Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Mzunguko wa tatu wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utaanza Agosti 21 hadi 27 mwaka huu,ukijumuisha mikoa ya Mwanza na Shinyanga huku wananchi wakihimizwa kuzingatia sheria kwa kujiandikisha mara moja tu.
Pia Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) mkoani Mwanza inatarajia kuandikisha wapigakura wapya 190,131 ikiwa ni ongezeko la asilimia 10.3 ya wapiga kura zaidi ya milioni 1.8(1,845,816),waliopo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na matarajio yake baada ya zoezi hilo Mkoa huo utakuwa na wapiga kura milioni 2,035,947.
Akizungumza Agosti 9,2024 katika ufunguzi wa mkutano waTume na wadau wa Uchaguzi mkoani hapa Mwenyekiti wa INEC Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jacobs Mwambegele amesema vituo vya kuajiandikisha vitafunguliwa saa 2 asubuhi na kufungwa saa 12 jioni kwa siku hizo saba.
Jaji Mwambegele ametoa rai kwa washiriki wa mkutano huo wakiwemo wanasiasa, viongozi wa dini,kuwaelimisha wananchi wanao kwenda vituoni kwa ajili ya kuomba kuandikishwa kuwa wapiga kura mara moja tu ili kuepuka uvunjaji wa sheria.
“Kujiandikisha kuwa mpiga kura zaidi ya mara moja ni kosa kisheria kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 114(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais,Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024,kifungu hicho kinasema kuwa mtu yoyote atakayeomba kuandikishwa zaidi ya mara moja atakuwa ametenda kosa kisheria na akitiwa hatiani adhabu yake ni faini isiyopungua kiasi cha 100,000 na isiyozidi 300,000 au kutumika kifungo kwa kipindi kisichopungua miezi sita na kisichozidi miaka miwili au vyote kwa pamoja,”amesisitiza Jaji Mwambegele.
Ambapo amesema watu kujiandikisha zaidi ya mara moja kwenye Daftari hilo siyo mara ya kwanza kutokea,mwaka 2015 watu zaidi ya 52000 walibainika kujiandikisha mara mbili.
Huku mwaka 2020 walibainika watu zaidi ya 42,000 walijiandikisha kwenye Daftari hilo zaidi ya mara moja na wote walichukuliwa hatua.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC Ramadhani Kailima, ameeleza kuwa idadi ya vituo vya kuandikisha wapiga kura kwa mwaka 2024 nchini vitatumika 40,126 kati ya hivyo 39,709 vipi Tanzania Bara na 417 vipo Zanzibar ni ongezeko la vituo 2,312 ikilinganishwa na vituo 37,814 vilivyotumika 2019/2020.
“Kwa Mkoa wa Mwanza vitatumika 2,251 kwenye uboreshaji kwa mwaka huu ikiwa ni ongezeko la vituo 73 katika 2,178 vilivyotumika kwenye uboreshaji mwaka 2019/2020,”.
Pia ameeleza kuwa kwa kuzingatia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 wapiga kura zaidi ya milioni 5.5(5,586,433), wapya wanatarajiwa kuandikishwa nchini sawa na asilimia 18.7 ya wapiga kura zaidi ya milioni 29.7(29,754,699), waliopo kwenye Daftari baada ya uboreshaji uliofanyika mwaka 2019/2020.
“Idadi ya wapiga kura zaidi ya milioni 4(4,369,531 inatarajiwa wataboresha taarifa zao na wapiga kura 594,494 wa wanatarajiwa wataondolewa kwenye Daftari hilo kwa kukosa sifa za kuendelea kuwepo,baada ya uboreshaji inatarajiwa Daftari litakuwa na jumla ya wapiga kura zaidi ya milioni 34(34,746,638),”.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Sauti ya Wanawake Ukerewe Sophia Donald, ameeleza kuwa kupitia majukwaa yao watahamasisha wanawake wajitokeze kushiriki katika kuboresha taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuelekea kwenye uchaguzi waweze kupiga kura na kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali.
“Kwa jiografia ya Ukerewe kwa siku saba hizo haziwezi kutosheleza,visiwa vipo zaidi ya 30,vinavyokaliwa na watu ni zaidi ya 15, kutoka Kisiwa kimoja kwenda kingine unaweza kutumia saa takribani 7 na hupatikanaji wa usafiri inaweza ikawa ni changamoto namna ya kuwapata wanawake ambao ni wachuhuzi wa samaki,”.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema(BAVICHA) Mkoa wa Mwanza Abbas Mayala, ameeleza kuwa zoezi la kujiandikisha wananchi wasione kuwa ni usumbufu kwani ni haki yao ya msingi na kama chama wamejipanga kuwahamasisha ili waweze kujitokezee kwa wingi hadi maeneo ya vijijini.
“Kwa upande wa CHADEMA hatujaridhika na siku hizo za zoezi la uandikishaji,hivyo Tume iangalie namna ya kuongeza siku badala ya wiki moja iongeze muda angalau ziwe wiki mbili,”.
More Stories
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto