Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Yusuph Juma Mwenda amesema Tanzania kujitegemea kwa mapato ya ndani haimaanishi kuwaongeza Wananchi Viwango vya ulipaji kodi bali ni kuongeza ufanisi kwa kutanua wigo wa kodi na kuzuia ukwepaji kodi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam November 21, 2025 Kamishna Mkuu Mwenda alirejea hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa wakati akizindua Bunge na kuwaapisha Mawaziri, kuwa Tanzania inapaswa kujitegemea kwa kiasi kikubwa kwa fedha za ndani.
Kamishna Mkuu Mwenda alisema ili kutekeleza kauli ya Rais kinachotakiwa ni kuzuia mianya ya ukwepaji kodi, kuweka mazingira mazuri kwa wanaolipa kodi vizuri na kuongeza wigo wa kodi na siyo kuongeza Viwango vya kodi inayolipwa.
“Nataka nichukue fursa hii, sisi TRA tukiwa sehemu kubwa ya kutekeleza ndoto na maagizo ya Mhe. Rais niwahakikishie kuwa kujitegemea kwa mapato ya ndani siyo kuongeza viwango vya kodi inayotozwa bali kuimarisha mifumo ya usimamizi wa Kodi kwa kuzuia mianya ya ukwepaji kodi, kutenda haki kwa walipakodi waliopo na kuongeza wigo wa kodi”

Amesema Serikali kupitia Wizara ya Fedha imeweka mifumo rafiki ya kidigitali inayorahisisha sana usimamizi wa kodi unaotoa fursa ya mlipakodi kupata huduma akiwa katika eneo lake la biashara bila kulazimika kwenda kwenye ofisi za TRA.
Katika hatua nyingine Kamishna Mkuu Mwenda amesema ustawi wa biashara yoyote unategemea utulivu ndani ya nchi na kuwataka wahitimu wa chuoni hapo kuwa mabalozi wa kuhakikisha Amani na utulivu nchini inakuwepo ili shughuli za kiuchumi ziweze kuendelea.

Amesema vijana wengi wana ndoto zao hivyo panapokuwa na changamoto zozote zitumike nyia rafiki katika kuzitatua ambazo hazitaharibu biashara na uchumi wa nchi ili kuwasaidia vijana kufikia ndoto zao.
Katika mahafali hayo ya 18 mgeni rasmi alikuwa ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bw. Elijah Mwandumbya ambaye alimuwakilisha Waziri wa Fedha Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) na kuunga moko kauli ya Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Mwenda kuwa Tanzania inaweza kujitegemea kiuchumi kwa kuongeza wigo wa kodi na kuongeza usimamizi katika sera na sharia za kodi.
Amesema Serikali imekuwa ikiiwezesha TRA kutekeleza majukumu yake na kuipa miongozo ambayo imesaidia kuiwezesha TRA kuvuka malengo kwa mwaka mzima wa fedha uliopita 2024/2024 kwa kila mwezi.

Mwandumbya ameipongeza TRA kwa kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini na uwekezaji na kuitaka iendelee kutekeleza wajibu huo wenye tija kwa ustawi wa Taifa.
Amesema TRA imekuwa ikifanya kazi kubwa katika kuendesha nchi kwa kuwa na mchango mkubwa wa mapato ya ndani ya nchi huku Chuo Cha Kodi kikitumika kuwapika watumishi wa Mamlaka hiyo na kuwafanya wawe bora zaidi.
Amesema TRA imechangia kwa kiasi kikubwa utulivu wa biashara uliopo nchini ambao pia unaletwa na amani na utulivu na kuongeza kuwa suala la amani siyo la kisiasa ni suala la uchumi na lina uhusiano wa moja kwa moja na maisha ya wananchi.
Awali Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRA,Uledi Mussa Abbas aliwataka wahitimu hao kuhamasisha jamii kuendelea kulipa kodi kwa hiari maana ulipaji wa kodi ni Uzalendo.
Amesema anatamani Chuo Cha Kodi kiwe kitovu cha umahiri cha masuala ya Kodi na Forodha Afrika ya kati kutokana na ubora wa hali ya juu wa mafunzo yanayotolewa na chuo hicho.
Katika mahafali hayo yaliyohusisha wahitimu 561 baadhi ya wahitimu waliofanya vizuri wametunukiwa vyeti na kupatiwa zawadi huku wahadhiri waliofanya tafiti mbalimbali nao wakitunukiwa vyeti na zawadi.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi