January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TSB yataka kampuni zijisajili

Na Penina Malundo,Timesmajira Online

BODI ya Mkonge Tanzania (TSB) imewataka wafanyabiashara na kampuni zinazojishughulisha na biashara ya mkonge nchini kuhakikisha wanajisajili katika bodi hiyo ili kuweza kutambulika kwa mujibu wa sheria inavyowataka.

Hayo yamebainishwa na Ofisa Masoko na Uhamasishaji wa TSB, David Magari wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya 47 ya biashara ya kimataifa yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere Temeke, jijini Dar es Salaam.

Magari amesema mpaka sasa wakulima wadogo zaidi ya 9000 wameshasajiliwa kufanya biashara ya zao la mkonge na kubainisha kuwa zipo faida nyingi za mtu kujisajili ikiwemo kufahamika na kupata fursa mbalimbali zinazoletwa na serikali.

“Ili kuweza kufanya biashara au kulima mkonge unatakiwa usajiliwe na TSB, sisi tunatoa leseni ya kilimo cha zao hilo, leseni ya msindikaji na ya kufanyabiashara hapa nchini na nje ya nchi pamoja na ya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali.


“Kwa hiyo ni takwa la kisheria kwa kila anayejihusisha na biashara ya mkonge kujisajili na anayefanya kazi hiyo bila kusajiliwa atakuwa amevunja sheria na akikamatwa atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yatakayokuwa yakimkabili,” amesema Magari.

Amesema soko la mkonge kwa sasa bado zuri kwa maana kwamba uuzaji unafanyika na hakuna changamoto ya wakulima kukosa soko na hiyo ndiyo inawafungulia zaidi watu wengi kuweza kujiunga na kilimo hicho kila siku.

“Tufahamu kuwa bodi hii ni taasisi ya serikali ambayo ina jukumu la kusimamia zao la mkonge na kwamba wanafanya shughuli za utoaji wa leseni na vibali kwa wafanyabiashara wa zao hilo pamoja na kukusanya takwimu na kufanya tafiti mbalimbali kwa ajili ya kuzisambaza kwa wateja wao,” amesema.

Aidha amesema wamekuja katika maonesho hayo ya sabasaba wakiwa na lengo la kutoa elimu kwa watanzania, kutangaza fursa mbalimbali zilizopo kwenye sekta ya mkonge na kuhamasisha matumizi ya bidhaa mbalimbali za mkonge.