January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TORITA yainua maisha ya wakulima Tabora

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

TAASISI ya Utafiti wa Zao la Tumbaku (TORITA) imepongezwa kwa kuinua maisha ya wakazi wa kata ya Tumbi katika halmashauri ya Manispaa Tabora kupitia kilimo cha zao la tumbaku.

Wakiongea na gazeti hili kwa nyakati tofauti wakazi wa Vitongoji vya Ufunga na Kibaoni katika Kijiji cha Tumbi kata ya Tumbi Wilayani ya Tabora wameishukuru sana Taasisi hiyo kwa kuwa karibu na wakulima na kuwapa elimu ya kilimo bora.

Gabriel Mwiga mkulima, mkazi wa Kijiji hicho ambaye pia ni Mwenyekiti wa wakulima wa tumbaku katika kata hiyo kupitia chama chao cha msingi Tumbi Amcos, amesema kuwa ushauri wa Taasisi hiyo umewapa manufaa makubwa sana.

‘Tunawashukuru sana TORITA kwa kuwa karibu zaidi na wakulima na kutupa elimu ya kilimo bora na mbegu bora zilizofanyiwa utafiti wa kitaalamu na zinazozaa tumbaku bora na yenye majani mengi’, ameeleza.

Amebainisha kuwa katika msimu uliopita pekee jumla ya kilo 263,000 za zao hilo zilizalishwa na wakulima wapatao 140 waliopo katika kata hiyo ambapo waliuza kila kilo kwa wastani wa bei ya sh 4800/- hadi 6000/- ambayo haijawahi kutokea.

‘Msimu uliopita zao hili limetuingizia zaidi ya sh mil 900 kitu ambacho hakijawahi kutokea katika Kijiji chetu, na kila mkulima alipata fedha zake zote kulingana na kilo alizozalisha, mimi nilipata zaidi ya sh mil 10, sio haba’, amesema.

Afisa Utafiti wa Taasisi hiyo Magdalena Raphael ameshukuru serikali ya awamu ya 6 chini ya Uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Taasisi hiyo zaidi ya sh mil 200 kwa ajili ya kuzalisha mbegu bora na kuzigawa kwa wakulima.

Amesisitiza kuwa mbali na kugawa mbegu zilizofanyiwa utafiti wa kina pia walitoa elimu ya matumizi sahihi ya mbegu hizo hivyo kuwezesha wakulima wote waliotumia mbegu hizo kupata kilo za kutosha za zao hilo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt Jacob Bulenga Lisuma ameeleza kuwa utafiti wa Taasisi hiyo umekuwa msaada mkubwa sana kwa wakulima wa kata hiyo, Mkoa wa Tabora na Mikoa mingine.

Amebainisha kuwa kwa msimu uliopita pekee takribani kilo mil 122 za zao hilo zilizalishwa hapa nchini kutokana na elimu ya matumizi ya mbegu bora iliyotolewa na wataalamu wa Taasisi hiyo.

Dkt Bulenga amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Haassan kwa kuendelea kuboresha utendaji wa Taasisi hiyo kwa kuwapatia vifaa vya maabara (mashine ya Polymerized Chain Reaction-PCR) kwa ajili kupima ubora wa mbegu za zao hilo.

Amesisitiza kuwa lengo la Taasisi hiyo ni kuwapa wakulima elimu sahihi ya kilimo cha zao hilo na kuwashauri kutumia mbegu bora zilizofanyiwa utafiti wa kina ili kuongeza uzalishaji na kuinua maisha yao.

Ili kilimo hicho kiwe na tija kubwa na kuinua maisha yao amewataka kuzingatia ushauri na elimu wanayopewa na kutumia mbegu zilizofanyiwa utafiti na kuidhinishwa na Wataalamu wa taasisi hiyo.