January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TSC watoa faraja kwa watoto yatima

Na Adili Mhina

WATUMISHI wa Tume ya Utumishi wa Walimu nchini (TSC) wametembelea kituo cha watoto yatima cha Nyumba ya Matumaini kilichopo eneo la Miyuji jijini Dodoma na kuwapatia mahitaji mbalimbali.

Ziara hiyo iliongozwa na Katibu wa TSC, Paulina Nkwama ambaPo ilikuwa ni sehemu ya kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma.

Mwalimu Nkwama alieleza kuwa, pamoja na kuwahudumia wateja wanaofika ofisi za TSC katika Wiki ya Utumishi wa Umma, wafanyakazi wa tume hiyo waliona ni vyema kuwatembelea watoto kituoni hapo kwa lengo la kuwasalimia.

“Pamoja na kwamba tumeendelea kutoa huduma kwa wateja wanaotembelea ofisi zetu, watumishi wa tume kwa hiari yao waliamua kuchangishana fedha kidogo wakanunua baadhi ya mahitaji ya watoto na wamekuja kuwaona,” aMEsema Nkwama wakati akizungumza na uongozi wa kituo hicho.

Katibu huyo amewaasa watoto katika kituo hicho kuhakikisha wanazingatia masomo yao kikamilifu ili waweze kufanya vizuri na baadae kumudu maisha yao wenyewe na kuwa na mchango katika kulitumikia Taifa.

“Pamoja na uwepo wa changamoto za hapa na pale ambazo tumeelezwa na Sister, tunawaomba mhakikishe mnasoma kwa bidii. Tume ya Utumishi wa Walimu inashughulika na walimu katika masuala ya ajira, maadili na maendeleo yao. Walimu hao ndio wanaowafundisha ninyi, na wakiwafundisha tunatarajia tupate matokeo chanya,”amesema Nkwama.

Nkwama aliongeza kuwa, “elimu ni haki yenu, hakikisheni kwamba walimu wanaingia darasani na wanawafundisha, na ninyi mnaofundishwa mpokee yale mnayofundishwa na myazingatie, mwanadamu atajikomboa pale ambapo atakuwa amejikomboa kifikra.”

Kwa upande wake Mkuu wa Kituo hicho, Aurea Kyara alieleza kuwa, kwa sasa kituo kinahudumia watoto 67 ambao wanaanzia umri wa miaka mitatu hadi miaka ishirini na tano na wanasoma madarasa tofauti tofauti.

Alimshukuru Katibu pamoja na watumishi wa TSC kwa kuwatembelea huku akieleza kuwa wanakaribisha mtu yeyote anayependa kuwatembelea watoto hao kwa kuwa wakiona wageni wanakuja kuwasalimia wanapata faraja na kuona kuwa jamii inawajali.

“Tunawashukuru sana kwa moyo wenu wa upendo, mnapokuja watoto hawa wanajisikia faraja na wanaona wamezungukwa na jamii ya watu wanaowapenda na kuwajali. Tunamkaribisha mtu yeyote anayependa kuja kuwaona na kuzungumza nao,” amesema.

Kwa upande wa watoto hao, waliwashukuru watumishi wa Tume kwa kuwatembelea na kuomba watu wengine wenye moyo wa kuwajali wasisite kuwatembelea.

Miongoni mwa zawadi zilizowasilishwa na wafanyakazi hao ni unga wa ngano, sukari, sabuni, daftari, mabegi ya shule, dagaa, pipi, vinywaji pamoja na fedha taslimu.