December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tuhuma za rushwa zamponza Asukile

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira online

SHIRIKISHO la Soka Nchini (TFF) limemfungia mechi tano pamoja na faini ya Sh. 500,000 nahodha wa Tanzania Prisons, Benjamin Asukile.

Asukile amepewa adhabu baada ya hivi karibuni kumtuhumu mwamuzi wa mchezo wao wa watua ya 16 bora wa Kombe la Shirikisho la Azam ‘ASFC’ dhidi ya Yanga uliomalizka kwa timu yao kukubali kichapo cha goli 1-0 na kuondolewa katika michuano hiyo.

Baada ya kumalizka kwa mchezo huo kupitia mahojiano yake na mtangazaji wa Azam TV, asukile alisema mbali na mwamuzi huyo kuwapendelea Yanga lakini pia viongozi wa klabu hiyo waliwatafuta wachezaji wa Prisons ili kuwahonga Sh. Milioni 40.

Tuhuma hizo zilizua mijadala mingi huku serikali kupitia Taasisi na Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) ikimtaka mchezaji huyo kuwasilisha Ushahidi juu ya tuhuma hizo.

Taarifa iliyotolewa jana na TFF imeweka wazi kuwa, Kamati ya Mashindano ilipitia ripoti ripoti mbalimbali za mchezo huo baada ya kumalizika kwa raundi ya Tano na kujiridhisha kuwa asukile ametenda kosa.

Pia Kamati hiyo ilibaini Asukile kutoa shutuma za rushwa dhidi ya timu pinzani na shauri hilo limepelekwa katika Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa hatua zaidi.

“Asukile ametenda makosa ya kutoa maneno ya kejeli, kashfa, udhalilishaji na shutuma dhidi ya wapinzani wao Yanga, wachezaji wao wa kigeni waamuzi pamoja na TFF,”.

“Kufuatia makosa hayoTFF imemfungia kucheza mechi tano za mashindano rasmi ya TFF pamoja na faini ya Sh. 500,000 kwa mujibu wa kanuni ya 38:2, 39:5-3 ya kanuni za Ligi Kuu ambazo zinasomeka pamoja na kanuni za kombe la Shirikisho,” ameweka wazi taarifa hiyo.

Baada ya adhamu hiyo, uongozi wa Prisons umeiomba radhi TFF, ciongozi na wanachama wa Yanga, waamuzi, wapenzi na mashabiki wa soka nchini kwani wanatambua na kuthamini misingi ya nidhamu na utu huku wakipingana na vitendo vyoyvyote vya udhalilishwaji wa kanuni za kiuanamichezo.