Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imetumia Maonesho 44 ya Biashara ya Kimataifa Dar is Salaam (DITF) yaliyomalizika jana kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa jijini kutoa elimu na shukrani kwa walipa kodi ikiwa ni pamoja na kuwaonesha jinsi kodi yao inavyotumika kwa maendeleo ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki kwenye Banda la TRA kwenye Viwanja hivyo, Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipa Kodi TRA, Richard Kayombo, amesema pamoja na kutoa shukrani kwa walipa kodi, pia wanao wadau mbalimbali ambao kwa miaka mitano wamekuwa wakiwasaidia katika ukusanyaji mapato kwa namna mbalimbali.
Ametaja wao hao kuwa ni Serikali yenyewe iliyopo madarakani, kuanzia Rais, wasaidizi wake kwa maana ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Waziri Mkuu, Bunge, vyombo vya utoaji wa haki kwa maana ya mahakama na viongozi katika ngazi ya mikoa na wilaya.
Amesema wanatambua mchango wa viongozi mbalimbali kama wakuu wa mikoa na wilaya ambao ni wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama katika maeneo yao.
Kayombo amesema kwa uwazi kabisa viongozi hao wamehusisha TRA kuwa sehemu ya kamati ya ulinzi na usalama katika mikoa yao kwa lengo la kuhakikisha makusanya ya mapato yanapatikana kwa usahihi na pale kunapokuwa na mkwamo wowote, tatizo hilo linashughulikiwa mara moja.
“Kwa hiyo kwenye ngazi ya mikoa na wilaya tunawashukuru sana wamekuwa sehemu ya matokeo ya mapato yote ambayo tumeyakusanya kwa miaka hii mitano,” amesema Kayombo na kuongeza;
“Tunavishukuru sana vyombo vya habari, sisi kama TRA tupo katikati hatuwezi kufika mbali, lakini kupitia vyombo vya habari tumepata msaada mkubwa kufikisha ujumbe kwa wananchi wetu waweze kuhamasika kulipa kodi.
Lakini vile vile vimekuwa mstari wa mbele kuibua mambo pale kunapokuwa na changamoto aidha kwa upande wa kwetu ili tuweze kujirekebishe, lakini pale panapokuwepo mianya ya ukwepaji kodi vimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha tunatambua wapi kuna mwanya ili tuweze kuuziba tuweze kuuziba.”
Kayombo alisema wao kama TRA wameshiriki Maonesho ya Sabasaba kuanzia tarehe moja hadi jana (Julai 13) na imekuwa ni faraja kubwa sana kwao kwa sababu wamepata nafasi ya kukutana na walipa kodi ambao wana maswali mbalimbali kuhusiana naa masuala wasioyajua.
Lakini pia alisema walipata nafasi ya kuwapa ufahamu wa jinsi gani wanakusanya mapato na kuwafahamisha yanakwenda wapi na yanafanya nini.
Amesema katika Banda lao Sabasaba walikuwa nazo picha za vielelezo mbalimbali ambavyo vinaonesha jinsi kodi yao inavyotumika.
Kayombo amesema katika Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi cha miaka mitano ni wakati muafaka mlipa kodi kutambua kodi yake imefanya kitu gani, kwani watu wengi wanajiuliza wakilipa kodi wanapata nini?
“Kwa hiyo kwenye banda letu ilikuwa ni wakati muafaka wa sisi kuwaonesha hayo, lakini pia kuwaonesha wananchi jinsi tunavyotoa huduma mbalimbali,” alisema Kayombo.
Alifafanua kwamba wamepata bahati ya kuwaonesha kwa mwezi huu wa saba kodi yao imefanya nini, ambapo wamekuwa na kampeni yao ya shukrani kwa mlipa kodi.
“Kwa hiyo tunapowaonesha tumefanya nini inakuwa nafasi nzuri kwetu kushukuru, kwani walipa kodi wamekuwa na mchango mkubwa na hii itahamasisha walipa kodi waliopo na wale ambao wanategemea kuwa walipa kodi, kama wafanyabiashara na wale ambao wamekuwa wakisuasua kwa njia moja au nyingine waweze kupata moyo wa kulipa kodi,” amesema Kayombo.
Ametoa mfano kwa upande wa sekta ya afya, akisema mambo mengi makubwa yamefanyika, upande wa miundombinu mbalimbali ya barabara, reli, meli, upande wa usafirishaji kwa njia ya anga na huduma za jamii kama maji, wananchi wanaona zimeboreshwa kwa kiwango kikubwa sana.
Amesema yote hayo yametokana na kodi ambayo kila mmoja wetu analipa kwa namna moja au nyingine.
Kayombo amesema kuna wale ambao hawafanyi biashara kabisa wanaweza kufikiri kuwa wao hawalipi kodi kwa sababu hawafanya biashara, au hajaajiriwa.
“Msisitizo ni kwamba kila mwananchi analipa kodi, kile kitendo cha kudai risti ukapewa risiti maana yake ni kwamba mauzo hayo ambayo yamefanyika kwa wewe kudai risiti ndiyo hesabu itakayotumika kukokotoa kodi,” amesema Kayombo na kuongeza;
“Kwenye Maonesho ya tumewasisitiza sana watu kudai risiti kila wanaponunua bidhaa na pale inapotokea mtu hatoi risiti au anatoa yenye udanganyifu, tunahamasisha wananchi waweze kutoa taarifa kwenye ofisi zetu zilizopo karibu au kwa chombo chochote cha dola kwa hatua zaidi na tuweze kuwatambua hao wanaohujumu juhudi nzuri za Serikali kukusanya mapato.”
Kayombo alizidi kufafanua kwamba hawaishi kwa kuwahamasisha wananchi kudai risiti, bali waweze kukagua risiti hizo wanazopewa, kwani wanaweza kupewa risiti, lakini ikawa haifanani na ile thamani ya bidhaa aliyonunua.
Amesema mchango wa wananchi iwe wanafanyabiashara au haujaajiriwa, bado unao mchango kwa kudai risiti na hapo wanakuwa wamechangia mapato ya Serikali.
Pia amesema wanahamasisha wananchi wanaofanyabiashara kutoa risiti kila wakati kwa kila mauzo, kwa sababu wale ambao wamesajiliwa kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) maana yake wao ni mawakala wa Serikali, hivyo wasipotoa risiti moja kwa moja ile asilimia 18 iliyopo kwenye mauzo yao wanakuwa wameiweka kwenye mifuko yao, hivyo wanakuwa wanaidhulumu Serikali na wanatudhulumu wote kama wananchi wa nchi hii.
“Kwa hiyo tunahamasisha pande zote mbili, wafanyabiashara wale wanaotoa risiti, lakini wateja wakumbuke kudai risiti kila wanapofanya manunuzi,” amesema Kayombo.
Kwa upande wake msimamizi mkuu wa banda hilo, Stephen Kauzee, ambaye ni Ofisa wa Elimu kwa mlipa kodi alisema katika banda lao la Sabasaba walikuwa wakitoa huduma mbalimbali.
Ametaja huduma hizo, kuwa ni huduma ya stempu kwa ajili ya mikataba, huduma ya TIN, huduma ya kulipia majengo na pia kupokea malalamiko na mawazo ambayo mlipa kodi anaona yanaweza kuisaidia TRA katika kukusanya kodi na katika shughuli zao.
“Na sisi pia tumekuwa tukichukua matatizo yao na kuyapatia ufumbuzi na yale ambayo hayawezekani tunayapeleka mbele. Kwa ujumla ujumbe wetu mkubwa ni kumshukuru mlipa kodi kwa sababu ni mtu muhimu sana kwetu katika miaka hii mitano iliyopita,” amesema.
More Stories
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best
Waziri Mavunde:Benki Kuu yanunua tani 2.6 za Dhahabu nchini
Kampeni msaada wa kisheria ya mama Samia kutatua kero za kisheria Katavi