Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
TAASISI ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) imeendelea kung’ara kwa mafanikio makubwa iliyoonyesha, hususan katika kuthibiti na kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari katika kilele cha maonyesho ya Kitaifa ya Wakulima (Nanenane) yaliyofanyika katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma,Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI, Nyasebwa Chimagu, amesema taasisi hiyo imepewa jukumu muhimu na Serikali la kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora, si tu kwa ajili ya uzalishaji, bali pia kwa kukuza ajira na biashara ya mbegu nchini na kimataifa.
“Mbegu bora ni msingi wa kilimo cha kisasa. Tunahakikisha ubora wa mbegu kuanzia shambani, kwenye maghala, maduka hadi viwandani. TOSCI imepata ithibati ya kimataifa, hivyo mbegu zinazozalishwa nchini zinaweza kuuzwa pia nje ya nchi,” amesema Chimagu.
Aidha amesema,TOSCI imetumia maonyesho ya mwaka huu, yaliyozinduliwa rasmi na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango, kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kutumia mbegu bora na namna ya kubaini mbegu feki.
Chimagu alieleza kuwa elimu hiyo imetolewa kwa wananchi zaidi ya 3,618 waliotembelea banda la TOSCI hadi kufikia Agosti 7, 2025.
“Tunawaelekeza wananchi kupiga 14852# na kuingiza namba za vocha ya mbegu walizonunua ili kujiridhisha na ubora wake. Hii ni hatua madhubuti dhidi ya mbegu feki,” aliongeza.
Zaidi ya wakulima 5,156 wamesajiliwa kupitia mfumo wa kidigitali kwenye maonyesho haya, hatua ambayo inawawezesha kunufaika na mbegu za ruzuku kupitia mpango wa Serikali ulioanzishwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuanzia msimu wa kilimo 2024/2025.
TOSCI imeendelea kusisitiza kuwa uzalishaji wa mbegu si tu kwa ajili ya chakula, bali ni fursa ya kiuchumi. Wakulima sasa wanaweza kuzalisha mbegu, kuuza, kuanzisha biashara, au kuajiriwa kama mawakala wa mbegu katika viwanda na maduka ya pembejeo.
Aidha, katika kuunga mkono kauli mbiu ya mwaka huu isemayo “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi,” amesema,TOSCI imetumia jukwaa hilo kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika uchaguzi ujao kwa kuchagua viongozi wenye dhamira ya kweli katika kuendeleza sekta ya kilimo.
Katika maonyesho hayo, TOSCI imehamasisha matumizi ya mbegu bora za mahindi, zao ambalo linachangia zaidi ya asilimia 60 ya nafaka nchini. Kupitia kampeni ya Rais Samia ya “Tupo Tayari Kuilisha Dunia,” taasisi hiyo imesisitiza kuwa mahindi ni zao la biashara na lisilo la chakula tu.
“Mpango wa mbegu za ruzuku ni mkakati wa Serikali kuongeza tija kwa wakulima. Maonyesho haya yamekuwa jukwaa muhimu la kutoa elimu hiyo kwa wakulima na wadau wote wa kilimo,” alisema Chimagu.
TOSCI imewahamasisha wakulima kote nchini ambao bado hawajasajiliwa, kwenda katika ofisi za kilimo za vijiji au kata ili kupata usajili na kunufaika na mbegu za ruzuku kabla ya msimu wa kilimo kuanza.
Chimagu alihitimisha kwa kusema kuwa mafanikio haya ni ushahidi kuwa maonyesho ya Nanenane si ya maonyesho tu, bali ni chombo cha mabadiliko katika kilimo na uchumi wa wakulima wadogo.
“Mbegu bora inalipa. Tunawaalika Watanzania wote kujifunza, kushiriki na kuwekeza kwenye sekta ya mbegu kwa sababu fursa ni kubwa sana,” alisisitiza.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina