December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TUCTA:Serikali ipandishe mishahara ya wafanyakazi

Judith Ferdinand,timesmajira,Online,Mwanza

WAFANYAKAZI  nchini kupitia Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania(TUCTA) wameiomba Serikali ipandishe mishahara ya wafanyakazi wa sekta zote binafsi na umma sanjari na kutolea maamuzi  suala la wafanyakazi waweze kupata stahiki zao zinazotokana na jasho lao.

Ombi hilo limetolewa na Katibu Mkuu wa TUCTA, Said Wamba akisoma risala mbele ya mgeni rasmi  ambaye ni Rais Samia Suluhu Hassan katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi)ambayo kitaifa yamefanyika mkoani Mwanza katika uwanja wa CCM Kirumba.

Wamba amesema kauli mbiu  katika sherehe za Mei Mosi mwaka huu ni “Maslahi bora,mishahara juu”Kazi iendelee ambapo zipo sababu nyingi za msingi  zilizowasukuma kuunda na kupitisha kauli mbiu hiyo kwa mwaka huu.

Amesema,ni wazi kwamba wafanyakazi wa sekta rasmi na walio katika sekta rasmi ni nyenzo muhimu katika kuinua uchumi wa nchi hivyo mishahara haijaongezwa kwa wafanyakazi hapa nchini miaka nane kwa sekta isiyo rasmi na miaka sita kwa sekta ya umma.

Hali hiyo imesababisha kupungua kwa ari na mori wa kazi hivyo kupunguza ufanisi na uwajibikaji mahala pa kazi huku gharama za maisha zimezidi kupanda ili hali stahiki na ujira zimeendelea kuwa duni.

Pia Amesema,kwa muktadha huo wa kuzingatia kuwa mishahara ya wafanyakazi haijapanda katika kipindi hicho chote huku hali halisi ya maisha imebadilika na gharama za bidhaa kupanda wanaiomba Serikali  ipandishe mishahara ya wafanyakazi wa sekta zote binafsi na umma.

TUCTA wanaiomba Serikali itolee maamuzi suala la baadhi ya mashirika ya umma ambayo miundo yao ya utumishi haijapitishwa na mamlaka  husika hivyo kuzuia nyongeza ya  mishahara za kila mwaka ili wafanyakazi waweze kupata haki yao stahiki inayotokana na jasho

lao.

Aidha ameishukuru Serikali kwa kufanya punguzo kidogo la Kodi kwa mwaka 2020 pamoja na kuwa viwango vya sasa vya kodi ni vikubwa huku wakiwahimiza waajiri na wafanyabiashara na wote wanaotakiwa kulipa kodi kufanya hivyo kwa kufuata sheria.