November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TRAMEPRO yawataka wananchi kushirikiana na Serikali kutunza mazingira

Na David John,Timesmajiraonline

SHIRIKA la Dawa Asili na Ulinzi wa Mazingira TRAMEPRO limewataka wananchi kufanya juhudi za kushirikiana na Serikali katika kutunza na kulinda mazingira Kwa Kila mtu kwenye nafasi yake ikiwa pamoja na kupanda miti.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam, katika mahojiano maalumu na Mwandishi wa habari hizi katibu mkuu wa Shirika hilo Boniventura Mwalongo amesema kuwa suala la utunzaji wa mazingira na upandaji miti lisiwe la Serikali pekee bali linapaswa kuwa ni la wananchi wote kwasababu mazingira ni uhai wa kila mtanzania.

Amesema kuwa wao kama Shirika la dawa asili na Ulinzi wa Mazingira TRAMEPRO wanaungana na Serikali katika kuadhimisha siku ya mazingira Duniani ambayo inafanyika Kila ifikapo Juni tano Kila mwaka.ambapo pia siku hiyo inatumika na watunga sera Serikalini na viongozi wa Wizara na wadau mbalimbali wa mazingira nchini na Duniani.

Amesema kuwa mazingira ni neno fupi ambalo linabeba hali zote zinazomzunguka binadamu ikiwamo viumbe hai wanyama,mimea,wadudu na Kila kitu kinachomzunguka binadamu hayo yote ni mazingira.

Amefafanua kuwa Katika nchi yetu kumefanyika juhudi mbalimbali kupitia Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan Kwa kutumia vipindi mbalimbali ambavyo vimerushwa lakini pia kupitia wiki ya MAMA hiyo yote ilikuwa ni hamasa ya kuhakikisha miti inapandwa na Mazingira yanaendelea kulindwa katika maeneo tofauti hivyo wao kama wadau muhimu wanaendelea na kampeni ya kuhamasisha kupanda miti katika maeneo kadhaa nchini.

“Lengo kubwa la kushiriki katika harakati za upandaji miti na utunzaji wa mazingira ni kutaka kuona azma ya Serikali ya kupanda miti milioni moja na laki tano inafikiwa katika Kila mkoa na mchakato huu hauwezi kufikiwa na Serikali pekee yake kupitia wakuu wa mikoa au Wilaya pekee yao bali kwa kushirikiana wananchi wote.”Amesema Mwalongo

Nakuongeza kuwa “Kila mwananchi akifanya juhudi za kupanda mti hata mmoja basi zoezi hili la kupanda mti litafikiwa kuliko kulifanya ni kazi ya watu furani tu.kuna wajibu wa kupanda miti hasa ya kivuli,matunda,nk.”amesisitiza

Ameongeza kuwa lazima kupanda miti ya asili ili kuendelea kuimarisha uoto wa asili katika nchi yetu ,kwani miti inatupatia hewa nzuri ,dawa ,marisho mazuri ya wanyama,hifadhi nzuri ya wadudu na viumbe wengine wanaotegemeana na binadamu katika kuishi kwao na binadamu hawapaswi kujipa haki miliki kama wanawajibu wa kuyatumia mazingira tupendavyo wakati Kila kiumbe kina nafasi yake.

Pia Katibu huyo wa Tramepro Amesema kuwa kabla hujafanya uharibifu wowote wa kimazingira basi Kuna haja ya kufanya tathimini ya athari ya kimazingira katika Kila eneo lazima iguse upoteaji wa mimea dawa maana lazima tukiri kwamba sehemu kubwa ya mimea dawa imeaza kupotea katika jamii yetu.

Naye Abdallah Kindamba ambaye ni mfagiaji wa barabara kuu ya morogoro akizungumzia utunzaji wa mazingira Amesema kuwa barabara inakuwa safi licha ya kukabiliana na changamoto za mikojo pamoja na vinyesi barabarani na hata madereva wa daladala kutokujari Koni ambazo wanaziweka wakati wakitekeleza majukumu yao.

Ameiomba Serikali kuendelea kutoa elimu Kwa madereva ili kuheshimu Alama za barabarani hasa wanapotekeleza majukumu ya kuliweka Jiji safi na waendelee kushirikiana ili kuweka mazingira sawa kwani ni jukumu la watanzania wote kuweka mazingira sawa.

Kwaupande wake Mwenyekiti wa zone B magomeni Kagera Mikoroshini Halfani Nambombe Amesema kuwa neno mazingira ni kitu mtambuka sana kwani mazingira ni mwanadamu na vitu vinavyomzunguka hivyo kama hayatatuzwa Kwa Dunia ya Leo basi tutakuwa kwenye changamoto kubwa sana.

Amesema kuwa mazingira ni muhimu Kila mmoja akaelewa na hasa akazingatia umuhimu wa kuacha utupaji wa taka ikiwamo mifuko ya plastiki yanaleta athari kubwa sana na kwakweli kama mazingira hayatatuzwa basi ni hatari hivyo kila mmoja Kwa nafasi yake na ikiwezekana elimu hiyo ipelekwe hata mashuleni ili elimu iwafikie zaidi watanzania kote waliko.