December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tujenge viwanda kwa maisha bora kote nchini-Prof Mpanduji

Na Mwandishi Wetu

SHIRIKA la Kuhudumia Viwanda Vidogo Nchini (SIDO) limesema linajivunia kuwa sehemu ya mafanikio ya Tanzania kuingia katika orodha ya nchini ya uchumi wa kati sambamba na kufanikisha azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kuwa nchi ya viwanda ifikipo mwaka 2025.

Aidha SIDO imewaomba Watanzania kujenga viwanda ili kuboresha maisha watu kila pembe ya Tanzania kwa sababu umeme upo na unaendelea kufuliwa hadi kufikia MW 3000 katika miaka mitatu ijayo.

Viwanda, ameeleza, vitaibua maisha bora kila vitakapokuwa hasa viwanda hivyo vitakuwa ni viwanda vya kuchakata mazao ya wananchi na vyakutengeneza vifaa vya kubadilisha maisha ya wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa SIDO, Profesa Sylvester Mpanduji, aliwataka Watanzania kuibua mawazo ya viwanda na kuyapeleka mawazo hayo katika ofisi za SIDO wilayani na mikoani ili yachambuliwe na kuweza kuanzisha viwanda.

Aliongeza kwamba SIDO ina matawi kila mkoa nchi nzima na ina wataalumu wa kutoa mafunzo ya kufanya biashara na kutumia teknolojia ili Watanzania wajiajiri katika nyanja mbali mbali ya ujasiriamali.

Aliwaomba Watanzania kulitumia shirika hilo kujipatia elimu na mafunzo yakuwawezesha kuanzisha viwanda vidogo kuchakata mazao yao na kuyaongeza thamani.

“Tayari SIDO imeshajenga viwanda darasa (industrial sheds) katika maeneo mbali mbali nchini lengo likiwa kuwawezesha wajasiriamali kupata mafunzo ya kuzalisha bidhaa zao katika mazingira wezeshi na kupatiwa vibali vyote vya mamlaka za nchi il iwafanye biashara ya uhakika,” alisema Prof.Mpanduji

Alitaja mikoa yenye viwanda darasa kuwa ni Dodoma, Mwanza, Simiyu , Kagera, Geita , Mtwara na Katavi. Kwa msukumo wa Serikali ya Rais John Maguli na ushirikiano wa wadau wengine, SIDO imesimamia kwa mafanikio ujenzi wa viwanda 8,477 ambavyo vimezalisha ajira zaidi ya 500,000.

Kati hivyo viwanda 201 ni viwanda vikubwa, viwanda 460 ni viwanda vya kati, and 3,406 ni viwanda vidogo na 4,410 ni viwanda vidogo kabisa.

Profesa Mpanduji amesema SIDO itaendelea kuimarisha idara ya teknolojia na ubunifu ili kuinua maendeleo katika sekta ya viwanda, na kutoa wito kwa Watanzania kutumia fursa ya uwepo wa SIDO kupata mafunzo ya ujasiriamali ili waweze kujiajiri.

“Uhai na uimara wa SIDO umeweza kudhihirika katika kipindi hiki cha miaka mitano chini ya serikali ya Rais John Magufuli, imeliwezesha shirika kifedha na kwa nyenzo na kuliwezesha shirika kuwafikia Watanzania kwa kuwapa elimu na mafunzo ya ujasiriamali,” amesema Prof.Mpanduji

SIDO kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo katika Maeonyesho ya Kimataifa ya Biashara jijini Dar es Salaam imekuwa ikiibuka mshindi wa kwanza kwa upande wa teknolojia na ubunifu.