Na Penina Malundo,TimesMajira.Online
MAWAKILI wanawake nchini, wametakiwa kuhakikisha wanatumia uzoefu wao katika kushiriki kesi zinazohusiana maslahi ya umma za kutetea haki za binadamu.
Wito huo umetolewa leo na Jaji wa Mahakama Kuu Tanzania, Lilian Mongela wakati wa ufunguzi wa mjadala wa kuwajengea uwezo mawakili wanawake katika kusimamia kesi zinazohusu maslahi ya umma, uliofanyika kupitia njia ya mtandao ambapo alisema kuna huhitaji mkubwa wa mawakili wanawake, kushiriki kesi za uteuzi wa haki za binadamu.
Amesema ushiriki wa mawakili wanawake katika kesi za maslahi ya umma, bado ni mdogo hivyo ni vyema kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi ili kusaidia wananchi kupata haki zao.
Jaji Lilian amesema, takribani mawakili wanawake waliosajiliwa Tanzania wanafikia 3,055 lakini wanaoshiriki katika kesi zinazohusu maslahi ya umma ni wachache na mchango wao ni mdogo, hivyo wanapaswa kushiriki katika kesi hizo kwa kuwa wanaweza kama wanavyofanya vizuri katima kesi nyingi.
Kwa upande wake, Wakili Najutwa Sengondo amesema kinachowakwamisha kutetea kesi zinazohusu utetezi wa haki za binadamu ni changamoto mbalimbali wanazokutana nazo.
Ametaja changamoto hizo kuwa ni uhaba wa rasilimali fedha na mafunzo kuhusu usimamiaji kesi, zinazohusu maslahi ya umma.
Naye Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa amesema bado nchi inakabiliwa na changamoto ya uwepo wa idadi ndogo ya mawakili, wanaotetea kesi zinazohusiana na haki za binadamu.
Amesema mawakili wanawake na wanaume waliosajiliwa hapa nchini, idadi yao inakaribia kuwa nusu kwa nusu lakini waliomstari wa mbele kutetea mashtaka ya umma ni wanaume huku idadi ya wanawake ikiwa ndogo.
“Wakati wa kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, tunataka kukaa na mawakili wanawake hawa ili tuwajengee uwezo na hatimaye idadi ya mawakili wanawake katika mashauri yanayohusu maslahi ya umma iongezeke,” amesema.
Mjadala huo uliratibiwa na Mtandao THRDC, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TWLA).
More Stories
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito