January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tume ya Haki za Binadamu yaridhishwa vita ya Corona

Na Mwandishi Wetu

TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imeunga mkono juhudi
zinazofanywa na Serikali dhidi ya mapambano ya mlipuko wa maradhi
yanayosababishwa na virusi vya Corona.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari THBUB Dar es Salaam jana na
kusainiwa na Mwenyekiti wa Tume Jaji Mstaafu, Mathew Mwaimu imeeleza
kuwa hatua hizo ni  katika kulinda haki ya afya ya wananchi wake pia
ni hatua muhimu katika kupunguza maambukizi ya maradhi hayo kwa jamii.

“Kipekee kabisa Tume inaipongeza Wizara ya Afya na watendaji wake
ikiwemo madaktari, wauguzi na wahudumu wengine kwa kazi kubwa
wanayoifanya ya kuhamasisha, kuelimisha na kutoa huduma stahiki kwa
wananchi ambao tayari wamepata maambukizi ya maradhi hayo,” ameeleza
taarifa hiyo na kuongeza;

“Tume inatumia fursa hii pia kuwapongeza jumuiya za AZAKI na
wafanyabiashara waliojitokeza  kuunga mkono kwa hali na mali jitihada
za Serikali katika kupambana na maradhi hayo.”

Aidha, Tume iliiomba jamii kutofanya  mzaha na jambo hilo, kwani janga
hilo ni kubwa hivyo ni muhimu kuunga mkono jitihada za Serikali kwa
kufuata maelekezo sahihi yanayotolewa ikiwemo wale wote washukiwa wa
maambukizi na wenye maambukizi kukaa Karantini kwa muda uliopangwa ili
kuzuia maambukizi ya ndani yasiongezeke.

Tume imetoa ushauri kwa Serikali na jamii iendelee kuzingatia
maelekezo ya kujikinga yanayotolewa mara kwa mara na Serikali kupitia
Wizara ya Afya.

Imetoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kujitokeza kuunga mkono
jitihada za Serikali katika mapambano dhidi ya maradhi hayo na
Serikali iendelee kuchukua tahadhari hususani katika mipaka yetu ili
kuzuia kuingia kwa maambukizi mapya kutoka nje ya nchi.

“Tume inaiomba Serikali kuliangalia kipekee kundi la watu wenye
Ulemavu kwani wao wanahitaji msaada zaidi kukabiliana na mlipuko wa
maradhi ya Virusi vya Corona, ikiwemo kuwapatia taarifa sahihi kupitia
njia sahihi, kwa mfano viziwi wapatiwe taarifa kwa lugha ya alama na
watu wasioona waandaliwe taarifa zao kupitia machapisho mbalimbali ya
nukta nundu, kuwapa huduma bora za afya na kuwalinda dhidi ya
unyanyapaa,” imeeleza taarifa hiyo.