December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tume ya Tehama yaelekeza nguvu usalama wa mtandao

-Yasema una siri kubwa uchumi wa kidigiti

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

IMEELEZWA kuwa katika ulimwengu wa sasa ambapo mageuzi ya kidijitali ni nguzo kuu ya kuwezesha uchumi wa kidijitali, endapo suala la usalama wa mitandao halitapewa uzito unaoendana na kasi ya maendeleo ya TEHAMA litakuwa kizuizi cha ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama, Dk Nkundwe Mwasaga wakati akifungua Jukwaa la Tatu la Usalama wa Mitandao linalofanyika Arusha leo (jana).

Alisema katika hotuba yake kuwa, Mageuzi haya ya kidijitali yanayojengwa na msingi wa dhana kuu mbili za kutumia teknolojia za kidijitali katika shughuli ili kuongeza ufanisi, na mabadiliko ya binadamu ambao ni watumiaji wa bidhaa zitokanazo na TEHAMA, dhana hizi mbili haziwezi kufanikiwa endapo mifumo ya kidijitali itatishia usalama wa nchi na hivyo kuwa kikwazo kwa ukuaji Uchumi.

Pia kutokuwepo kwa matumizi sahihi ya mifumo ya kidijitali kunaweza kusababisha kutwezwa kwa utamaduni wa taifa na utu kwa kuruhusu taarifa za siri za Serikali, Kampuni na hata zile za mtu binafsi kupatikana kwa utaratibu usio.

Alisema hali hiyo ya taarifa kutumiwa na watu wasiokuwa na dhamana ya kutumia taarifa husika, kunaweza pasi shaka kuvuruga malengo ya mageuzi ya kidijitali.
Alisema kutokana na kutambua umuhimu wa kuhakikisha kuwa Tanzania iko katika nafasi salama katika ulimwengu wa kidijitali, Tume imeitisha kikao hicho cha siku mbili kuangalia matumizi salama ya mitandao ya kompyuta na huduma za kielektroniki kwa ujumla.

Akisisitiza zaidi katika mkutano huo wenye kaulimbiu ya “Kutengeneza Dunia ya Mtandao iliyojumuishi na Shirikishi”, Mkurugenzi mkuu huyo alisema mkutano huo utajadili na kutafakari masuala ya umadhubuti wa sekta za Uchumi katika ulimwengu wa kidijitali, kuibua na kutumia teknolojia ibukizi za kidijitali zilizo salama, uendelevu na ujumuishi katika huduma za kidijitali, kuongeza chachu ya ukuaji Uchumi na kuondoa vishawishi vinavyochochea vihatarishi katika ulimwengu wa kidijitali.

“Ninaamini kupitia jukwaa hili mtabadilishana mawazo, uzoefu na kufanya tathmini ya masuala husika pamoja na yale ya jumla ya hali ya usalama wa miundombinu, mifumo ya TEHAMA na huduma zitokanazo na mitandao ya kilektroniki hapa nchini,” alisema.

Alisema pamoja na uwekezaji mkubwa unaofanywa katika miundombinu ya mawasiliano, ujenzi ya mifumo ya TEHAMA, kuendeleza wataalamu na wabunifu wa TEHAMA, Sera na Sheria zimeandaliwa kuchagiza maendeleo ya kidijitali hususan kuhakikisha uwepo wa matumizi salama ya huduma zitokanazo na maendeleo ya kidijitali.

Serikali kwa sasa inaendelea kuhuisha Sera ya TEHAMA ya mwaka 2016 ili iweze kuchagiza ukuaji wa Uchumi wa kidijitali kwa kasi zaidi.

Aidha, mwaka 2022 Bunge limepitisha Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi na kupitia sheria hiyo tayari tumeanzisha Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.

“Ninaamini kupitia jukwaa hili tutapokea mawazo na maoni mbalimbali ya maeneo ya kisera na kisheria yanayohitaji kuboreshwa zaidi ili kuendelea kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa katika nafasi salama ya ulimwengu wa kidijitali,” alisema.