January 25, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TTB yatakiwa kuongeza ubunifu

Na Penina Malundo, timesmajira Online

Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imetakiwa kuongeza jitihada katika kubuni programu mbalimbali za kutangaza vivutio vya Utalii.

Wito huo umetolewa leo na Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana (MB),alipo kutana na Menejimenti ya Bodi hiyo Jijini Dar es Salaam.

Chana ameeleza kuwa licha ya kwamba TTB inafanya jitihada kubwa ya kuhamasisha utalii bado jitihada hizo haziendani na utajiri Mkubwa wa mazao ya Utalii yaliyopo Tanzania.

Waziri Chana ameongeza kuwa, ipo haja kwa Bodi hiyo kuongeza nguvu kuelimisha umma juu ya umuhimu wao kushiriki kikamilifu katika masuala ya Utalii.

Akielezea Mafanikio mbalimbali yaliyotokana na utendaji wa Bodi hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Bodi hiyo, Felix John ameyataja kuwa ni pamoja na kuongeza Masoko katika nchi mbalimbali kama China, Urusi, India, nchi za Kiarabu na Ulaya.

Mafanikio mengine ni pamoja na kuhamasisha Utalii wa ndani kupitia Maonesho, program za kielimu kama vile ya “Panda Mbegu”, kuimarisha Matumizi ya TEHAMA katika kuhamasisha na kuhabarisha watalii hasa kipindi hiki cha janga laUVIKO 19.

Licha ya kupongeza jitihada za Waziri wa Maliasili, Balozi Dkt. Pindi Chana kwa kusimamia vyema dira ya Wizara, Afisa Utalii Mwandamizi Kanda ya Pwani Goodluck Mdumi, ametoa wito kwa jamii kuungana na Serikali kulipeleka mbele gurudumu la maendeleo kupitia sekta ya Utalii.