November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tulichonacho ni almasi tusidanganyike na walioshindwa kuungana

JAMHURI ya Muungano wa Tanzania ni Jamhuri ambayo imefanikiwa kuulinda, kuulea,na kudumisha Muungano kwa miongo mitano na nusu sasa ambapo unarithishwa kwa vizazi kwa kuwa waasisi wengi wa Muungano wametangulia mbele ya haki na kuufanya kuwa mfano wa pekee katika sayari ya dunia.

Unapoitaja Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huna budi kuwashukuru kwa dhati kabisa Waasisi wa Muungano ambao ni Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Shekhe Abeid Amani Karume, Watanzania wanawaombea wapumzike kwa amani na hakika wataendelea kuenziwa na kuombewa siku zote za maisha yao.

Kuna faida nyingi kwa kuwepo Muungano hapa Tanzania ikilinganishwa na changamoto za hapa na pale ambazo zinatatuliwa kadri siku zinavyosonga mbele na zipo sababu nyingi zinazowafanya Watanzania kuwa wamoja, kushikamana na kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar:

UNDUGU WA DAMU

Ipo tofauti kubwa sana kati ya Muungano wa Tanzania na nchi nyingine walioungana ambao kiasili hawana mahusiano na udugu wa damu kama ilivyo kwa Tanzania Bara na Visiwani mfano wakazi wengi wa Mji wa Tanga wana ndugu wa damu na jamaa zao walioko Unguja au Pemba, hivyo kwao mipaka na Jiografia sio sababu ya kuwatenganisha.

Wamekuwa na ushirikiano tangu hapo awali Muungano kwao umekuja kama tu kuhalalisha udugu wao kutowekewa mipaka na utaratibu wa ushirikiano kitu ambacho kimepandikizwa na wakoloni walioweka mipaka.

Aidha, kutokana na tabia za kiafrika za kuhama kutoka eneo moja kwenda lingine wananchi wenye asili ya Bara wamehamia Unguja tangu enzi hizo na kuanzisha familia na kuacha baadhi ya ndugu zao Bara.

Pia, kwa wazaliwa wa Unguja wengi wamehamia Bara na kuweka makazi yao ikiwemo na vitega uchumi vingi takriban nchi nzima. Misingi hii imeweka mizizi ambayo unapomwambia kihalisia mwananchi wewe wa Bara huyu wa visiwani na kumuita yeyote yule mhamiaji anakushangaa na hii inahitaji elimu ya ziada kwa mwananchi wa kawaida.

MAHUSIANO YA BIASHARA TANGU ENZI ZA WAHENGA

Biashara za aina mbalimbali zimefanyika tangu karne ya 14 ambapo wageni mbalimbali kutoka Ureno, India, Uchina, Uarabuni na Europa walifika nchini na kuwa na mahusiano na wazazi waliotangulia na kuweka makazi maeneo mbalimbali kama kule Kilwa Kisiwani ambapo Mfalme wa Ughaibuni wa Saudia aliweka makazi na kuacha kizazi chake ambacho mpaka leo kimebakia Kilwa Kisiwani na majengo yanayovutia katika utalii wa majengo ya kale ya Kilwa Kisiwani kama vile Msikiti wa Kale, na tabia, desturi, mila na taratibu za kiarabu ambazo zimesalia.

LUGHA YA KISWAHILI

Kutokana na biashara hizo zilizofanyika ingekuwa vigumu sana kusikilizana kwa kuwa kila mmoja alikuwa na lugha yake. Lakini uundwaji wa lugha ya Kiswahili kutokana na mashirikiano na mchanganyiko wa watu kutoka mataifa mbalimbali waliweza kuelewana na kusikilizana na kujenga uhusiano ambao kimsingi sio rahisi mtu mwingine yeyote kuutenganisha.

Hii ndio asili ya Mtanzania kuwa mkarimu na mtu wa kukaribisha mgeni yeyote ajaye bila kujali ametoka wapi, yeye ni nani, ana rangi gani, kabila gani au ana wadhifa gani. Mchango wa lugha ya Kiswahili katika kukuza biashara, kuwasiliana na kuwa na mahusiano ya kifamilia ni mkubwa ambao pia umechangia kwa kiasi kikubwa kurahisisha na kuufanya Muungano wetu kuwa na nguvu na mizizi ya asili.

