira online

BADO Watanzania na Waafrika kiujumla hawaamini kama aliyekuwa Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli amefarika na amezikwa katika makaburi ya Familia nyumbani kwake Wilayani Chato.

Ukiwasikia mazungumzo yao katika vijiwe mbalimbali nchini ambako walikuwa wanafuatilia hatua kwa hatua matukio ya kuaga mwili wake utashuhudia wazi kuwa bado wananchi hawaamini kilichotokea,

Vilio na majonzi vilitawala wakati wa kumuaga sehemu mbalimbali nchini ambapo shughuli ya kutoa heshima ya mwisho kwa kiongozi huyo alieonekana kuwa na misismamo ya kujitegemea kiuchumi zilifanyika huku baadhi ya wananchi wakibeba mabango mbalimbali ambayo yalikuwa yanamuelezea namna alivyolitumikia Taifa.

Lakini ukweli utabaki kuwa tumempoteza rais wetu kipenzi aliyejitoa kuwatumikia Watanzania wote kwa uadilifu, umahiri, bidii na moyo wa uzalendo wa hali ya juu.

Nuru ya urithi wa uzalendo na kujitolea kwa ajili ya Uafrika itaendelea kukumbukwa kote barani Afrika kwani alitumia muda wake mwingi zaidi wa maisha yake kulitumikia taifa na ubinadamu kama vile yalivyo maagizo ya katiba ya nchini na miongozo ya dini zetu.

Hayati Magufuli atakumbukwa kwa mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupunguza ukubwa na gharama za utawala, kusisitiza kuhusu bajeti inayowalenga watu,yenye vipaumbele vya wazi kuhusu elimu na afya, na kupambana wakati wote na ubadhirifu katika matumizi ya umma.

Pia alikabiliana na kufuta maelfu ya wafanyakazi hewa kutoka katika mfumo wa malipo ya serikali na ‘kuwatumbua’ hadharani maafisa waliotuhumiwa kwa ufisadi ama kutofikia viwango vya ufanisi vilivyotakiwa.

Alikuwa kiongozi mwenye maono wa Tanzania,pia alikuwa anaamini katika ujasiri na upendo kwa nchini jambo ambalo vizazi vitaendelea kuyakumbuka mambo hayo kikamilifu.

Pia alikuwa ni ishara kuu ya ufufuo wa uchumi wa Afrika, na kifo chake ni pigo kubwa kwa bara hili kwani alikuwa kiongozi ambaye anaongoza kwa uhalisia na aliyeamini katika kukuza uchumi wa Afrika Mashariki.

Rais Magufuli kama mtu aliependa kutenda haki kwa kila tabaka la watu, hivyo kulitolea mwito taifa kuja pamoja katika kipindi hiki kigumu kwa taifa.

Katika kipindi hiki kigumu viongozi mbalimbali wa dini wametutaka tuliombee taifa ambalo Hayati Magufuli alilipenda na kulihudumia kwa nguvu zake zote, kusudi taifa liendelee kuwa na umoja,liendelee kujituma, liendelee na utawala wa haki, kushughulikia usawa utu na maendeleo ya raia wake.

Rais wetu alivyokuwa mtetezi wa wanyonge ameweza kusaidia watu waliokuwa wamedhulumiwa,na kuna mambo mengi sana ambayo tulikuwa tunategemea kuwa hii miaka mitano inayokuja atafanya makubwa zaidi.

Kwa kweli ni pigo kubwa sana kwa Watanzania, na hata dunia nzima kwa kuwa walikuwa wanajua ni mtu aliyekuwa anatenda kazi nzuri sana, ni mtu aliyetoa uhai wake kwa ajili ya wanyonge kwa miaka mitano iliyopita amefanya mengi sana,

Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuimarika kwa nidhamu kwa Watumishi wa Umma; mabadiliko ya hali ya uchumi; kutekelezwa kwa miradi ya maendeleo; kuongezeka kwa mapato ya ndani; kupungua kwa rushwa, kuimarika kwa Muungano wetu na kushughulikiwa kwa migogoro ya ardhi.

Serikali yake iliweka dhamira ya kuwahudumia wananchi wote hususan maskini kwa kuwapelekea miradi ya maendeleo na huduma muhimu za jamii ili kufikia azma hiyo ilibidi kujenga nidhamu ya watumishi wa umma kwa kubaini wazembe, wabadhilifu,

Wezi wa mali na fedha za umma,wala rushwa mahali pa kazi na wasio tayari kuwatumikia wananchi na hasa wanyonge; na kusimamia mwenendo wa uchumi kwa kuongeza uzalishaji mali na kukusanya mapato.

