June 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

‎Tumaini Larejea Mbulu— Serikali Yapongezwa kwa Mradi wa Visima, Yaweka Mikakati ya Kitaifa kwa Programu ya Visima 900



‎Na Joyce Kasiki,Timesmajira  online, Dodoma

‎WAKAZI  wa Jimbo la Mbulu Mjini wameonyesha shukrani zao kwa Serikali kufuatia uchimbaji wa visima vitano vya maji safi, ambavyo tayari baadhi vimeanza kutoa huduma kwa wananchi.

‎ Hii ni sehemu ya hatua muhimu katika kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama, iliyodumu kwa muda mrefu katika eneo hilo.

‎Mbunge wa Mbulu Mjini Zacharia Isaay  kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiuliza swali , alitaka kufahamu mpango wa jumla wa Serikali katika kuendeleza visima hivyo kama sehemu ya programu kubwa ya kitaifa ya uchimbaji wa visima 900.

‎Akijibu swali Hilo,Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Mathew Kundo  amesema kuwa uchimbaji huo ulikuwa sehemu ya mchakato wa tathmini ya wingi wa maji kabla ya kuanza usanifu wa miradi mikubwa ya usambazaji.

‎“Zoezi lililofanyika lilikuwa ni kuchimba na kuangalia wingi wa maji. Baada ya hapo, tunafanya usanifu ili kuhakikisha tunatengeneza mtandao wa wananchi kupata huduma ya maji,” alifafanua Naibu Waziri.

‎Aidha, alieleza kuwa katika maeneo ambako maji yanapatikana lakini si kwa kiwango cha kutosha kuwahudumia wananchi wengi, Serikali huweka mfumo wa ‘point source’ katika eneo hilo hilo la kisima kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanaanza kunufaika na maji mara moja, huku usanifu mkubwa ukiendelea kutafutiwa fedha.

‎ “Nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga, na kwa bajeti ya mwaka ujao wa fedha changamoto hizi zinaenda kutatuliwa,” alisisitiza Naibu Waziri.

‎Kwa mujibu wa Wizara ya Maji, program ya visima 900 ni mkakati wa kitaifa unaolenga kupunguza utegemezi wa vyanzo vya maji vya mbali na kuongeza upatikanaji wa maji katika maeneo ya pembezoni na yenye changamoto za miundombinu ya usambazaji.