January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tupige kura kuwapata viongozi wakutuletea maendeleo

Na Fredy Paschal, TimesMajira Online

WENGI hutoa tafsiri,maoni ama mtizamo yao juu ya kauli za viongozi mbalimbali walio maarufu duniani hususani katika nchi yetu pendwa ya Tanzania kwa kadiri ya ufahamu,mawazo, pamoja na mitazamo yao kama yanavyowaelekeza.

Kila mmoja ameonekana kuvutia kwake katika kutafsiri hotuba na mawazo ya viongozi wao kwa kadiri ya mitazamo yao kiitikadi na mara nyingine hutafsiriwa kwa njia potofu ama jenzi kutokana na nia ya kuvutia wanachama wa itikadi husika ziwe za kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni,michezo nk

Miongoni mwa hotuba ambazo hutolewa tafsiri tofauti tofauti zenye usahihi ama kutafsiriwa kwa namna tofauti kulingana na mitazamo na malengo ya kisiasa kwa lengo la kuongeza umaarufu wa kisiasa wa vyama na makundi ya watafsiri ni pamoja na zile za Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ambaye juma lililopita Oktoba 14, 2020 tuliadhimisha miaka 21 tangu alipofariki Oktoba 14,1999 katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas Jijini London huko Uingereza ambapo alikuwa akipatiwa matibabu.

Katika moja ya maelfu ya hotuba zake ambayo leo nimependa kuifafanua kwa mtazamo wangu ambapo naamini huo ndio ulikuwa msingi wa maneno yake katika hotuba hiyo aliyolenga kutufikishia Watanzania,Mwalimu alisema “Ni vizuri sasa wakasikiliza wananchi wanasemaje,msidhani kwamba mnaweza kupata ushindi mkipuuza maoni ya wananchi’’ mwisho wa kunukuu.

Kwa mujibu wa hotuba hiyo ya Mwalimu Nyerere,yatupasa kujiuliza na kutambua je ni yapi maoni ya wananchi?

Kimsingi maoni ya wananchi yapo katika maeneo mengi ya kimahitaji na kimaumbile yanayowakabili wananchi,tuanze kwanza na kuangalia mahitaji muhimu ya kila mwananchi(mwanadamu) ambayo wanazuoni wameyaainisha kuwa binadamu wote ni sawa na wanahitaji mahitaji ya msingi ambayo ni chakula, malazi na mavazi

Kila mwanadamu anahitaji chakula,kazi ya chakula katika mwili wa binadamu na viumbe hai wengine ni kwamba chakula kina virutubisho ambavyo vinawezesha mwili kupata nguvu kwa ajili ya kuweza kufanyakazi mbalimbali za kimaisha, huwezesha mwili kukua, na pia kuwesha masuala mengine kama vile upumuaji, kuwezesha kufanya kazi kwa mfumo wa chakula,kurekebisha joto la mwili na kuimarisha kinga za mwili.

Upande wa malazi ambayo kwa lugha nyingine tunaweza kuita makazi ni muhimu kwa mwanadamu katika maeneo mbalimbali kama vile kutupa kivuli wakati wa jua,kukinga wakati wa mvua na upepo na pia kutupa uvuguvugu,kulala na kujipumzisha,kutuweka salama dhidi ya wanyama nk.

Mbali ya hayo,maoni ya watu yaliendelea kutolewa falsafa na viongozi mbalimbali akiwepo Mwalimu Nyerere ambapo alisisitiza kuwa alama ya mandeleo ya watu yapo katika uwepo wa vitu vinne yani watu,ardhi,siasa safi na uongozi bora,hapo tunaona kuwa maoni ya wananchi,ndio maoni ya watu ambayo ndio ishara ya kwanza ya maendeleo.