Pia Serikali ilitilia mkazo sekta ya kilimo ili kukifanya kilimo kuwa cha kisasa,chenye tija na cha kibiashara ambacho mazao yake yaliongezwa thamani,jambo hilo lilifanikiwa kwa serikali kuimeimarisha upatikanaji wa pembejeo na zana za kilimo,

Kuimarisha huduma za ugani, kuimarisha huduma za umwagiliaji, kuwezesha upatikanaji wa masoko na kuhamasisha Sekta binafsi, vyama vya ushirika na kanzisha viwanda vya kusindika mazao ya kilimo.

Aliyewahi kuwa Rais kijana wa Marekani John Fitzqerald Kennedy alipochaguliwa kuwa Rais wa nchi hiyo aliwaambia wamarekani wenzake kuwa “usiulize Marekani itakufanyia nini, bali jiulize wewe utaifanyia nini marekani”.

Ni swali muhimu sana ambalo kila Mtanzania mwenye umri,afya na uwezo wa kuchangia jambo kwa maendeleo yake binafsi na jamii kiujumla anaweza kufanya jambo lenye maslahi kwa nchi yake.

Ni lazima Watanzania sasa tubadilike na tuwe na tija kwa taifa na jamii zetu badala ya kushinda katika vijiwe tukicheza kalata, kamali, kuangalia mpira huku tukibeza juhudi zinazofanyika na viongozi sambamba na kuzusha mambo ya uongo ambayo licha ya kulidharirisha taifa bali pia linatuzalilisha sote nawe ukiwemo.

Ili taifa lipige hatua tunahitaji tuungane kwa kufanya kazi kwa bidii ili tuweze kupata kipato cha kuendesha maisha ya kila siku ya familia na tuweze kuchangia nguvu kazi zetu kwa taifa letu.

Ni muhimu kuwa raia mwenye tija kwa taifa kuliko kuwa raia wa kukosoa na kulalamika bila kuwa na mchango wowote ambao utasaidia kuboresha hali ambayo inalalamikiwa kwani kila taifa linapaswa kujengwa na raia wake.

Tubadilike na kujenga uzalendo wa kujali maslahi ya taifa dhidi ya maslahi binafsi na kuendelea kuhubiri umoja wa kitaifa kwa lengo la kuhakikisha tunasonga mbele kama taifa katika mapambano ya kujikwamua kiuchumi kutoka kwenye makucha ya mabeberu.

Hivyo basi viongozi wetu kufanya kazi na kutekeleza ahadi zao kwa kuzingatia katiba na sheria za nchi kwakuzingatia haki ni suala muhimu sana katika kukuza demokrasia na jamii yenye ustawi stahiki.

Kwa sababu maendeleo ni kupiga hatua kutoka nafasi moja kwenda nyingine katika uelekeo chanya, licha ya kuwa maendeleo ni neno la jumla na ni neno pana sana

Na kwamba maana halisi ya maendeleo inategemea unazungumzia maendeleo ya kitu gani, kama vile maendeleo ya uchumi, kiteknolojia, kijamii, kibailojia aula

Kiuhalisia kila aina ya maendeleo huwa na maana yake ambayo ni mahususi katika mazingira ama eneo husika tu na msingi wa maendeleo yoyote yale katika taifa ni matokeo ama zao la kutenda haki kwa raia wake ambao ndio walengwa wa maendeleo yenyewe.

Maendeleo na haki ni vitu ambavyo vinaendana,ingawa haki inatangulia maendeleo kwa maana unapokuwa mwanajamii fulani basi wewe una haki katika jamii hiyo na ni haki yako kuendelea na kushiriki katika shughuli zote za maendeleo.

Haki ninayoijadili hapa si haki ya awali yaani haki ambayo mtu anayoipata kwa kuzaliwa mfano haki ya kuishi, kuwa mwanajamii au mwanafamilia wa ukoo fulani.

Si hivyo, kwa sababu hizo ni haki ambazo dola haliwezi kukuondolea na ikitokea hivyo, basi dola hiyolinakuwa imeondoa uhalali wake wa kuwepo kwa binadamu.

Katiba ndio makubaliano ya wananchi husika hivyo kama waliamua vyema, watatekeleza vyema, watalinda vyema na watawajibishana vyema na hatimaye wataendelea vyema kama walivyokubaliana toka mwanzo na kamwe hakuna mtu ambaye atabaki salama kama atavuruga utaratibu huo ambao umekubaliwa na wengi.