October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tutahamasisha kampuni kuanzisha timu – Mkenge

Na Omary Mngindo, TimesMajira Online, Bagamoyo

MGOMBEA Ubunge Jimbo la Bagamoyo Mkoa wa Pwani Muharami Mkenge, amesema endapo atachaguliwa kushika nafasi hiyo, mbali ya shughuli za kiuchumi pia atahakikisha anakaa na wamiliki wa Makampuni mbalimbali yaliyopo ndani ya jimbo hilo ili kuanzisha timu za michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu.

Malengo yake ni kuhakikisha kuwa Bagamoyo inarejesha heshima yake ya michezo, ukizingatia kuwa sekta hiyo ina mchango mkubwa kiuchumi kwani kunapokuwepo na michezo wakazi wanatumia fursa hiyo kufanya biashara mbalimbali.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mataya Kata ya Kiromo, amesema kuwa wapo wamiliki wa Makampuni wa viwanda na Taasisi wanaopenda michezo lakini wanakosa uhamasishaji, hivyo moja ya kazi atakayoifanya itakuwa ni kuhamasiha makampuni na taasisi hizo kuanzisha timu.

“Tumeshuhudia vijana wengi wana ajiliwa katika viwanda au makampuni kupitia taaluma zao walizosomea, lakini pia sekta ya michezo nayo ni taaluma hivyo uwepo wa makampuni yatayokuwa na timu vijana wetu wengi wenye vipaji watapata ajira kupitia vipaji hivyo,” amesema Mkenge.

Amesema, tayari kampuni ya Bagamoyo Sugar inayolima miwa eneo la Makurunge Razaba wakati inajiandaa na uzalishaji wa Sukari, imeshaanza uandaaji wa viwanja kwa ajili ya michezo hatua inayoonesha dhamira ya uundwaji wa timu ambazo zitazokuja kuhamasisha ushindani katika medani hiyo.

“Oktoba 28 nikifanikiwa kuchaguliwa kushika nafasi hii, katika kipindi changu cha miaka mitano nitatamani sana kuliona Jimbo la Bagamoyo linarejesha heshima yake katika michezo, nazikumbuka baadhi ya vilabu kama Black Magic, Mbegani Fc, Coast Star, The Winners na Chafosa na vingine vingi ziliitangaza sana Bagamoyo,” amesema Mkenge.

Amesema kuwa, zoezi hilo litakwenda sanjali na kukutana na viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Bagamoyo BFA, pia kwa upande mwingine na viongozi wa klabu ili kuzungumzia mikakati ya uboreshwaji wa Ligi Daraja la Nne ngazi ya Wilaya.

“Juzi kati nilishuhudia michuano ya Umoja Cup pale Matimbwa Kata ya Yombo, ambapo nimeambiwa yanashirikisha vilabu zaidi ya 15, wakati nasikia Ligi Daraja la Nne wilaya ikiwa na timu chache, hili tutakutana kuona iliyopo ili tuone kwa namna moja tunavyoweza kuifanyiakazi,” amesema Mkenge.