Basi baada ya watu na tuangalia ardhi ambayo ni nyenzo muhimu sana katika maendeleo ya mahali popote na ya watu wowote ,bila ardhi hakuna maendeleo,katika ardhi ndipo tunapopata makaa,maji na mafuta ambavyo hutumika katika uzalishaji wa nishati na nguvu mbalimbali za uendeshaji wa mitambo,juu ya ardhi ndipo viwanda vikubwa na vidogo hujengwa kwa ajili ya uzalishaji mali na kuzalisha ajira.

Ardhi ni muhimu kwa wanadamu maana utajiri wote wa nchi upo ndani ya ardhi na juu ya uso wa ardhi mfano madini,na maliasili mbalimbali,ardhi hutumika pia kwa kilimo cha mazao ya biashara na chakula,ardhi huhifadhi maji ya mito,bahari,maziwa na mabwawa ambapo maji hayo hutumika katika uvuvi,umwagiliaji na uzalishaji wa nguvu za umeme nk.

Katika siasa safi ndipo penye asili ya kupokea maoni ya wananchi na kuyafanyia kazi,nchi yetu inafuata mfumo wa siaisa ya vyama vingi tangu mwaka 1992 ambapo wananchi walipata fursa ya kutoa maoni juu ya mfumo wa kufuata ama vyama vingi au wa chama kimoja.

Serikali ya Awamu ya Pili chini ya Rais Ally Hassan Mwinyi iliunda tume iliyoongozwa na Jaji Francis Nyalali kwa ajili ya kukusanya maoni juu ya uamuzi huo ambapo mwishoni mfumo wa vyama vingi ulipata kibali na kuasisiwa rasmi,ni mfumo ambao hupokea mawazo ya wengi na kuyafanyia kazi kwa mujibu wa matakwa ya wananchi.

Kwa upande wa uongozi bora ni pale ambapo kiongozi anakuwa mwema mwadilifu,mwenye kujiamini,anayejituma,muungwana,mwenye mawasiliano mazuri na wengine,mwenye kukasimisha madaraka,mwezeshaji na mwenye kulinda mila,utamaduni na desturi za nchi yake sambamba na kuilinda katiba ya nchi.

Kwa maelezo hayo tunaona kuwa asili ya maoni ya watu ambayo vyama vya siasa na uongozi kwa ujumla wanaelekezwa wayasikilize yameegemea katika falsafa zilizotajwa awali ambazo wanazuoni wameyataja mahitaji muhimu ya wanadamu ambayo ni chakula,mavazi na malazi,lakini maoni yanaweza kutoka pia katika vitu vinne ambavyo ni watu,ardhi,siasa safi na uongozi bora.

Wananchi watahitaji ardhi kwa ajili ya kujipatia mahitaji mbalimbali kama vile kilimo kwa mazao ya chakula na biashara,kwa ujenzi wa nyumba za makazi bora,ardhi kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vidogodogo na vikubwa ambavyo vitazalisha bidhaa mbalimbali za kilimo ikiwepo nguo kwa ajili ya kukidhi hitaji muhimu la mavazi,ardhi kwa ajili ya ujenzi wa shule za kuelimisha wananchi elimu ambayo wataitumia katika uendeshaji wa viwanda,kuwapa ujuzi madaktari,wahandisi nk

Wananchi watatoa maoni yatakayoimarisha uwepo wao(watu)ambao kihalisia ndio nyenzo za uzalishaji na kuwa wanategemeana katika uendeshaji wa shughuli mbalimbali katika uso wa ardhi ikiwepo viwandani,mashambani,uvuvi, utawala,uhandisi na shughuli nyingine za kiuchumi.

Ni muhimu kwa watu kujikita katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali kama moja ya kauli mbiu za Serikali yetu ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) inayosema “Hapa Kazi Tu”,ni katika uzalishaji wa mashamba tunapojipatia pamba inayotumika kutengenezea nguo ambayo ina matumizi mbalimbali.

Kiujumla maoni mengi ya watu yamelenga katika maendeleo yao ambapo mengi ya maoni hayo yamelenga katika huduma bora za afya,Miundombinu bora ya barabara, huduma bora za elimu, nishati ya uhakika ya umeme, usafiri wa anga,majini,nchi kavu na reli na vi, uwepo wa siasa safi na uongozi bor.

Maoni ya wananchi huelekezwa kwenye vyama vya siasa ambavyo vinakuwa na jukumu la kuyatekeleza yale yote ambayo ni mahitaji ya msingi ya wananchi,hili la utekelezaji kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linahusu chama ambacho kimeshinda uchaguzi mkuu hivyo mtekelezaji wa majukumu yaliyotokana na maoni ya wananchi kwa kipindi kilichopita cha miaka mitano ni CCM ambacho kilishinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na kutekeleza majukumu hayo toka Mwaka 2015-2020.

Tutakuwa mashahidi kwa namna alivyotekeleza kwa zaidi ya asilimia 100 ya yale yote aliyoahidi kupitia ilani ya CCM na alifanya hata ziada ya yale yaliyokuwepo katika ilani kwa ajili ya kutimiza mahitaji ya wananchi wake wa Tanzania na pia kuna machache sana ambayo yameanzishwa na yanaendelea kutimizwa kwa kasi sana.

Yote hayo pamoja na ukusaji mzuri wa kodi,urekebishwaji wa mikataba ya madini na kudhibiti utoroshwaji wa madini hayo umewezesha kuinua pato la taifa kiasi cha kuitoa Tanzania katika nchi masikini na kuiingiza katika nchi zenye uchumi wa kati.

Jumatano Oktoba 28 Watanzania wanakwenda kuchagua madiwani,wabunge,wajumbe wa baraza la wawakilishi na Marais wa Zanzibar na wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao wataongoza kwa kipindi cha miaka mitano jambo ambalo kutafakari kabla ya kufanya maamuzi.

Vyama vya siasa hufanya kampeni takribani miezi miwili nchi nzima kwa lengo la kuelezea ilani yao yani kile kilichoandaliwa na vyama hivyo kwa ajili ya kutatua kero za wananchi na wananchi nao wanapata fursa ya kusikiliza kwa kina sera hizo na mwishoni wanapata fursa ya kuchagua ‘viongozi bora’ kutoka katika vyama vyenye ‘Siasa safi’ ambao wanaweza na wanawaamini kuwa watatekeleza kwa hakika na pasi na shaka yale yote waliyoyaahidi kwa kipindi cha miaka mitano toka siku atakayoapishwa kwa wadhifa wake.

Kesho yaani Jumatano Oktoba 28 ndio siku ya Uchaguzi Mkuu kama ndio wasaa wenye umuhimu wa kipekee zaidi kwa wananchi kutoa maoni yao kwa njia ya kura ambayo ndio itakuwa mwamuzi wa mwisho wa kuamua nani atakuwa mbeba maoni atakaepewa dhamana na mpiga kura,mbemba maoni ni yule atakaechaguliwa kuwa diwani,mbunge ama Rais,mpiga kura atakuwa amejiridhisha kuwa ni kiongozi.

Lakini pia wanapaswa kujiridhisha kuwa je viongozi hao wanatokana na vyama vyenye siasa safi na chenye kuakisi uwepo wa uongozi bora ndani ya vyama vyao? Waungwana wanasema kosea vitu vyote lakini usikosee kuchagua,ni wakati watoa maoni wanatakiwa kufanya uamuzi wao wa kuchagua chama kitakachobeba maoni yao kupitia wawakilishi wanaowachagua ambao ni diwani,mbunge na Rais kwa upande wa Jamhuri ya Muungano na wawakilishi na Rais wa Zanzibar kwa upande wa Tanzania Visiwani.

