December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TRA yawataka wananchi kutoingiza bidhaa za magendo

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Wafanyabiashara wadogo wadogo wametakiwa kuacha kuingiza bidhaa za magendo zinazopitishwa katika njia zisizohalali ili kuepuka madhara ya kiafya na kiuchumi kwa Tanzania na mtu binafsi.

Hayo yameelezwa na Afisa Msimamizi wa Kodi Mkoa wa Kilimanjaro Odupoi Papaa katika zoezi la utoaji elimu kwa wafanyabiashara wa mipakani kuhusu athari za biashara za magendo kutoka TRA makao makuu iliyofanyika katika mpaka wa Kenya na Tanzania wa Holili.

Aidha amesema madhara ya bidhaa hizo yameanishwa katika maeneo matatu ikiwemo Afya ya walaji, kutokana na kutumia bidhaa ambazo zimeisha muda wake wa matumizi.

“Kumekuwepo na baadhi ya watu ambao wanabadilisha bidhaa kwenye mifuko mipya ikiwa bidhaa hizo zimekwisha muda wa matumizi na kupelekea,madhara makubwa kwenye afya zetu, hivyo tukatae bidhaa za magendo”amesema Papaa.

Aidha amewataka wananchi hao kuacha kutumia bidhaa za magendo kutokana na athari kubwa zinazopatikana katika bidhaa, huku akiwataka kuhakikisha bidhaa zinapita katika njia halali Ili ziwe bidhaa salama kwa afya ya walaji.

“Madhara mengine yanayopatikana ni kwa nyinyi wenyewe kukamatwa na bidhaa za magendo ambapo madhara yake ni makubwa ikiwemo kupigwa faini na kupelekea jela”Amesema Papaa.

Kwa upande wake, Afisa Mfawidhi Kituo cha Forodha Holili Yusuph Mwahu amewashauri wafanyabiashara wadogo wadogo kupitia lango Kuu kwani barabara ipo vizuri na ushuru upo vizuri na wameweka dirisha malumu kwa ajili ya kulipa ushuru kwa mujibu wa sheria kanuni na taratibu.

Hata hivyo, amewataka wafanyabiashara hao kutopita maporini kwa ajili ya kukwepa kodi kwa kupitisha bidhaa za magendo bali wapite lango kuu la Holili.

Sambamba na hayo, amekitaka kitengo cha elimu kwa mlipa kodi cha TRA kuendelea kutoa elimu mara kwa mara hasa sehemu za mipakani Ili uwelewa uwe mkubwa zaidi kwa jamii.

Naye Mkaazi wa Holili Abdul Abdul ambae awali alikua akifanya biashara ya magendo amesema baada ya kupata elimu ameacha kazi hiyo na anapita katika lango kuu, hivyo amewataka maafisa wa RTA waendelee kutoa elimu Ili watu wengi wawe na uelewa kuhusiana na athari za kupitisha bidhaa za magendo.

“Nawaomba maafisa wa forodha mnaozunguka nchi nzima katika kutoa elimu ya mlipa kodi muhakikisha elimu hii inawafikia watu wote, kwani kuna baadhi ya watu wanadhani kuna bidhaa ambazo haziruhusiwi kupita katika lango kuu jambo ambalo sio sahihi kwani bidhaa zote zikishakaguliwa zinaruhusiwa kupita”amesema Abdul.