Na Joyce Kasiki – TimesMajira Online, Dodoma
KATIBU wa Siasa na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi Jawadu Mohamed amesema tuhuma za zinazotolewa na aliyewahi kuwa Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Balozi Humprey Polepole na Askofu Gwajima dhidi ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan zinazodai kuwa hana uwezo wa kiuongozi,ni chuki binafsi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Julai 21,2025 Jawadu amesema viongozi waliowahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya chama hicho walitamani kuona Rais Samia anashindwa kuiongoza nchi jambo ambalo limekuwa tofauti na matarajio yao.
“Kwa jicho la karibu na tathmini ya maendeleo ya sasa, hoja zao hazina msingi wowote na zinaakisi chuki binafsi dhidi ya kiongozi anayefanya kazi kwa bidii kwa ajili ya Taifa.”amesema Jawadu na kuongeza kuwa
“Tofauti na kauli zao, ukweli ni kwamba Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia inaendelea kusonga mbele kwa mafanikio makubwa,kupitia miradi ya kimkakati, kama vile uzinduzi wa Dira ya Taifa 2050, Rais Samia ameweka mwelekeo wa kulifikisha Taifa katika uchumi wa trilioni 1 kwa mwaka.”
Aidha amesema katika uongozi wa Dkt.Samia,Taifa linaendelea kushuhudia ustawi mkubwa, kuimarika kwa amani, utulivu na nafasi ya Tanzania Kimataifa ,haya yote yakiashiria uongozi imara na wenye maono.
“Ni wazi kuwa shutuma hizi hazihusiani na ukweli wa utendaji kazi wa Rais, bali ni njama na jitihada za makusudi kujaribu kuvuruga taswira ya kiongozi ambaye anaungwa mkono na wananchi wengi,
“Lakini hii siyo mara ya kwanza , kila kipindi cha uchaguzi huibuka watu wanaotengeneza uzushi kwa lengo la kumdhoofisha kiongozi anayepata mvuto mkubwa kwa wananchi.”
Vile vile Jawadu amesema,kundi la watu kama Gwajima na Polepole, waliowahi kuwa sehemu ya mifumo ya uongozi, ni kubwa ambalo walitegemea Rais Samia atakwama.
“Kwa hiyo kikubwa hapa ni chuki binafsi ,walitarajia nchi ikwame, miradi ishindwe kuendelea , lakini tofauti na matarajio yao, Tanzania ya sasa ni ya mafanikio,
“Wamebuni hoja ya bandari, mikopo, na hata madai ya ufisadi ,lakini serikali imekuwa wazi kwa kutoa maelezo kwa umma, huku nchi nyingine zikiendelea kutumia njia hizo hizo kufanikisha maendeleo yao.”Amesema na kuongeza kuwa
“Tunajua bado kuna wengine walioko mafichoni, wakisubiri kujitokeza kwa nia ya kusambaza chuki zaidi dhidi ya Rais,lakini jambo moja ni wazi , Watanzania wamezidi kuonyesha imani yao kwa Dkt. Samia,wanaona maendeleo yanayopatikana, wanaguswa na maisha yao yanavyobadilika, na wanaelewa kuwa siasa za chuki hazitawasaidia.”

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi