March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TPDC Yajivunia Miradi ya Kimkakati Inayobadili Taswira ya Sekta ya Nishati Nchini

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

SHIRIKA  la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) linaendelea kutekeleza miradi kadhaa ya kimkakati ambayo inalenga kuimarisha sekta ya mafuta na gesi asilia nchini, sambamba na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Akizungumza katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, Afisa Utumishi kutoka TPDC, Elinaike Nabuti amesema,kupitia maonesho hayo, TPDC inaonesha kwa vitendo namna inavyotekeleza majukumu yake ya msingi, ikiwa ni pamoja na kusimamia na kuendeleza rasilimali za mafuta na gesi kwa manufaa ya Taifa.

“Elimu hii ni muhimu kwa wananchi ili waelewe fursa zilizopo katika sekta ya gesi na mafuta. Wananchi wanapata kujifunza kuhusu matumizi ya gesi asilia kwenye magari, majumbani, pamoja na miradi mikubwa kama ule wa LNG unaotarajiwa kutekelezwa mkoani Lindi,” amesema Nabuti.

Ametumia nafasi hiyo kuwakaribisha  wananchi kutembelea banda la shirika hilo ili kujifunza na kupata elimu juu ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na taasisi hiyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa TPDC, Marie Msellemu, amesema moja ya mafanikio makubwa yaliyopatikana ni usambazaji wa gesi asilia majumbani ambapo sasa wameshafikia Mikoa minne ya  Lindi, Mtwara, Pwani na Dar es Salaam.

“Tayari nyumba zaidi ya 5,000, magari takriban 7,000 pamoja na viwanda 57 vimeunganishwa na huduma ya gesi asilia,hii ni hatua kubwa ya maendeleo katika kuhakikisha nishati safi inapatikana kwa matumizi ya kila siku,” amesema Msellemu.

Vile vile amesema,kipo   kituo kikubwa cha usambazaji gesi asilia kilichopo Mlimani City jijini Dar es Salaam ambacho kinahudumia vituo vingine vya kujaza gesi kwenye magari, hatua inayochochea matumizi ya nishati safi na kupunguza utegemezi wa nishati zenye madhara kwa mazingira kama mkaa na kuni.

“Matumizi ya gesi asilia ni rafiki wa mazingira,hii ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kuhakikisha wananchi wanatumia nishati safi kwa ajili ya afya yao na ustawi wa mazingira yetu,” ameongeza.