November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TSC yajivuni kuhudumia Walimu 266,388 katika malalamiko mbalimbali

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

KATIBU Ofisi ya Rais,Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC)Mwl.Paulina Nkwama amesema mpaka kufikia Septemba 30, 2022, Tume hiyo imehudumia jumla ya Walimu 266,388 Tanzania Bara, wakiwemo 177,956 wa Shule za Msingi na 88,432 wa Shule za Sekondari.

Katibu huyo ameeleza Jijini hapa leo Katika kikao chake na Waandishi wa habari wakati akieleza kuhusu utekelezaji wa Taasisi hiyo na vipaumbele vyake kwa mwaka  2022/2023.

Amesema katika kipindi cha kuanzia Machi, 2021 hadi Septemba, 2022, TSC imefanikiwa kutekeleza majukumu mbalimbali ambayo yameendelea kuboresha mazingira ya Walimu na Sekta ya Elimu kwa ujumla.

Ameeleza kuwa jumla ya Walimu 16,749 waliajiriwa, wakiwemo 8,949 wa Shule za Msingi na 7,800 wa Shule za Sekondari na jumla ya Walimu 15,802 walisajiliwa, Walimu wa Shule za Msingi walikuwa 8,512na Sekondari walikuwa 7,290.

“Katika kuboresha mazingira ya elimu nchini Jumla ya Walimu 6,949 sawa na asilimia 100 walithibitishwa kazini wakiwemo 3,949 wa Shule za Msingi na 3,000 wa Shule za Sekondari,”amesema.

Sambamba na hayo alisema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa kuhakikisha kila Mwalimu aliyestahili amepanda cheo na kwa  kuwa zoezi hili ni endelevu, TSC imekuwa ikishughulikia changamoto ya mwalimu mmoja mmoja kwa wale ambao wamekuwa wakilalamika kucheleweshwa kupandishwa madaraja.

Kwa kudhihirisha  hayo,Katibu huyo wa TSC amesema jumla ya Walimu 47,158 waliopandishwa cheo (Walimu 22,943 ni wa Shule za Msingi na 11,524 wa Sekondari kwa mwaka 2021/2022) huku kwa mwaka 2020/2021 walimu waliopandishwa cheo ni 126,346.

Amefafanua kuwa,jumla ya Walimu 12,546 walibadilishiwa vyeo baada ya kujiendeleza kielimu, kati ya hao Walimu 9,059 ni wa Shule za Msingi na Walimu 3,487 ni wa Shule za Sekondari na kuongeza kuwa katika kipindi hicho jumla ya Walimu 3,912 wa Shule za Msingi na Sekondari walistaafu kazi.
  
Ametaja mafanikio mengine ya tume hiyo kuwa mkataba wa ajira za Walimu uliokuwa umeandikwa kwa lugha ya kiingereza ulitafsiriwa kwa lugha ya kiswahili ili kuwarahisishia walimu kwenye matumizi ya Mkataba huo.

Pamoja na hayo amezungumzia miiko na maadili ya Utumishi wa walimu amesema Serikali imetoa fedha zilizoiwezesha Tume kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wajumbe wa Kamati za Wilaya zote 139 ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Walimu na Utumishi wa Umma.  

Aidha tume hiyo imetoa mwongozo wa kuwajengea uwezo Wakuu wa Shule kusimamia nidhamu ngazi ya Shule. Mwongozo huo ulisambazwa na OR – TAMISEMI, kwa Wakuu wa Shule na unapatikana kwenye tovuti ya Tume – www.tsc.go.tz. Wakuu wa Shule ni Mamlaka ya nidhamu kwa Walimu wanaofanya makosa mepesi kwa mujibu wa Kanuni ya 12(1-3).

Katika hatua nyingine Mwalimu Nkwama ametumia nafasi hiyo kueleza vipaumbele vya tume hiyo Kuwa itaendelea kusimamia Utumishi na Maendeleo ya Walimu kwa kudumisha Maadili na Nidhamu kwa Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari katika Utumishi wa Umma.

Amesema TSC  itahakikisha Walimu wenye sifa ya kupandishwa vyeo na kubadilishiwa kazi wanapata huduma hiyo kwa wakati baada ya kibali kutolewa na Mamlaka husika.

“Tume itaendelea na ujenzi wa jengo la Ofisi za Tume Makao Makuu na kufuatilia ukamilishaji wa Muundo wa Maendeleo ya Utumishi na Mishahara wa Tume pamoja na kuanza kutumia Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Masuala ya Utumishi wa Walimu kwa majaribio na kuendelea kutoa elimu kwa watumiaji wa Mfumo huo kuanzia ngazi ya Shule,”amesisitiza na kuongeza kuwa;

Tume itaendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa Watumishi wa Tume kwa kuwaongezea ujuzi, kuwapatia ofisi na vitendea kazi na kuongeza uelewa kwa Wadau kuhusu Tume ya Utumishi wa Walimu na majukumu yake,”amesema.