Mikusanyiko na watu kutoka mataifa mbalimbali kuchangamana na Watanzania.
Uwepo na ujio wa wageni mbalimbali katika ardhi ya nchi zetu zote mbili, umeweka mahusiano kuwa karibu zaidi na kuweza kuoleana na kuanzisha familia ambazo zina mizizi ya nchi wanazotoka wageni hao, lakini ukizingatia mzaliwa kwao ni Tanzania iwe Visiwani au Bara.

Kama ilikuwa rahisi kwa watu wanaotoka mataifa ya mbali kushirikiana na watu wenye asili ya Zanzibar au Tanganyika inakuwa ni rahisi zaidi kuhimili undugu na uhusiano wa watu kutoka pande hizi mbili za Muungano. Nina hakika ni vigumu sana kumtenganisha mtu wa aina hii.

MATOKEO YA MAHUSIANO

Suala zima la kuoleana limeleta kufanana kwa mila, desturi, utamaduni, na mifumo ya maisha kuendeana na kufanana katika pande zote mbili za Muungano, hii imesaaidia sana watu kuona kuwa ni wamoja na kuthibitisha ni tofauti tu za kijiografia, mipaka na uwanda wa Mashariki, Magharibi, Kaskazini au Kusini.

MUUNGANO NI FARAJA KWA WATANZANIA

Muungano huu ni faraja kwa Watanzania kwa kuwa umewaweka huru ndani ya nchi yao, kila mmoja ana uamuzi wa kwenda kaskazini, MasharikiI, Magharibi na Kusini ili mradi havunji sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hamkwazi mtu yeyote ambaye anapashwa kuishi ndani ya Jamhuri pendwa na ya kipekee duniani ya nchi ya TANZANIA.

NCHI ZILIZOWAHI KUUNGANA NA KUSAMBATARIKA

Tuangalie nchi ambazo zilijaribu kuungana duniani wakati wa karne ya 18 na 19 wimbi la kuungana lilikuwa kubwa mno na nchi nyingi duniani ziliungana na kudumu kwa muda mrefu kama ule wa Jamhuri ya Nchi za Kishosalist za Kisovieti –USSR iliyokuwa na nchi 15 zilizoungana na kugeuzwa kuwa majimbo.

Utakumbuka katika miaka ya 1990 Rais na Katibu Mkuu wa wakati huo wa nchi ya USSR Michael Gobachiev, alikuja na sera yake ya “Uwazi na Uwajibikaji” au “Glasinosis and Perestroika” ambapo alitaka majimbo hayo 15 yawe huru kila moja likijiendesha lenyewe pasipo kutegemea mfuko mkuu wa Muungano na huu kuwa chanzo kikubwa cha majimbo yaliyounda USSR kusambaratika na kurejea katika nchi zao ndogondogo za awali.

Katika suala zima la Muungano mambo ambayo yanaweza kuusamabatisha ni pamoja na mifano hai kama maafa yaliyowahi kutokea katika suala zima la ubaguzi kama vile Hitler wa Ujerumani na dhana ya chuki kwa Wayahudi, Wahispania dhidi ya Waislamu, huko Hispania na Makaburu wa Afrika ya Kusini dhidi ya wazalendo Weusi wa Afrika ya Kusini huko Sharpville na yale ya Wahutu dhidi ya Watusi.

Ukirejea kilichoandikwa hapo juu utaona faida ya ukarimu na maamuzi ya kushirikiana na watu mbalimbali ambayo imejenga dhana ya kuwa na utu na kumthamini kila binadamu ambayo waasisi wetu wa Muungano walisisitiza sana na kuelimisha kila uchweo.

Muungano mwingine wa nchi za Afrika kama ule wa Elitria na Ethiopia ambao ulidumu kuanzia mwaka 1952 mpaka 1962 ndani ya miaka 10 Elitria lilikuwa jimbo ndani ya Shirikisho la Ethiopia.

Kutokana na ubinafsi na kutofautiana kwa viongozi nchi hizi mbili zilivunja Muungano na baadaye kusababisha vita ya wenyewe kwa wenyewe na kuleta madhara makubwa ikiwemo vifo na uharibifu wa mali kwa kipindi kirefu hadi viongozi wa Ethiopia na Elitria wametia saini mkataba wa amani tukio ambalo lilishuhudiwa na Mfalme wa Saudi Arabia Salman bin Abdulaziz katika Mji wa Jeddah, Katibu Mkuu ya Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na maafisa wa Umoja wa Afrika walikuwepo katika tukio hilo tarehe 16 Septemba 2018.

