Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online DSM
TANZANIA Red Cross Society kwa ushirikiano na Serikali, inaendelea kutoa misaada ya kibinadamu kwa waathirika wa maafa yaliyosababishwa na mvua za El Niño katika mikoa takriban sita, hususan mkoa wa Manyara ambapo maporomoko ya ardhi yamesababisha madhara makubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Meneja wa kukabiliana na majanga wa Tanzania Red Cross Society Samwel Katamba amesema wanajenga nyumba 35 kati ya 163 zitakazojengwa na serikali kwa ajili ya waathirika wa maporomoko ya tope, mawe na magogo wilayani Hanang Mkoani Manyara yaliyosababisha vifo na watu kupoteza makazi yao.
“Mara baada ya tukio hili, (msalaba mwekundu) Red Cross Society ilifanya tathmini na kugundua mahitaji muhimu ya waathirika, kama vile magodoro, blanketi, vifaa vya jikoni, na neti. Tunataka kuhakikisha kuwa watu wanaopatwa na maafa wanapata mahitaji muhimu kama hivi ili kujilinda dhidi ya madhara ya mvua,” amesema Samwel Katamba, Meneja wa kukabiliana na majanga wa Red Cross Tanzania.
Red Cross imewafikia zaidi ya watu 163 ambao wameathirika kisaikolojia na kuwapa msaada wa kisaikolojia pamoja na elimu ya afya ya akili na jinsi ya kujilinda na mazingira yaliyoharibika.
“Hali ya Mkoa wa Manyara imeanza kutengemaa kutokana na misaada ambayo imepatikana, Watu wamepokea msaada wa chakula na vifaa vingine muhimu kama vile vifaa vya kuhifadhi maji, Timu yetu kubwa ya Red Cross, yenye zaidi ya watu 100, imejitolea kuelimisha jamii kuhusu usafi wa mazingira na jinsi ya kuzuia magonjwa kama vile kuchemsha maji na kuhifadhi taka,” alieleza Katamba.
Aidha, Red Cross inaendelea na juhudi za ujenzi wa nyumba kwa waathirika, Kati ya nyumba 112 zinazohitajika, tayari wameanza hatua za awali za ujenzi wa nyumba 35, huku serikali ikiahidi kujenga nyumba zilizobaki.
“Tutaendelea kushirikiana na serikali katika ujenzi wa nyumba kwa waathirika. Tupo katika hatua za awali za tathmini na utekelezaji wa mipango ya ujenzi. Miundombinu muhimu kama vile barabara, umeme, na maji itawekwa ili kuhakikisha maisha ya waathirika yanarejea katika hali ya kawaida,” aliongeza Katamba.
Kwa upande wake, serikali imeahidi kusaidia katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi na kupeleka huduma za kijamii kama vile umeme na maji.
“Sisi kama Red Cross tunaenda kujenga nyumba tutakuwa na wenzetu wa Serikali tunaenda kujengea watu nyumba ambazo zile nyumba jumla yake ni 112 lakini red cross tunaenda kujenga nyumba 35. Hatua za awali za ujenzi zimeanza na tunatarajia kuendelea kushirikiana na serikali katika utekelezaji wa miradi hii,” alisisitiza Katamba.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua