Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Dar
CHAMA cha Umoja wa Makandarasi na Watoa Huduma Shirikishi Tanzania (TUCASA),kimeiomba Serikali kuanzisha mfumo wa kisheria wa sheria ya malipo(Security of Payment Act (SOPA),katika sekta ya ujenzi ili kusaidia kuimarisha mazingira ya kazi kwa waaakandarasi wazawa katika utekelezaji wa miradi ya umma.
Ombi hilo limetolewa jijini Dar-es-Salaam Machi 6,2026 na Mwenyekiti wa TUCASA,QS Samuel Marwa wakati akizugumza na waandishi wa habari.
Amesema TUCASA inapendekeza kuanzishwa kwa mfumo wa kisheria wa sheria ya malipo ili kusaidia kuweka mfumo wa kisheria unaolazimisha malipo ya kazi za ujenzi kufanyika ndani ya muda maalumu pamoja na kuweka utaratibu wa haraka wa kutatua migogoro ya malipo.
“Uwepo wa sheria hii utasaidia kuweka utaratibu wa wazi wa malipo na kupunguza changamoto ya ucheleweshaji wa fedha, hali ambayo kwa sasa imekuwa ikiathiri uwezo wa kifedha wa wakandarasi wengi wa ndani,”amesema Marwa
Amesema ucheleweshaji wa malipo ya kazi zilizokamilika na kuthibitishwa umekuwa changamoto inayokwamisha ukuaji wa wakandarasi wa ndani na kupunguza uwezo wao wa kushiriki kikamilifu katika miradi ya maendeleo.
Amefafanua kuwa kutokana na hali hiyo, wakandarasi wengi hulazimika kukopa fedha katika taasisi za kifedha kwa riba kubwa ili kuendelea na utekelezaji wa miradi waliyopewa na taasisi za umma.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo amesema hali hiyo huongeza gharama za miradi na wakati mwingine husababisha baadhi ya kampuni kushindwa kuendelea na shughuli zao au hata kufilisika kutokana na mzigo wa madeni unaotokana na kuchelewa kwa malipo.
Akielezea uzoefu wa kimataifa Marwa amesema unaonesha kuwa uwepo wa sheria kama hiyo husaidia kuimarisha mtiririko wa fedha katika sekta ya ujenzi na kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa miradi.
Amesisitiza kuwa sheria kama hiyo tayari inatumika katika nchi mbalimbali zikiwemo Australia, Uingereza, Singapore na Malaysia ambapo imechangia kuimarisha sekta ya ujenzi na kulinda maslahi ya wakandarasi.
Katika hatua nyingine TUCASA imeipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali zinazochukuliwa kuimarisha ushiriki wa waaakandarasi wa ndani katika miradi mikubwa ya maendeleo ya miundombinu nchini.

More Stories
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama
Kihongosi amtaka mkandarasi kuwalipa vibarua stahiki zao