Hii inakuja miezi miwili baada ya Rais wa Eritrea Isaias Afewerki na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kusaini mkataba mwingine wa amani wa kumaliza uhasama uliodumu kwa takriban miongo miwili na kurejesha tena uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo mbili jirani. Aidha, Muungano wa Cape Verde na Guinea Bissau ni muungano uliodumu kwa muda mfupi sana na kusambaratika.

1960 Cameroon iliyotawaliwa na Wafaransa ilipata uhuru na mwaka uliofuata 1961 Cameroon iliyotawaliwa na Waingereza ilipata uhuru na kuungana kuwa Jamhuri ya watu wa Cameroon ambayo matatizo yake ni makubwa na wanapigana na kutoelewana kwa misingi ya kuongea lugha mbili tofauti na wale wanaoongea Kiingereza kuona wanaonewa na Cameroon ya Kifaransa.

Aidha hapa inadhihirisha dhana ya kuongea lugha moja na kuelewana ni msingi wa kujenga Muungano imara na kutokubali kuyumbishwa na watawala wakoloni kwa kuwadanganya na kuwachanganya waafrika kuwa anayeongea kifaransa ni bora zaidi kuliko anayeongea kiingereza, jambo lililotawaliwa na dhana ya ubaguzi.

Columbia ni jina lililomiliki nchi tatu yaani Equador, Venezuela, na Columbia baada ya kuanguka utawala wa Gran Columbia mwaka 1830 nchi hizi zikawa mahasimu na kusambaratika kila moja kuelekea muelekeo wake na kutawaliwa na wakoloni ambao kwa asili walihakikisha wanawagawa kwa kuwapa mipaka na kuhakikisha hawawi wamoja ili kudhoofisha juhudi zozote zinazoelekea kudai uhuru na kuwa na nguvu ya pamoja.

Nchi ya Comoro ni ya Muungano wa visiwa vingi ambavyo Muungano huo ni wa mashaka mashaka kwani mara baada ya uhuru 1975 kutoka kwa Nchi ya Ufaransa hadi 2020 Muungano huo umeshashuhudia dhamira na uthubutu wa kufanya mapinduzi mara 20. Hii inadhihirisha Muungano huwafanya kuwa imara zaidi na kudhibiti maadui wanaotaka kusambaratisha Taifa lolote lile duniani.

Nchi ya Croatia ilikuwa ni sehemu ya dola ya Austro- Hungariano Dola katika mwaka 1978 Croatis, Serbia na Slovenia ambayo ilikuwa chini ya himaya ya ufalme ilijulikana kama Yugoslavia kufuatia vita kuu ya pili Yugoslavia ikiwa Shirikisho huru la Kikomunisti chini ya Rais Warshal Tito ingawa Croatia ilitangaza uhuru wake mwaka 1991 ilichukua miaka kadhaa kuuweka katika mikono yake .

Bali wangekuwa wamoja isingewasumbua kwa kiasi kikubwa kama hicho siku zote umoja na nguvu utengano ni udhaifu. Checkslovakia kabla ya vita ya Pili ya Dunia ilikuwa ni Muungano wa nchi mbili yaani ya Cherck na Slovakia.

TUKILINDE TULICHONACHO TUSITEGEMEE KILICHOPO MTINI

Kwa kuwa wahenga walisema “Ndege mmoja mkononi ni mali na bora mara elfu mia kuliko ndege mia ambao hunao mkononi”. Wakaongeza wahenga hao “Msafiri Pwani aliyeko baraste huyo ameshafika, kadhalika wakanena “Silaha haijaribiwi vitani”. Misemo yote hii inampa mwanadamu tahadhari na ufunuo katika ustawi wa maisha yake. Tulichonacho ni Almasi tusidanganyike na walioshindwa kuungana.

Tumeona nchi nyingi zilizoungana na kusambaratika tumeona USSR ilivyosambaratishwa na Gorvachev kadhalika Ujerumani Mashariki ilivyomezwa na ile ya kibepari, Yaani Magharibi, Yugoslavia ilivyosambaratika, na baadhi ya Muungano katika nchi za Ulaya Mashariki.