December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TPA yashinda tuzo kwa utendaji bora

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline,Dar

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari (TPA) imeshinda tuzo ya mshindi wa tatu kwa utoaji huduma bora iliyotolewa katika Mkutano wa siku tatu wa Kikao Kazi kwa Wenyeviti wa bodi na Watendaji Wakuu wa Mashirika ya umma uliofanyika katika ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) wiki miliyopita.

TPA ni miongoni mwa mashirika yanayoshiriki katika mkutano huo, ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alikabidhi tuzo kwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka hiyo, Dkt. Elinami Minja aliyeamvana na Mkurugenzi Mkuu, Plasduce Mbossa.

“Tuzo hii imetokana na mamlaka hii kuleta mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma katika bandari zinazosimamiwa na TPA ikiwemo Bandari ya Dar es Salaam ambayo ipo chini ya uwekezaji kwa sasa katika baadhi ya maeneo ya utendaji,”alisema Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa TPA, Dkt. George Fasha.

“Kiuweli tumeanza kuona matunda ya uwekezaji huu yanayotokana na juhudi za uongozi wa TPA kuanzia bodi ya Wakurugenzi, uongozi pamoja na wadau wengine mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara wanaotufanya kuwa kinara katika utoaji huduma,” alisema Dkt Fasha kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu Mbossa.

Rais Dkt Samia Suluhu Hassan akimkabidhi Tuzo,Makamu Mwenyeki wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Dkt. Elinami Minja kwenye Kikao kazi cha Wenyeviti na Wakuu na Watendaji Mashirika na Taasisi zote za Serikali kilichofanyika kwa siku tatu Jijini Arusha ambapo TPA ilishinda nafasi ya tatu kwa utoaji bora wa huduma. kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa.

Dkt. Fasha alisema tuzo hiyo imetokana na utendaji mzuri wa mamlaka hiyo katika utoaji mzuri wa huduma na ukusanyaji wa mapato kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

“Hii inatupa motisha zaidi ya kufanya kazi kwa bidi na kuifanya TPA kuendelea kusimamia bandari zetu kwa ufanisi mkubwa kupitia maboresho makubwa ya utendaji yanayoendelea ili kuwavutia zaidi wafanyabiashara kutumia bandari hizi kupitisha mizigo yao,”alisema.

Katika kuhakikisha maboresho makubwa yanaendelea kufanyika, Dkt. Fasha alisema TPA kwa kushirikiana na Wizara ya Uchukuzi imekuwa ikichukua hatua mbalimbali , ikiwemo kuruhusu uwekezaji wa sh. bilioni 675 uliofanywa na DP World katika maeneo mbalimbali ya uendeshaji wa Dandari ya Dar es Salaam ili kuleta ufanisi.

Alisema uwekezaji huo tayari umeanza kuzaa matunda ambapo shehena za mizigo zimeongezeka ndani ya kipindi cha miezi mitatu kutoka makontena 7,151 Aprili 2024 hadi makontena 20.151 ilipofika Julai 2024

“Ni mikakati yetu kuifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa na ushindani zaidi na bandari nyingine duniani katika kutoa huduma bora zenye ufanisi,”alisisitiza.

Alisema kama Mamlaka imani kuwa kupitia mikakati mbalimbali ya utendaji , Bandari ya Dar es Salaam itashinda tuzo mbalimbali za kitaifa na kimataifa kupitia utendaji mzuri wa utoaji huduma.