Tunahakikisha tunachagua viongozi wanaohitajika na wananchi kwa uzalendo wao,uwajibikaji wao,upigaji vita wao dhidi ya rushwa,uadilifu wao na pia uwezo wa kupambana na majanga ya dharura bila kutegemea maelekezo yatakayoondoa utu,uzalendo,mila na utamaduni wetu na kupinga tamaduni chafu zisizolingana na za nchi yetu na vilevile kulinda na kusimamia amani ya nchi yetu,kulinda na kutetea katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na awe kiongozi atakaelinda na kusimamia rasilimali za nchi yetu.

Kuna vyama takribani 15 ambavyo vinashiriki uchaguzi mkuu huu hususani kwenye nafasi ya urais ambavyo miongoni mwao kupitia ilani ya uchaguzi yao kitaunda serikali na ilani hiyo kutumika kama mkataba wa kuongoza iwapo kitashina uchaguzi mkuu huu.

Tukumbuke ilani ndio maoni ya wananchi,iwapo chama kitachaguliwa basi hakuna lawama katika utekelezaji wa ilani ya chama hicho bali ni majuto utakapochagua kwa mihemko kwani ni maoni yako yaliyokipatia ushindi chama husika,ni furaha utakapochagua chama ambacho kitatekeleza maoni yako bila wasiwasi,kwa mujibu wa Mwl Nyerere amesisitiza kuwa maoni hayo ambayo yamemwezesha kiongozi fulani na chama chake kushinda yasipuuzwe,hivyo tusichague hovyo kwa kufata ahadi hewa ama kwa kufata mkumbo.

Baada ya vyama vya siasa,Tume ya uchaguzi ya Taifa NEC ndio chombo pekee kilichopewa mamlaka ya kuratibu Uchaguzi Mkuu na hatimae kutangaza matokeo ya uchaguzi huo hususani matokeo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo kanuni zinakataza mtu,taasisi ama chombo chochote kutangaza matokeo ya uchaguzi kabla ya tume ya uchaguzi haijafanya hivyo na kila mmoja yampasa kuzingatia suala hilo.

Katika uchaguzi huu nawakumbusha kuwa inatupasa kusikiliza kwa makini ilani za vyama ili tusijejutia kuchagua sera ambazo zitalinda utu wetu,rasilimali zetu,amani yetu,heshima yetu,maendeleo yetu na kuwaachia urithi bora watoto wetu.

Sera ya CCM kwa sasa ni kuboresha zaidi yale yaliyofanyika katika miaka mitano iliyopita,kushusha zaidi bei ya umeme baada ya uzalishaji kukua,kuboresha zaidi sekta ya afya,kuimarisha usafiri wa anga kwa kuongeza ndege na viwanja zaidi,kuimarisha usafiri wa majini,usafiri wa reli, ,miundombinu ya barabara za kawaida na za juu yani flyovers,sekta ya elimu,mikopo kwa wajasiriamali kupitia vitambulisho vyao,kuboresha upatikanaji wa maji nchini ,kuimarisha zaidi sekta ya madini na sekta ya utalii nchini nk.

Hakika uwezo mkubwa wa kutatua matatizo ya wananchi,matumizi mazuri ya rasilimali za nchi,ukusanyaji mzuri na matumizi mazuri ya kodi za wananchi na uadilifu wa Rais Magufuli,utekelezaji wa kauli yake ya Tanzania ya viwanda katika kujimudu kuzalisha bidhaa za ndani na za kuuza nje,kupinga rushwa,uimarishaji wa nidhamu ya utumishi wa umma hii imekuwa ni mtaji mkubwa kwa mgombea uraisi kupitia Chama cha Mapinduzi ambazo zinamwelekeo wa kumpa ushindi wa kishindo.

Napenda kuchukua fursa hii kuwaomba wananchi wote waliojiandikisha kama wapiga kura,kujitokeza kwa wingi siku kesho kuitumia vizuri haki yao ya msingi ya kupiga kura ya kuchagua.