May 21, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tume yasisitiza haitaongeza siku uboreshaji Daftari awamu ya pili

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi, imesema zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya pili mzunguko wa pili ulioanza Mei 16 hadi 22, 2025 ukikamilika Tume haitaongeza siku za ziada.

Tume hiyo imesema, wananchi wenye sifa wajitokeze katika siku mbili zilizobaki kujiandikisha au kuboresha taarifa zao na kuwaondoa wale wasio na sifa kuwepo kwenye Daftari hilo.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Tume, Jaji wa Rufani, Jacobs Mwambegele wakati wa ziara ya kukagua mwendendo wa zoezi hilo la Uboreshaji na uwekaji wazi Daftari la Awali katika Halmashauri za Wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga, yenye majimbo ya Uchaguzi ya Lushoto na Mlalo.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele akimkabidhi Kadi mpya ya Mpiga Kura mkazi wa Kata ya Ubiri Wilayani Lushoto ambaye alifika Ofisi ya Kata hiyo kuboresha taarifa zake leo Mei 20,2025. Jaji Mwambegele yupo Mkoani Tanga kuangalia mwenendo wa zoezi la ubpreshaji awamu ya pili. (Picha na INEC)

Kwa upande wake Afisa Mwandikishaji Jimbo la Lushoto na Mlalo, Dkt. Ikupa Harrison Mwasyoge ameeleza namna uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na Uwekaji Wazi wa Daftari la Awali unavyoendelea.

Zoezi hilo linakwenda sambamba na uwekaji wazi wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mikoa 11 ya Tanzania Bara na Mitano ya Tanzania Zanzibar.

Mikoa hiyo ni Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Pwani, Singida, Dodoma, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja.

Kusini Unguja, Kaskazini Pemba na Kusini Pemba ambapo zoezi hilo linafanyika kwa siku saba na lilianza Mei 16 hadi 22, 2025.

Katika zoezi hilo vituo vinafunguliwa Saa 2:00 asubuhi na kufungwa Saa 12:00 jioni kila siku kwa siku saba na kauli mbiu ya zoezi ni “Kujiandikisha kuwa mpiga kura ni msingi wa uchaguzi bora’.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele akizungumza na wakazi wa Kata ya Ubiri Wilayani Lushoto ambao walijitokeza kuhakiki taarifa zao katika Daftari la awali la Wapiga Kura lililobandikwa katika kituo cha Ofisi ya Kata hiyo  leo Mei 20,2025. Jaji Mwambegele yupo Mkoani Tanga kuangalia mwenendo wa zoezi la ubpreshaji awamu ya pili. (Picha na INEC).