December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TPHPA yaelimisha wananchi kufahamu mlipuko wa panya shambani

Na Joyce Kasiki Timesmajira online,Dodoma

MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA), imesema panya shamba ni moja ya visumbufu vya mazao vinavyofanya uharibifu mkubwa wa mazao shambani.

Kufuatia hali hiyo ,Ofisa kutoka Kituo cha Kitaifa cha Kudhibiti Baa la Panya Tanzania wa TPHPA,amesema lazima wananchi wagundue uwepo wa panya shamba hao mapema ili waweze kudhibitiwa na Mamlaka husika kabla hawajaanza uharibifu.

Tewele ameyasema hayo katika maonesho ya wakulima na wafugaji yanayoendelea jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari namna TPHPA wanavyodhibiti visumbufu vya mazao shambani ili kuzuia baa la njaa nchini.

“Huyu panyashamba anapatikana maeneo yote nchini,kwa hiyo ni vyema wananchi wakatambua dalili za uwepo wake shambani na kutoa taarifa ili wadhibitiwe.”amesema Tewele

Akielezea viadhiria vya mlipuko wa panya hao shambani,Tewele amesema , mkulima ataona mashimo hai ya panya, vinyesi vingi vya panya shambani, pia ataona njia nyingi za panya katika shamba lake, lakini pia ukipita usiku unakuta panya wanakatiza mara nyingi.

“Pia kutakuwa uharibifu wa mimea na mazao yaliyopo shambani kwa sababu panya anafanya uharibifu tangu hatua ya kwanza ya kupanda mbegu ambapo anaweza kuzifukua mbegu zote na kesho mkulima akirudi shambani anakuta mashimo yote yapo wazi.”amesema na kuongeza kuwa

“Hata mahindi yakifanikiwa kuota na kuanza kukomaa, panyashamba ana uwezo wa kulipandia na kulitafuna lote,na kumaliza mazao yote na hivyo kusababisha hasara kwa mkulima na Taifa kuweza kukumbwa na baa la njaa”

Amesema panya ana uwezo wa kufanya uharibifu wa hadi asilimia 100, hivyo mkulima anaweza kupanda mbegu kesho yake akakuta zimeliwa mashimo yote yako matupu.

Aidha amesema kuna milipuko ya panya iliyotokea katika baadhi Mikoa hapa nchini ikiwemo maeneo ya Kanda ya Ziwa wilaya ya Bariadi na Kishapu ambapo TPHPA imefanikiwa kuidhibiti kwa kutumia sumu .

Amesema panya wanapoingia shambani hufanya uharibifu mkubwa kwa kula mazao yaliyopo hivyo kusababisha hasara kwa mkulima.

Kufuatia hali amwsema,ni vyema wakulima wapate elimu hiyo ili waweze kubaini uwepo wao mapema.