Na Penina Malundo, TimesMajira Online
MAKAMU Mwenyekiti wa CHADEMA (Bara), Tundu Lissu na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha ACT- Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, waamelaani tukio la kuvamiwa na kuumizwa Kiongozi wa Upinzani Bungeni (KUB) na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, wakati akipanda ngazi kuingia nyumbani kwake Area D.
Viongozi hao walitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti jana, ambapo Maalim Seif alikuwa akizungumza na wanahabari akiwa jijini Dar es Salaa na Lissu alikuwa akitumia mitandao ya kijamii akizungumza kitokea Ubelgiji.
Maalim Seif amesema kitendo hicho alichofanyiwa Mbowe ni kitendo kibaya na cha kinyama kinachostahili kulaani.
Amesema ameshangazwa na baadhi ya viongozi ambao wanafurahia namna kiongozi huyo wa upinzani alivyoumia na kusema kuwa huo sio ubinadamu.
“Kitendo hiki ni kibaya alichofanyiwa Mwenyekiti Mbowe na mbaya zaidi baadhi ya viongozi wanafurahia tukio hili na kufanya kejeli, najiuliza ni kweli Tanzania tumepoteza ubinadamu kiasi hiki?”Alihoji Maalim Seif na kuongeza;
“Mwenzako anafikwa na maafa badala ya kumuhurumia na kumuombea wewe unamkejeli.” Kwa upande wake, Lissu pamoja na mambo mengine alikosoa hoja inayotolewa kuwa Mbowe aliumia kwa sababu alikuwa amelewa. Lissu amesema katika sheria za Tanzania hakuna inapoelezwa kwamba kunywa pombe na kulewa ni kosa la jinai.
Kuhusu hoja kwamba Mbowe, alikuwa wapi hadi usiku wa maneno, Lissu amesema Tanzania hakuna tangazo lolote la hali ya hatari linalomzuia mtu kutembea usiku wa manane.
Amesema kauli hizo zinaweza kuwa ni maandalizi ya kuwafanya Polisi kutofanya uchunguzi wa kutosha kuhusiana na tukio hilo. Lissu amesema kitendo hicho cha kushambuliwa, Mbowe ni cha kulaaniwa na kukemewa na kila mwananchi wa Tanzania ili wanaovifanya vitendo hivyo wasipate mahali popote pa kujificha. amesema wale wote wanaochukizwa na vitendo hivyo kuvipigia kelele.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa