Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya
TAASISI ya Tulia Trust inayoongozwa na Mbunge wa Jimbo la Uyole jijini Mbeya ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Tulia Ackson, imeanza rasmi ujenzi wa nyumba ya familia ya mzee Anyomwisye Mwalyaje Mkazi wa mtaa wa Mwafute,Kata ya Ilemi, ambaye makazi yake yaliteketea kwa moto usiku wa Septemba 5, 2025 kufuatia hitilafu ya umeme.
Ujenzi huo umeanza baada ya Dkt.Tulia kutembelea familia hiyo mara baada ya tukio hilo na kutoa ahadi ya kuwajengea nyumba mpya kufuatia kupoteza makazi na mali zote.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha vifaa vya ujenzi katika eneo la tukio, Addi Kalinjila, Mwakilishi wa Taasisi ya Tulia Trust Kitengo cha Habari, amesema taasisi hiyo imeanza ujenzi mara moja ili kuhakikisha familia hiyo inarejea kwenye maisha yao ya kawaida.

“Tulia Trust imekuwa mstari wa mbele kushughulikia masuala ya kijamii. Leo tupo hapa Mwafute kumwakilisha kiongozi wetu, Dkt. Tulia Ackson, kutekeleza ahadi yake ya kuwajengea nyumba familia hii ili warejee katika hali ya kawaida,”amesema Kalinjila.
Amebainisha kuwa vifaa muhimu vya ujenzi vimewasili, vikiwemo tofali, mchanga na saruji, na kwamba kazi imeanza rasmi eneo la mradi.
Aidha, Kalinjila amesema nyumba hiyo ni miongoni mwa nyumba 22,zilizojengwa kupitia Tulia Trust katika Jimbo la Uyole, Jiji la Mbeya na maeneo mengine nchini, ikiwa ni muendelezo wa juhudi za taasisi hiyo kuboresha maisha ya wananchi.
Kwa upande wake, Diwani Mteule wa Kata ya Ilemi, Baraka Zambi (CCM), amesema aliambatana na Dkt. Tulia mara baada ya kupata taarifa za janga hilo na kukutana na familia hiyo, ambapo mbunge huyo aliahidi kujenga nyumba mpya. Amesema vifaa vyote vimejumuishwa na ujenzi tayari unaendelea.

“Wananchi wa Ilemi tutaungana mkono na Tulia Trust kusaidia katika mahitaji madogo madogo yatakayojitokeza ili kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati,”amesema diwani huyo.
Naye Nsajigwa Mwalyaje, mmoja wa wanafamilia, ameishukuru serikali na Dkt. Tulia kwa msaada mkubwa walioupata tangu kutokea kwa janga hilo.
“Tunamshukuru Mungu kwa kutuepusha na maafa,tulikuwa watu watano ndani ya nyumba na wote tuliokoka. Hata hivyo, mali zote ziliteketea. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Mbunge na kuomba aendelee kuwasaidia hata wengine watakaokumbana na majanga kama haya,” amesema.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi